BARACK Obama ametua Afrika. Mguu wake wa kwanza ameukanyagia Senegal. Neno lake kuu akiwa Senegal ni DEMOKRASIA. Ameisifu Senegal kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kukuza demokrasia barani Afrika.
Kisha ametua Afrika Kusini. Jana Jumamosi ametembelea Kisiwa cha Robben, mahali ambapo Nelson Mandela alifungwa kwa miaka 27. Inahusu DEMOKRASIA. Bila shaka, Obama ataisifu Afrika Kusini kwa kukuza demokrasia yake na hivyo kuinua uchumi wake. Maana, pasipo na demokrasia ni nadra kwa uchumi kukua.
Kesho Barack Obama atatua Dar es Salaam, Tanzania. Huhitaji kuwa mtabiri, kujua , kuwa Barack Obama atalitamka neno DEMOKRASIA akiwa Tanzania.
Huenda Obama akaitaja Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha Amani na Umoja miongoni mwa watu wake.
Lakini, bado Obama atasisitiza pia umuhimu wa demokrasia na uhuru zaidi wa vyombo vya habari barani Afrika.
Obama anaipenda Afrika, ni bara alilozaliwa baba yake mzazi, Dk Barack Hussein Obama. Hivyo, kwa Barack Obama, Afrika ni bara la asili yake na Kenya ndiko iliko asili yake. Ndiko liliko kaburi la baba yake.
Lakini, Obama ana simulizi mbaya juu ya bara hili na hususan inapohusu demokrasia na uhuru wa watu kujieleza. Obama hahitaji kutoa mifano ya wengine anapozungumzia waathirika wa kukosekana kwa demokrasia. Obama ana mfano wa baba yake mwenyewe wa kumzaa; Dk Barack Hussein Obama.
Baba yake alikufa kwenye ajali ya gari Nairobi, lakini, ni matokeo ya kuandamwa na mfumo kwenye Serikali ya Mzee Jomo Kenyatta, kwa vile tu, baba yake Obama alikuwa anafikiri tofauti na watawala.
Na mwishowe alikuwa anatembea na siri ya aliyemwua mwanasiasa Tom Mboya. Aliitwa na mamlaka na akaambiwa; ” Funga Mdomo!”
Baba yake Obama alikuwa rafiki wa karibu sana wa Tom Mboya aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha. Lakini, inaaminika, aliuawa kwa vile alifikiri tofauti na watawala.
Kwenye kitabu kiitwacho; ’ The Bridge’ kilichoandikwa na mwandishi David Remnick, mwandishi anaelezea siku ambayo Jomo Kenyatta alifika Kisumu na kupokewa na kelele za wananchi wakimwuliza;
” Tom yuko wapi?” ” Tom yuko wapi?”
ambo hilo lilimwaibisha sana Jomo Kenyatta. Akalaumu chama cha Jaramong Odinga cha KPU- Kenya People’s Union kwa kuwagawa wananchi. Naye Rais Jomo Kenyatta akatamka hadharani; ” Odinga ni rafiki yangu, lakini anawapotosha wananchi na anaendelea kuwapotosha watu wa eneo hili. Tutawapondaponda muwe kama unga. Yeyote anayecheza na maendeleo yetu tutamwangamiza kama nzige. Msije mkasema sijawaonya.”
Baada ya hapo gari la Jomo Kenyatta liliondoka mahali hapo kwa kasi huku umati ukilirushia mawe.
Polisi hawakurusha mabomu bali, walielekeza mitutu yao ya bunduki kwenye umati ule . Watu tisa walikufa hapo hapo na wengine sabini kujeruhiwa.
Siku mbili baadaye Jomo Kenyatta akawakamata Jaramongi Odinga na viongozi wengine kadhaa wa KPU. Walishtakiwa kutaka kumpindua Rais Jomo Kenyatta. Odinga akawekwa jela kwa miaka miwili na kila msomi mwenye asili ya Kijaluo alionja joto ya jiwe. ( The Brigge, David Remnic, page 67-68)
Ndiyo maana ya kusema, kuwa hayo machache tu kwenye simulizi mbaya ya Obama juu ya Afrika, yanamfanya Barack Obama kuwa wakili mtetezi wa kweli wa kupigania demokrasia katika Afrika.
Obama anaposisitiza umuhimu wa uwepo wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari barani Afrika anamaanisha anachosema na hasemi asichomaanisha.
Na hapa tuyakumbuke maneno ya Obama pale alipotoa hotuba ya kutawazwa kuwa Rais wa Marekani kwa mara ya pili. Obama alisema;
” Taifa la Marekani ni mahali ambapo kila mmoja ana nafasi ya kutimiza ndoto yake.
Ndoto ya kuwa yeyote yule, bila kujali rangi, dini au jinsi yako. Wakati tukiyaongea haya hapa, kuna wanadamu wenzetu mahali pengine duniani wako gerezani kwa kosa la kufikiri tofauti. Kwa kosa la kuonyesha dhamira ya kutimiza ndoto zao.”- Barack Obama.
Naam, kuna mahali fulani hata Barack Obama anajua, kuwa kama angeliishi Kenya, kwenye nchi ya baba yake na kuwa na ndoto ya kuwa Rais wa Kenya. Akaitamka hadharani na kuonyesha kwa matendo basi, huenda, siyo tu angefungwa gerezani kwa kufikiri tofauti na watawala bali, huenda leo angeshakuwa amezikwa kando ya kaburi la baba yake kule Kerego Kisumu, Kenya.
Ndiyo maana, tunaamini, kuwa kauli za Barack Obama kuhusu demokrasia ni za dhati na aendelee kuwa wakili wa kweli wa kutetea demokrasia kwenye bara la asili ya baba yake. Ni kwa vile, bila uwepo wa demokrasia ikiwamo uhuru wa kujieleza, Afrika itabaki kuwa bara la giza. Tuna nafasi na kila sababu za kurudisha nuru kwenye bara hili.
Karibu sana Tanzania, Barack Obama. Mungu Ibariki Afrika.
Maggid Mjengwa
Iringa
No comments:
Post a Comment