Gazeti la uchunguzi la The Sunday
Independent la Afrika Kusini limesema mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe Mandela
na binamu yake, Ndileka wapo kwenye mipango ya kupata fedha kutoka kwa
Televisheni ya CNN wakati wa mazishi ya baba yao.
Mmoja wa maofisa wa Shirika la
Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) ambaye pia alishiriki mkutano huo
alikaririwa akisema kwamba Makaziwe na Ndileka walikaa katika mkutano wa siri
mwishoni mwa Juni mwaka huu pamoja na maofisa wa shirika hilo na Ofisi ya Rais
ili kupanga jinsi ya kuyarusha matangazo ya mazishi ya kiongozi huyo kwa vyombo
vya kimataifa.
Hata hivyo, Mwakilishi wa CNN
Johannesburg, Kim Noorgard alisema hafahamu chochote kuhusu suala hilo.
The Sunday Independent liliwatafuta
viongozi wa CNN wa makao makuu jijini Atlanta, Marekani lakini hawakupatikana
kuzungumzia suala hilo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo,
Makaziwe alikataa kuzungumza lolote na kumtaka mwandishi kuwataja maofisa wanaoelezwa
kwamba walizungumza nao.
“Hadi uniambie nani amekwambia
habari hii ndipo nitakujibu unachotaka kufahamu,” alisisitiza Makaziwe.
“Niambie nani kakwambia,” alizidi
kuomba. “Huo ulikuwa mkutano wa siri na sidhani kama kuna kitu cha kuongelea
hapo.”
Ndileka naye alikataa kuzungumza
lolote kuhusu mkutano ule.
Ripoti ya mkutano huo ilieleza kuwa
majadiliano makuu yalikuwa ni kwa namna gani mazishi ya Mandela yatarushwa
hewani lakini watoto wa Mandela walilazimisha CNN wapewe haki ya kurusha
matangazo ya mazishi hayo.
Mmoja wa maofisa hao aliyehudhuria
mkutano aliyaponda mazungumzo hayo na kusema kuwa hayafai kutoka katika vinywa
vya wanafamilia ambao wanazungumzia kifo cha baba yao wakati akiwa bado yupo
hai.
“Wanataka kupata fedha kutoka
mashirika ya kimataifa na ndiyo maana wanapanga mipango hiyo. Kama Serikali
hatuna cha kufanya kwa sababu inaonekana wanafamilia tayari wana mipango yao,”
alisema afisa huyo.
Ilibainika kuwa tayari CNN walikuwa
wameshafanya mazungumzo na wanafamilia hao na kukubaliana.
Mandla avuliwa uchifu
Mfalme wa Kabila la Thembu,
Zwelibanzi Dalindyebo amemwondoa Mandla Mandela katika wadhifa wake wa uchifu.
Mandla anatuhumiwa kuivuruga familia
yake baada ya kuhamisha makaburi matatu ya watoto wa babu yake, Nelson Mandela.
Alihamisha makaburi hayo kutoka Qunu
na kuyapeleka katika Kijiji cha Mvezo mwaka 2011 yaliko makazi yake.
Miili ya watoto hao ilirudishwa Qunu
baada ya familia ya Mandela kwenda mahakamani kuomba na kukubali kumlazimisha
Mandla airudishe miili hiyo.
Mfalme Dalindyebo alisema kuanzia
sasa Mandla hataruhusiwa kujihusisha na masuala ya kabila hadi aombe radhi.
“Kitendo alichofanya kimeudhi watu
wengi wa kabila letu na hatutaki kumuona akijihusisha na masuala ya familia ya
Mandela.”
Mandela amelazwa hospitalini mwezi
mmoja sasa na mvutano wa familia yake umeishtua dunia.
Mandla alitaka Mandela azikwe Mvezo
kwa maelezo kwamba ndiko alikozaliwa lakini habari nyingine zinadai kwamba
alitaka kunufaika kifedha kutokana na watu ambao wangekwenda kutembelea kaburi
la Mandela.
Mandela aliacha wasia kuwa
atakapofariki azikwe karibu na makaburi ya wanae.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment