Rais wa Simba Aden Rage (kushoto) akipeana mkono na mwakilishi wa Azam huku mwanasheria wa Azam akishuhudia mara baada ya kusaini mkataba wa mil 331 wiki iliyopita. |
Wiki
iliyopita timu kongwe ya soka nchini Simba SC iliingia mkataba mnono wa mil 331
na Azam Media Group ili kuweza kuitumia Simba TV kurusha matukio mbalimbali ya
timu hiyo wakati huohuo watapata faida
ya kutangaza biashara zao.
Siku zote waswahili
husema penye fungu ndipo huenda nyongeza lakini watu husahau kuwa anayehangaika
ndiye anayepata.
Wapinzani
wakubwa wa Simba yaani Yanga nawo walipata kuingia kwenye mazungumzo na Azam
Media Group ili kupata mkataba aina hiyo ila haijulikani mazungumzo yao
yameishia vipi. Ila kikubwa ni dalili za wazi kuwa vilabu vya soka
Tanzania vinaanza kuendeshwa kwa faida.
Hili ni somo
kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara kutafuta wadhamini
watakaowapa kipato kikubwa kitakachowawezesha kujenga majengo ama kuanzisha
miradi itakayowasaidia kupata fedha za
kuendesha timu kwa mwaka mzima, bila kutegemea fedha za mlangoni ambazo hazina
uhakika.
Fedha
inayopatikana lazima itumike kutengeneza fedha, Simba na Yanga wamejaaliwa
kupata busara hiyo ya kuwekeza kwenye soka kwa kuendeleza vyanzo vya mapato.
Kingine ni kuwa na uongozi uliokamilika ambapo kunakuwa na ofisi zilizo hai
zenye kushughulikia masuala ya fedha, miradi, usajili, kuuza taswira ya timu
ndani na nje ya nchi na kamati maalum inayokutana na wafadhili kujadili thamani
ya timu.
Hapa ndipo
timu nyingine zinaposhindwa, mfadhili lazima aangaliwe kiwango anachonufaika
kwa kutangaza biashara yake kwenye vifua ama migongo ya wachezaji, timu nayo inanufaika
kwa kiwango hichohicho?
Huu si wakati
wa kun’gan’gania wafadhili bali timu zinahitaji kupata wadhamini watakaoingia
mikataba na timu ili iwepo ‘win win
situation’ timu inufaike na mdhamini anufaike.
Kwa kipindi
kirefu nembo ya Yanga ilitumika vibaya, wajanja waliuza bendera, fulana na
vifaa vingine vyenye nembo ya Yanga. Mpaka miezi michache ilipopita baada ya
watu wenye akili kukaa na kujadili uhalali wa watu kuitumia vibaya nembo ya
timu, ndipo ikapitishwa hoja kuwa nembo lazima iiletee faida timu.
Yanga sasa
wanazungumza kuhusu kujenga uwanja utakaoingiza watazamaji 40,000 hicho ni
kitega uchumi kikubwa kitakachowaingizia mapato mengi kwa mwaka mzima.
Viongozi wa
timu zinazoshiriki ligi kuu wafunguke macho katika hili, ligi ya Tanzania muda
si mrefu itaingia kwenye orodha ya ligi zinazorushwa kwenye kituo maarufu cha
luninga Supersport. Wadhamini lazima watambue gharama ya kutangaza biashara zao
kwenye luninga inayorusha matangazo dunia nzima.
HAFIDH KIDO
23 JULAI,
2013
No comments:
Post a Comment