Monday, July 15, 2013

Mnyika aitupia lawama CCM juu ya sera zake mbovu za michezo.



 
Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema ukosefu wa maandalizi ya mapema katika micheo kunatokana na sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiko kunakoibua matokeo mabovu katika sekta hiyo hususan kwa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, aliyasema hayo jana wakati akizindua michuano ya Mama Kevin Cup kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe (DUCE), jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema katika ilani ya uchaguzi ya Chadema 2010, waliahidi masualaya michezo hususan Tanzania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia Brazil mwakani endapo wangekabidhiwa cnchi, lakini kutokana na baadhi ya maeneo kutowataka waingie serikali mpya, hayo yameshindikana chini ya sera mbovu za CCM.


“Matumaini yanazidi kufifia nah ii inachangiwa na mengi. Ili michezo yetu ifanikiwe yanatakiwa maandalizi ya muda mrefu kwa kuibua na kuendeleza vipaji vya kuanzia ngazi za chini huku mchangani, kama ambavyo nyinyi mnafanya kwa kuandaa mashindano kama haya, nawapongeza sana na sisi Chadema Taifa tunawaunga mkono” alisema na kushangiliwa.

Aliongeza kuwa pia tatizo la miundombinu ndilo linalochangia kudorora kwa michezo hapa nchini, kwani viwanja vingi vilivyojengwa enzi za chama kimoja vimehodhiwa na CCM na hata yale maeneo ya wazi yameuzwa.

“Miundo mbinu si kuwa na kiwanja kikubwa kama hiki (Taifa), ni pamoja na vile vya mitaani ambavyo watoto wetu wanatakiwa kuwa wakicheza ili kuibua na kuendeleza vipaji vyao, lakini vimeuzwa na kusababisha matokeo haya mabaya tunayoyapata hivi sasa, mfano mechi iliyopita ya Taifa Stars na Uganda ni matokeo ya maandalizi hafifu. Tushirikiane jamani 2015 tuiingize serikali kusimamia michezo” alisema.

Michuano hiyo ambayo imeandaliwa na Edith Bunjora maarufu kama Mama Kevin, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Chang’ombe inashirikisha pia michezo ya kuvuta kamba na kukimbiza kuku.

Inashirikisha timu kutoka kata zote za Manispaa ya Temeke. Timu hizo ni Senet FC, Inter Milan, Ubaya FC, Corner Boy, Umoja FC, Amka Force, Scud, Panama, Mseto, Tandika, Professional na Masota FC.

Chanzo: Gazeti la TanzaniaDaima Toleo Na. 3146 Jumatatu Julai 15, 2013 ISSN 08569760 Uk. 23

No comments:

Post a Comment