Friday, July 12, 2013

Mgomvi wa Rais Zuma katika ANC aanzisha chama chake.



Julius Malema
 
Aliyekuwa kiongozi wa vugu vugu la vijana la chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC, Julius Malema amezindua kundi la kisiasa litakalojulikana kama Wapiganiaji wa Uhuru wa Kiuchumi au Economic Freedom Fighters, EFF.
Malema, ambaye alitimuliwa kutoka kwa chama cha ANC, mwaka wa 2012, amesema chama chake cha EFF kinataka zoezi la kugawanya mashamba kuanzisha upya na pia kutaifishwa kwa migodi yote ya madini.
''Tutagawana ardhi sisi zote ukiwa mweusi au mweupe. Lakini ukikataa kugawanya itamaanisha kuwa utalazimishwa kufanya hivyo'' Alisema Bwana Malema.
Ametaja dhamira kuu ya vugu vugu hilo kuwa kupamabana mfumo wa kipebari.
Akiwa amevalia kofia nyekundu iliyo na maandishi ''Amirijeshi Mkuu wa EFF'' Bwana Malema amewaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kimebuniwa ili kutetea maslahi ya raia wanaoteseka katika maeneo ya mashinani.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
 
Malema ambaye alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa rais Zuma, kwa sasa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa na aliongoza mikakati ya kumuondoa kama kiongozi wa chama cha ANC wakati wa mkutano wa baraza kuu la chama hicho mwaka wa 2012.
Malema ameshutumu rais Zuma kwa kutoimarisha juhudi za kuwasaidia raia weusi wa nchi hiyo ambao ni masikini na waliompigia kura.
Hata hivyo haijabainika ikiwa atawania kiti chochote katika uchaguzi mkuu utakaoandaliwa mwaka ujao, akisema kuwa uamuzi huo utatolewa baada ya mkutano wa baraza kuu la chama hicho cha EFF utakaofanyika mwisho wa mwezi huu.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema idadi kubwa ya raia wa Afrika Kusini, wamepoteza imani na chama cha ANC, ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka wa 1994.
Rais wanasema maafisa wengi wa chama hicho ni wafisadi na hawana nia ya kuimarisha hali ya maisha.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment