Sunday, June 2, 2013

Boban mchezaji halali wa Coastal Union: Binslum.

Dar es Salaam. Kiungo mwenye mikasa na vituko vingi, Haruna Moshi ‘Boban’ amejiunga na Coastal Union ya Tanga kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku Simba wakikanusha kutaka kumsajili Mganda Hamisi Kiiza wa Yanga.

Hivi karibuni uongozi wa klabu ya Simba ulitangaza kuwatema wachezaji wao wanane akiwamo Moshi ‘Boban’ kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Mfadhili Mkuu wa Coastal Union, Nassoro Binslum alisema klabu yake imekamilisha usajili wa Boban, ambapo sasa ni mchezaji wake halali.

“Boban ni mchezaji halali wa Coastal Union na hii ni baada ya mimi na yeye kumalizana leo yaani kwa kifupi nimemsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja,” alisema Binslum.

Kuhusu dau alilompa Boban hadi kusaini Union, Binslum hakutaka kuweka wazi kwa madai kwamba uswahiba baina yao ndiyo ulifanikisha zoezi hilo siyo fedha.

“Siwezi kutaja kiwango cha fedha nilichompa kwa sababu urafiki wetu ndiyo uliomleta kwetu ingawa siyo kwamba amekuja bure kabisa kuna kiasi nimempa,” alisema Binslum.

Alisema kuwa, klabu yake itakuwa tayari kumwongezea mkataba zaidi Boban endapo ataonyesha kiwango cha kuridhisha uwanjani.

“Tumeanza naye kwa mkataba wa mwaka mmoja ili tuangalie mchango wake kama atatusaidia tutamwongeza mwingine, lakini tusiporidhika basi tutakuwa tumemalizana,” alisema Binslum.

Wakati huohuo; Uongozi wa Simba umekanusha kutaka kumsajili mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza.

Awali kulikuwa na tetesi kuwa Kiiza atajiunga na timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi Kariakoo baada ya kumaliza mkataba wake na mabingwa wa Tanzania, Yanga.

“Hatujafanya mazungumzo na Kiiza ili kutaka kumsajili acheze Simba msimu ujao,” alisema Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala.

Kwa mujibu wa kigogo huyo wa Simba hivi sasa klabu yao inajipanga kusajili wachezaji watakaoisaidia timu hiyo kutwaa kombe la ligi msimu ujao baada ya kuvuliwa ubingwa na Yanga msimu huu.

“Kila kitu ni mipango kwa suala la usajili hatuwezi kukurupuka tunaangalia nani hatatufaa na je anastahili kucheza Simba na vinginevyo,” alisema Mtawala na kusisitiza katika usajili wao Kiiza hana nafasi.

Kiiza amekataa kusaini mkataba mpya Yanga, baada viongozi wa mabingwa hao kugoma kumpa dau kama walilompatia Haruna Niyonzima aliyesaini mkataba mpya wa miaka miwili kwa gharama ya Dola 50,000 pamoja na kulimpa mshahara wa Dola 3,000 kwa mwezi.   

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment