Dar es Salaam. Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana ilizindua rasimu ya Katiba Mpya inayopendekeza kuwapo kwa mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa utawala, yakiwamo ya kuwa na Serikali Tatu; Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar.
Mabadiliko mengine yaliyosheheni kwenye rasimu hiyo ni kufutwa kwa viti maalumu vya ubunge, suala la maadili ya viongozi wa taifa, umri wa urais kubaki kama ulivyokuwa na kuruhusiwa kwa wagombea binafsi katika ngazi zote; urais, ubunge, udiwani mpaka ngazi za mitaa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema Tume pia imependekeza kuingizwa kwenye Katiba Mpya mambo kadhaa kama Tunu, Dira na Misingi ya Taifa.
“Tulitaka kuifanya rasimu hii iwe fupi kadri iwezekanavyo, lakini kutokana na wingi wa maoni tumeifanya iwe na Ibara 240. Katiba ya sasa ina Ibara 152,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tumeendelea kuitambua misingi mikuu minne ya taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Lakini pia tukaongeza misingi mingine mitatu ambayo ni Usawa, Umoja na Mshikamano. Tumependekeza Katiba yetu mpya iwe na misingi saba.”
Jaji Warioba alisema Tume pia imetambua mambo kadhaa kuwa ni Tunu za Taifa: “Tunu ya kwanza ni Utu. Tunaamini kuwa watu wote ni sawa, tusiwe na ubaguzi wala tofauti zozote. Tunu nyingine ni Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi Uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili.”
Jaji Warioba alisema pia kuwa Tume imebainisha malengo ya Taifa ambayo yatakuwa mwongozo wa Mihimili ya Dola; Serikali, Bunge na Mahakama.
“Malengo hayo yatakuwa ya aina mbalimbali. Kuna malengo ya kisiasa, kiuchumi, kimazingira na mengine mengi yatakayofafanuliwa baadaye,” alisema.
Jaji Warioba alisema Tume pia imependekeza Katiba ijayo ionyeshe wazi maadili ya kijamii, kiutawala na kiuongozi.
“Tumependekeza kuwapo maadili ya viongozi, miiko na kiundwe chombo cha kusimamia maadili. Tunapendekeza sekretarieti ya maadili ya viongozi iliyopo, iwe tume kamili,” alisema.
Muundo wa Serikali Tatu
Jaji Warioba alisema baada ya kupitia maoni mengi, Tume imeridhika kwamba inafaa Tanzania iwe na mfumo wa Serikali tatu, yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Tumependekeza Serikali ya Muungano iwe na mawaziri wasiozidi 15 na wabunge 75. Wabunge 50 kutoka Bara, 20 Zanzibar na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais,” alisema wabunge wa kuteuliwa watatoka katika kundi la watu wenye ulemavu tu.
Alisema Serikali hiyo ya Muungano itakuwa inaongozwa na Rais Mtendaji. Alitaja mambo yatakayoingia kwenye Muungano kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mikutano 1,942
Jaji Warioba alisema rasimu hiyo ya Katiba imekamilika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na watu 1,306,500.
“Watu 395,000 walitoa maoni ya ana kwa ana na makundi 160 maalumu yalitoa maoni yao. Pia tulizungumza na viongozi wa kitaifa; walioko madarakani na wastaafu. Viongozi 43 walitoa maoni,” alisema.
Jaji Warioba alisema baada ya maoni hayo, walikuwa na miezi mitatu kuyachambua na kuandaa rasimu ya Katiba, lakini wakalazimika kuongeza muda huo hadi Mei mwaka huu.
“Kutokana Sheria, Rasimu hii itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali na baadaye kwenye magazeti kabla ya Mabaraza ya Katiba kuanza kazi,” alisema Jaji Warioba .
Alisema mchakato huo wa Mabadiliko ya Katiba ulioanza kwa Sheria iliyotungwa Novemba 2011 na baadaye kufanyiwa mabadiliko Februari 2012, umepangwa kumalizika ndani ya miezi 18... “Hivyo Tume imekusudia kumaliza mchakato huo Novemba Mosi mwaka huu,” alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment