Sunday, June 23, 2013

UTATANISHI NA UKIMYA KATIKA RASIMU YA KATIBA MPYA Issa Shivji: MHADHARA WA KUAGA KIGODA CHA MWALIMU KIGODA CHA TAALUMA CHA MWALIMU NYERERE.

                                                                    Prof. Issa Shivji

UTATANISHI NA UKIMYA KATIKA
RASIMU YA KATIBA MPYA
Issa Shivji
MHADHARA WA KUAGA KIGODA CHA MWALIMU
KIGODA CHA TAALUMA CHA MWALIMU NYERERE

Copyright © Issa Shivji, 2013
Kwa dhati kabisa ningependa kuwashukuru wanakigoda
wenzangu, Ng’wanza Kamata, Saida-Yahya-Othman na
Bashiru Ally, kwa mazungumzo marefu na mabishano
makali ambayo yamenisaidia

kunoa hoja zangu na kuwaza
yasiyowazika. Shukrani zangu kwa Walter Rodney Luanda na
Bashiru Ally, waliosimamia uchapishaji wa Mhadhara katika
muda mfupi wa siku mbili. Walter amekuwa bega kwa bega
nami kwa miaka mitano yote ya uNyagoda wangu. Amefanya
kazi za Kigoda kutokana na imani na msimamo wake na sio
kiajira tu.
Mwishowe, namshukuru sana, kwa moyo mkunjufu, Saida
Yahya-Othman ambaye amehariri Mhadhara kwa ustadi wa
mtaalam wa lugha katika masaa ishirini na nne, tena katika
siku yake ya mapumziko maalum.
Shukrani
1. Naialika kaumu, tutafakari pamoja,
Kuhusu Tunu muhimu, Rasimu ilizotaja,
Kati ya Tunu adhimu, mojawapo ni umoja,
Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu
2. Umoja hauwi Tunu, Kwa taifa tegemezi,
Bali umoja ni Tunu, baada ya ukombozi,
Umoja hasa ni mbinu, ya kuunda mapinduzi,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
3. Uchumi wa nchi yetu, ni uchumi tegemezi,
Na hasa kilimo chetu, siyo cha kimapinduzi,
Na pia elimu yetu, ni chombo cha ubaguzi,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
4. Tanzania nchi yetu, sasa haina amani,
Uhuru na utu wetu, kwa sasa viko rehani,
Fikra na mila zetu, havina tena thamani,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu,
5. Tutafakari maoni, ya waliotangulia,
Ya Mkwawa na Fanoni, na ya Bibi Titi pia,
Umoja walithamini, hoja waliujengea,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
6. Umoja imara hasa, siyo uliopo sasa,
Huu umoja wa sasa, ni umoja wa mikasa
Mikasa ya kisiasa, na hila za wenye pesa,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
7. Umoja si mapatano, baina ya wala tonge,
Umoja si mikutano, ya Jangwani na Kisonge,
Umoja ni muungano, wa tabaka la wanyonge,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu,
8. Umoja sio ubia, wa mitaji ya ‘mabwana’,
Umoja ni ujamaa, wa watu wasonyonyana,
Umoja kwa wenye njaa, ni nyenzo muhimu sana,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
9. Mhimili wa umoja, ni dira ya ukombozi,
Na adui wa umoja, ni mifumo kandamizi,
Na kitanzi cha umoja, ni sera za kibaguzi,
Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.
10. Tunataka ukombozi, wa fikra za wanyonge,
Tunataka mapinduzi, ya uchumi wa wanyonge,
Tunataka mageuzi, ya Umoja wa wanyonge
Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu
UMOJA
HAUWI TUNU,
KABLA YA
UKOMBOZI
– Na Mwalimu Bashiru Ally
5
UTANGULIZI
Niliposimikwa mnamo tarehe 18 Aprili 2008 kuwa Profesa wa
Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa
Afrika, nilitoa mhadhara wa uzinduzi juu ya ‘Umajumui wa Afrika
katika Fikra za Mwalimu’. Sasa ninakaribia kumaliza muda wangu
hapo tarehe 31 Agosti 2013, nimeona si vema nikiondoka bila
kutoa mhadhara wa kuaga Kigoda, wanakigoda na wanachuo
wenzangu, na wale wote waliokuwa pamoja nasi katika shughuli
na mijadala yetu.
Tumepanga mhadhara huu mapema kidogo kwa sababu mbili.
Moja, wanafunzi, vijana wa Kigoda, wanaondoka leo kwenda
kwenye likizo yao. Ya nini kutoa mhadhara wakati wenyewe
hawapo? Pili, mapema mwezi ujao, pamoja na wasomi wenzangu
wawili, tumejipangia kwenda nje ya nchi kufanya utafiti wa
kuandika wasifu (biography) wa Mwalimu. Kwa hivyo, tukaona
tarehe ya leo ni mwafaka.
Nimegawa mhadhara huu katika sehemu kuu nne. Hoja yangu
ambayo itaeleza udhani (hypothesis) wangu ulioniongoza
kuchambua Rasimu ni sehemu ya kwanza. Sehemu ya pili
itazumgumzia dhana ya ‘ukuu wa katiba’ ya shirikisho, yaani
supremacy of the federal constitution. Kwa kirefu kidogo, ‘moyo’
wa rasimu, yaani muundo na taasisi za muungano, nitazichambua
katika sehemu ya tatu. Sehemu ya mwisho, ambayo ni ya nne,
kabla sijahitimisha mhadhara wangu, itakuwa juu ya matumaini
ya wananchi ya Tanzania Mpya.
6
I. HOJA
Awali ya yote ningependa kuweka wazi, mosi, mtazamo wangu
utakaoniongoza katika kuchambua Rasimu ya Katiba Mpya; pili,
jambo ambalo ninaliona kuwa ni ‘moyo wa Katiba,’ na tatu udhani
(au hypothesis) wangu.
Mtazamo
Kwanza, kwa wananchi walio wengi, mchakato wa Katiba mpya
ulitoa matumaini ya mwanzo wa kujenga Tanzania Mpya: nchi
na jamii zitakazojikita kwenye kujali wavuja jasho, zenye msingi
wa haki ya kijamii (social justice), na sio tu haki ya kisheria (legal
justice). Tulitarajia kwamba tutatafakari kwa makini hali halisi
ya watu wetu kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita ambacho
kimetufikisha kwenye hali hii ya leo. Tulifikiri tutatafuta njia
mbadala itakayorudisha imani na matumaini ya watu katika
mifumo yetu ya utawala, siasa na uchumi - mfumo unaoweka
mazingira na nafasi pana kwa wananchi walio wengi kuendeleza
mapambano yao ya kujikomboa.
Kwa dhati kabisa, tungechagua njia mbadala itakayojenga
mshikamano palipo na utengano; itakayotuelekeza kwenye usawa,
palipo na mpasuko wa kitabaka, itakayo imarisha Muungano
kwa mtazamo wa Umajumui wa Afrika, palipo na mwelekeo
wa kurubuni wananchi na kugawanya madaraka. Na tulitarajia
kwamba Katiba Mpya itatangaza rasmi matumaini haya na
dhamira hii bila kupinda dhana au kutafuna maneno.
Haya ndio yalikuwa matumaini yetu ya Katiba Mpya na haya ndio
yatakayoniongoza katika kuchambua Rasimu. Ila nitatumia pia
utaalaam wangu wa kisheria, nilioupata kutokana na wananchi
wenyewe waliogharimia elimu yangu. Huu ndio mchango wangu
mdogo kwa jamii iliyonilea.
7
‘Moyo wa Katiba’
Pili, moja kwa moja, niseme kwamba moyo wa katiba yetu, au
mchakato wowote wa kuwa na katiba mpya, ni Muungano. Hili
linatokana na hali halisi ya kihistoria ya katiba zetu. Suala la
Muungano ndilo limesheheni mambo muhimu ya mfumo wa
kidemokrasia na jamii. Kwa hivyo, muundo wa Muungano sio
suala la idadi ya serikali – moja, mbili, tatu, mbili na nusu n.k. –
bali ni suala la demokrasia.
Isitoshe, maoni yaliyokuwa yanakusanywa yalikuwa juu ya Katiba
ya Muungano, wala sio katiba ya Tanganyika au katiba ya Zanzibar.
Na Rasimu iliyokabidhibiwa kwetu kwa ajili ya kujadiliwa pia ni
Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hivyo,
uchambuzi wangu, kwa sehemu kubwa, ni kuhusu Muungano.
Udhani (hypothesis)
Baada ya kuisoma Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba
masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya
mivutano mikali katika Tume. Bahati mbaya hatuna mwenendo wa
majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, hata taarifa ya awali.
Lakini usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii
ni maelewano kwa maana ya compromise, na sio mapatano, au
mwafaka, kwa maana ya consensus. Nijieleze kidogo.
Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye
zinakubali kwa shingo upande ili kutokukwamisha maamuzi.
Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande
huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili.
Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi.
Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege.
Mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano
yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga
kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake
8
kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka,
kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika
compromise, kila mmoja anatoka amenuna. Ni wazi kwamba
huwezi ukapata mwafaka fastafasta. Lazima utachukua muda.
Ili nieleweke vizuri, nitoe mifano miwili, mmoja mwepesi,
mwingine mzito. Ib. 1(3) ya Rasimu inasema:
Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika
Ibara ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri
itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa
Makubaliano hayo.
Maana ya aya hii ni:
Hati ya Makubaliano ya 1964 ni msingi wa Katiba hii (yaani
Rasimu); na
Katiba hii ni mwendelezo wa Makubaliano.
Ukiangalia kwa jicho la kisheria, , ukisema Hati ndio msingi, maana
yake ni kwamba Hati bado inaendelea kuwa na nguvu ya kisheria
na ndio sheria kuu inayotawala Katiba. Lakini Hati iliweka serikali
mbili; sasa, iweje rasimu inayozungumzia serikali tatu iwe na
msingi ambao ulijengeka kwenye serikali mbili?
La pili, Katiba iliyojikita kwenye serikali tatu haiwezi, kwa vyovyote
vile, ikawa mwendelezo wa Hati.
Ni kweli kabisa kwamba Hati ya Makubaliano ya 1964 ni chanzo
cha Muungano. Historia hii, kama inavyostahili, imewekwa kwenye
Utangulizi. Lakini masharti ya katiba yenye nguvu za kisheria
hayawezi tena kurudia historia. Ukitaja maneno kama haya katika
masharti ya Katiba, kimahakama inachukuliwa kwamba nia yako
ilikuwa kuipa Hati nguvu ya kisheria. Nina uhakika kabisa kwamba
haikuwa nia ya Tume kuifufua Hati ya 1964 na kuipa nguvu ya
kisheria.
9
Pia, ninaamini kabisa kwamba Tume iliyosheheni wanasheria
wazoefu na waliobobea huenda walijua na kuelewa kabisa
walichokuwa wanaandika. Kwa hivyo, haiwezekani kwamba
walikosea, au kuteleza, bali ilikuwa ‘kusalimu amri’ na “kuelewana”
ili mambo yaendelee. Ndivyo tulivyopata ibara legalege ambayo
kisheria haina kichwa wala mkia.
Inawezekana kabisa kwamba ibara hii isiwe na madhara makubwa
kwa sababu majaji wenye busara, kwa hakika, hawatatia maanani
sharti kama hili. Lakini unaweza kupata jaji ambaye anaegemea
zaidi kwenye ufundi na kuitafsiri ibara hii kama ilivyo. Madhara
yake yanaweza kuwa makubwa. Vyovyote vile, ibara kama hii
isiyoeleweka inashusha hadhi ya Katiba.
Mfano wa pili, mzito zaidi, ni kuhusu mipaka ya madaraka. Eneo
la utawala wa Serikali ya Shirikisho limetajwa kuwa ‘eneo lote la
Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote
la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari’ (ib. 2). Lakini
eneo la utawala wa serikali ya Bara na serikali ya Zanzibar
halikutajwa. Bila shaka, katiba za Washirika zitataja maeneo yao
na kuna uwezekano mkubwa kwamba kutakuwa na msuguano
na kutoelewana hasa juu ya mipaka ya bahari katika ‘Zanzibar
channel’. Katiba ya Zanzibar ya Mwaka wa 1984 iliopo, kwa mfano,
inataja mipaka ya Zanzibar kuwa ni ‘eneo lote la Visiwa vya Unguja
na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake
ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.’ (ib.1)
Pande mbili za Muungano zimewahi kutofautiana kuhusu eneo
lao la bahari, hasa kwa sababu inadhaniwa kwamba bahari
inayopakana na maeneo ya Tanganyika na Zanzibar ina mafuta na
rasilimali nyingine. Waziri Tibaijuka alipopeleka ombi Umoja wa
Mataifa kuongeza eneo la nchi kwa maili 150, mjumbe mmoja wa
Baraza la Wawakilishi aliwasilisha hoja binafsi kumlaumu Waziri
10
wa Zanzibar mhusika kwa kuridhia ombi hilo. 1
Ukimya wa Rasimu juu ya kueleza kwa uwazi mipaka ya utawala
wa Washirika ni wa ajabu kweli kwa sababu ni wazi kwamba
huwezi kuzungumzia utawala wa mamlaka yoyote yale bila
kubaini mipaka yake. Ukimya huu unaweza kuzaa migogoro.
Nitaendelea kutoa mifano mingine katika uchambuzi wangu
unaofuata.
***
Sasa, ni juu yangu kuthibitisha udhani (au hypothesis) wangu.
Kabla sijaanza kufanya hivyo, ningependa kusema kwa dhati
kabisa kwamba Tume hii ya watu 32 wenye kuwakilisha maslahi
tofauti na hisia mbalimbali ilifanya kazi katika mazingira na hali
ngumu sana. Hayo yalitegemewa kutokana na mfumo wenyewe wa
Tume. Wachache wetu tulitahadharisha mapema lakini viongozi
waliosheheni busara wakaamua vinginevyo.
Katika hali hii, mhadhara wangu usichukuliwe hata kidogo kama
kuibeza au kuipuuza kazi waliyofanya akina Mzee Warioba na
wenzake. Sina shaka kwamba wengine wao walipoteza usingizi
na hata kuteseka moyoni mwao kuhusu maaumuzi mengine
waliyoyafanya. Kwa hili, wanastahili pole zetu, zaidi ya pongezi.
II. UKUU WA KATIBA
(SUPREMACY OF THE CONSTITUTION)
Magwiji wa katiba (Wheare 1966, Singh 1994: A-29 na kuendelea,
Nwabueze 2003: juz. 1, sura 3, Seervai 1997: juz. 1, sura v, Shivji
1990/2009) wanaafiki kwamba mfumo wa shirikisho una angalau
sifa ku nne. Hizo ni:
11
Kwamba mwananchi anatawaliwa na serikali mbili, yaani serikali
ya shirikisho na serikali ya mshirika;
Kwamba kuna mgawanyo wa madaraka miongoni mwa serikali;
Kwamba Washirika, na katiba na sheria zao, zina hadhi sawa; na
Kwamba Katiba ya Shirikisho ni sheria kuu (supreme law).
Je, Rasimu inakidhi sifa hizi? Kwa maoni yangu, kwa kiasi kikubwa,
mfumo wa shirikisho katika Rasimu unakidhi sifa tatu za awali.
Kila mwananchi pande zote mbili atatawaliwa na serikali mbili;
Wabara watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na Serikali ya Bara,
Wazanzibari watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na serikali ya
Zanzibar. Pia kuna mgawanyo wa madaraka kati ya serikali tatu.
Washirika, yaani Bara na Zanzibar wana hadhi sawa (ib. 61(5)).
Sifa inayotatanisha ni ya mwisho, ile inayosema kwamba Katiba
ya Shirikisho ni sheria kuu. Nitazichambua ibara zinazohusika.
Kabla sijafanya hivyo, nieleze kwa muhtasari tu maana na dhana
ya Ukuu wa Katiba (supremacy of the constitution).
‘Ukuu wa Katiba’ maana yake ni sheria zote, madaraka, majukumu
na mamlaka yanatokana na katiba na katiba ndio chanzo cha
uhalali wa utawala. Katiba yenyewe inapata mamlaka yake kutoka
kwa wananchi katika ujumla wao. Ndiyo maana, katika msamiati
wa kawaida, tunasema katiba ni sheria mama. Nikitumia msamiati
huo kwa katiba ya shirikisho, naweza nikasema kwamba katiba
ya shirikisho ndio mama na baba wa shirikisho. Katiba na sheria
za Washirika, ingawa zina mamlaka kamili katika maeneo yao,
zinatokana na katiba ya shirikisho na zinapata uhai wao wa kisheria
kwa mujibu wa katiba ya shirikisho. Muhimu zaidi ni kwamba,
kama kuna masharti ya katiba au sheria za Washirika ambazo
zinakinzana na katiba au sheria za shirikisho zilizopitishwa kwa
mujibu wa katiba ya shirikisho, basi sharti husika inakuwa batili
kwa kiasi kile. Kwa lugha ya kimombo dhana hii inaitwa supremacy
12
clause, yaani kipengele cha ukuu wa katiba ya shirikisho. Katika
katiba zote za shirikisho duniani kuna kipengele cha ukuu;
Marekani, Australia, India, Canada n.k. Sitazinukuu zote isipokuwa
mbili, Katiba za Marekani na Australia. Ibara ya VI ya Katiba ya
Marekani inasema:
This Constitution, and the Laws of the United States which
shall be made in Pursuance thereof; and all Treaties made,
or which shall be made, under the Authority of the United
States, shall be the supreme Law of the Land; and the
Judges in every State shall be bound thereby, any Thing
in the Constitution or Laws of any State to the Contrary
notwithstanding.
Na kifungu 109 cha Katiba ya Australia kinasema hivi:
When a law of a State is inconsistent with a law of the
Commonwealth, the latter shall prevail, and the former
shall, to the extent of the inconsistency, be invalid.
Kwa kifupi, vipengele vyote viwili vinasisitiza ukuu wa katiba
ya shirikisho. Na hii ina mantiki na umuhimu wake usiopingika.
Ukitaka shirikisho liwe imara na liwe na nguvu, basi hakuna
budi Washirika wakubali kutambua na kutii masharti ya katiba
ya shirikisho. Bila hivyo, shirikisho litayumba na kutakuwa na
migogoro kutokana na vipengele vya katiba na sheria na vitendo
vya vyombo vya Washirika kukinzana na kugongana kila mara.
Sasa tuangalie vipengele vya Rasimu vinasemaje kuhusu ukuu wa
Katiba ya Shirikisho. Ibara 8(1) inasema:
Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za Washirika wa
Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba
hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano.
(Msisitizo wangu)
13
Hii ina maana kwamba ukuu wa Katiba ya Shirikisho ni kwa
mambo saba tu ya muungano yaliyotajwa katika nyongeza; licha
ya mambo hayo, katiba za Washirika ni sheria kuu katika maeneo
yao kwa mambo yote mengine yaliyosalia (residual powers).
Tuendelee. Ibara ya 61(4) inasema:
Washirika wa muungano watatekeleza majukumu yao
kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na Katiba zao.
‘Kuzingatia’ sio kubanwa; Kiingereza chake ni ‘to take account
of’, ‘to bear in mind’. Unaweza ukazingatia masharti ya Katiba
ya Shirikisho na baada ya hapo ukatenda kinyume chake, lakini
hata hivyo utakuwa hujavunja katiba. Hii inaeleweka zaidi
ukisoma ibara ndogo inayofuata inayotaka Washirika kutekeleza
majukumu yao kwa masuala yasiyo ya Muungano ‘kwa mujibu’ wa
masharti ya katiba zao. ‘Kwa mujibu’ inaleta maana ya kubanwa,
huwezi ukakiuka. Kwa hivyo, masharti ya Katiba ya Shirikisho
yanakushawishi; masharti ya katiba ya Mshirika yanakushurutisha.
Niangalie ibara nyingine ya mwisho ambayo inakaribia kidogo
kuuzungumzia ukuu wa Katiba ya Shirikisho. Ibara 109(5)
inasema:
Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Tanzania Bara
na Katiba ya Zanzibar, Katiba hii itakuwa na nguvu
ya sheria katika Jamhuri ya Muungano kwa mambo
yanayohusu Muungano na endapo sheria nyingine
yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii,
basi sheria hiyo nyingine, kwa kiasi kinachokiuka
Katiba hii, itakuwa batili.
Kuna dhana mbili zilizotumika katika kipengele hiki: ‘mambo
yanayohusu’ (Muungano) na ‘sheria’. Bila shaka ‘mambo
yanayohusu Muungano’ ni dhana pana zaidi kuliko ‘mambo ya
14
Muungano’. Mambo ya Muungano ni yale saba yaliyotajwa katika
nyongeza. Mambo yanayohusu Muungano ni hayo saba pamoja
na yale yote yaliyozungumziwa katika Katiba ya Shirikisho. Kwa
mantiki hiyo hiyo, neno ‘sheria’ haliwezi likawa na maana pana
zaidi ya sheria inayohusu mambo ya Muungano yanayotungwa na
Bunge la Shirikisho kwa mujibu wa ibara 109. Kwa hivyo, ukuu wa
Katiba ya Shirikisho unaozungumziwa katika ibara hii ni juu ya
shughuli za Muungano tu. Sheria yoyote juu ya mambo yanayohusu
Muungano ikikiuka masharti ya Katiba ya Shirikisho, sheria hiyo
ni batili. Lakini hii haihusu katiba na sheria za Washirika.
Uchambuzi wangu wa ibara hizi zote zinazohusu hadhi ya Katiba ya
Shirikisho katika uhusiano wake na katiba na sheria za Washirika,
unaweza kuhitimishwa kama ifuatavyo:
Mosi, hakuna popote pale katika Rasimu tunapokuta Ukuu wa
Katiba ya Shirikisho (kwa maana ya supremacy clause) umewekwa
kwa uwazi na ufasaha, kama ilivyo katika katiba nyingine za
shirikisho nilizozitaja hapo awali.
Pili, vipengele vinavyohusika, ama vinatatanisha au viko kimya, au
yote mawili, kuhusu kipengele cha ukuu.
Tatu, hii, kwa maoni yangu, haikutokea kwa makosa au kwa
kuteleza bali ni tokeo la maelewano kwa maana ya compromise.
Nathubutu kusema kwamba kama jambo hili lingejadiliwa katika
Tume, kungekuwa na mvutano mkali sana.
Mwisho, utatanishi na ukimya huu utapalilia vyanzo vya migogoro
na mivutano kati ya mamlaka ya Washirika na Muungano siku za
usoni. Athari zake haziwezi kuepukika. Nitatoa mifano michache
muhimu kadri ninavyoendelea na mhadhara wangu.
15
A.Tunu, Dira, na Malengo
Rasimu ina Tunu, Dira na Malengo ambayo yamesistizwa sana
na Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Mzee Warioba. Yaliyomo
katika Tunu, Dira, na Malengo ni udugu, utu, umoja, uzalendo,
uwazi, n.k. na haya yamerudiwarudiwa. Kwa upande wangu,
sitasemea hayo. Kwa kadri nijuavyo, hakuna utawala popote pale
duniani, uwe wa kibepari, kijamaa au wa mabavu, utakaopinga
hizi Tunu, hata kama hawatekelezi. Lakini jambo mojawapo
ambalo liko kwenye utangulizi (ib. 1(2)) na Malengo (ib. 11(1)) ni
suala zima la kujitegemea. Kwa mfano, lengo kuu mojawapo katika
Malengo (ib. 11(1)) linasema na ninanukuu:
Lengo Kuu la Katiba hii ni kulinda, kuimarisha na
kudumisha udugu, amani, umoja na utengamano wa
wananchi wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia
ustawi wa wananchi na kujenga Taifa huru lenye
demokrasia, utawala bora na kujitegemea (msisitizo
wangu).
Nimechagua ibara hii kuizungumzia kwa sababu kujitegemea
kuna nafasi ya kipekee katika historia yetu ya kisiasa. Mwalimu
na Sokoine walikuwa wanasistiza sana umuhimu wa kujitegemea
kwa hoja kwamba tusipojitegemea tutapoteza uhuru wetu.
Pamoja na hili, kwetu sisi mtazamo wa kujitegemea uliendana
na ujamaa, ujamaa na kujitegemea. Haya mawili yalikuwa kama
chanda na pete. Sasa ujamaa umefutwa kabisa katika Rasimu kwa
hoja kwamba ni itikadi (kana kwamba soko huria, ubinafsishaji
n.k. sio itikadi). Kwa vyovyote vile, kidole kimekatwa, tumebaki
na pete inahengihengi.
Niendelee na mfano wangu. Sura ya Pili inazungumzia Malengo
Muhimu. Malengo yapo katika Katiba ya sasa lakini Malengo
yalivyowekwa katika Rasimu, yanaturudisha nyuma hatua mbili.
16
Kwa nini? Kwanza, katika Rasimu Malengo ni mwongozo kwa
hivyo hayabani kisheria. Katika Katiba iliopo Malengo yana nguvu
ya sheria (ib. 7(1)) ingawa sio kimahakama (ib 7(2)). Pili Malengo
katika Rasimu ni kwa ajili ya vyombo vya Muungano tu (ang. ib.
10(1) na ib. 238(1) maana ya neno ‘serikali’). Katika katiba iliopo
Malengo yalibana vyombo vyote vya serikali zote mbili.
Lakini hata kama yangekuwa yanabana vyombo vya Washirika,
bado yasingekuwa na nguvu ya sheria kwao. Hii ni kwa sababu
ya kutokuwa na kipengele cha ukuu. Kwa mfano, inaweza kutokea
washauri waelekezi wa ndani na nje wakaishauri serikali ya
Tanganyika2 kwamba mtazamo wa kujitegemea umepitwa na
wakati katika dunia ya utandawazi. Katika utandawazi kuna
kutegemeana, sio kujitegemea. Isitoshe, washauri wataendelea,
tukiweka mtazamo wa kujitegemea, ambao unahusishwa na
ujamaa, katika katiba, kuna hatari ya kutoweza kuvutia uwekezaji
kutoka nje. Kutokana na ushauri huo, katika katiba ya Tanganyika,
lengo kuu linaweza likasomeka hivi:
Lengo kuu la Katiba hii ni kulinda, kuimarisha na kudumisha udugu,
amani, umoja na utengamano wa wananchi wa Tanganyika kwa
kuzingatia ustawi wa wananchi na kujenga Tanganyika huru yenye
demokrasia, utandawazi bora na kutegemeana.
Pasipo na shaka, lengo hili linagongana na lengo kuu la Katiba ya
Shirikisho. Hata hivyo, ndio lengo litakalo ongoza vyombo vya
Tanganyika kwa sababu Katiba ya Shirikisho haiko juu ya katiba
za Washirika; yaani, inakosa ukuu.
Kwa mujibu wa lengo jingine (ib. 11(1)(xi), Serikali inaagizwa
‘kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji
wa haki ya mtu kujipatia elimu …’. Serikali inayomaanishwa
katika kipengele hicho ni Serikali ya Muungano, lakini Serikali
ya Muungano haisimamii elimu kwa sababu elimu sio jambo la
17
Muungano. Na inawezekana kabisa katiba za Washirika zisiwe na
lengo linalofanana na hili. Kwa hivyo, lengo hili jema halina maana
- chombo kinachoagizwa kutekeleza lengo, hakisimamii elimu,
na vyombo vya Washirika vinavyosimamia elimu havibanwi na
lengo. Kwa hivyo, jambo linalopendeza kulisikia ni ganda tupu bila
tunda!
Kwa hitimisho, nigusie ibara (10)(2) ambayo inaagiza Serikali ya
Muungano kutoa taarifa Bungeni juu ya utekelezaji wa Malengo
angalau mara moja kwa mwaka. Swali ni kwamba malengo yote
muhimu yanaangukia chini ya mamlaka ya Washirika ambao
ni watekelezaji na hawabanwi na Katiba ya Shirikisho. Katika
ukweli huu, hii taarifa itakayowasilishwa Bungeni itakuwa na nini
na itakuwa na maana gani. Kwa kifupi basi, watekelezaji wakuu
wa Malengo hawabanwi na masharti haya; yule ambaye sio
mtekelezaji ndiye anayebanwa!
B. Maadili na Miiko ya Uongozi
Mzee Warioba pia amechangamkia maadili na miiko ya viongozi
iliyowekwa katika Rasimu, Sura ya Tatu. Kuna ibara kama nane
pamoja na ibara ndogo chungu nzima juu ya suala la maadili na
miiko. Hizi zinawahusu viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa
na ambao watatajwa katika sheria ya Bunge (ib.14(3)). Bunge
linalozungumziwa hapa ni Bunge la Muungano. Lakini Katiba za
Washirika hazihitaji kufuata au kuwa sambamba na vipengele
hivyo. Wana hiari kuweka au kutokuweka, au kurekebisha au
kuchagua vipengele wanavyotaka kwa sababu maadili na miiko sio
jambo la muungano na Katiba ya Shirikisho haiwabani Washirika.
Kwa mfano, ib.20(2)(a)(iii) inasema kwamba kiongozi wa umma
hapaswi ‘kujilimbikizia mali kinyume na sheria’. Sasa, sheria ipi
inayozungumziwa hapa? Je kama hakuna sheria ya Washirika
inayokataza viongozi wa umma kujilimbikizia mali, kipengele
18
hiki katika Katiba ya Shirikisho kitakuwa na uzito gani? Ni wazi,
haiwezi ikawa na nguvu yoyote katika maeneo ya Washirika.
Sasa nimulike kwenye haki za binadamu.
C. Haki za Binadamu
Wakereketwa wameshangilia sana haki za binadamu katika
Rasimu na wana sababu nzuri tu kufanya hivyo. Rasimu imeeleza
kwa ufasaha haki za binadamu na imeongeza haki nyingine
ambazo hazimo katika katiba zilizopo. Kuna mapungufu hapa na
pale lakini haya yanarekebishika. Kwa mfano, haki ya wananachi
kuandamana kuonyesha hisia zao za kulaumu au kutoridhika na
jambo fulani haikuwekwa. Pia hakuna haki ya wafanyakazi kugoma
kama silaha yao muhimu ya kushinikiza waajiri wao kutekeleza
matakwa yao.
Kuna haki mbili muhimu ningependa kuzitaja hapa. Ib. 39(3)
inaeleza kwamba raia wa Jamhuri ya Muungano ‘hatapelekwa
katika nchi ya nje yoyote kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano
ya aina yoyote kinyume cha ridhaa yake.’ Hili ni jambo jema;
hususan inapiga marufuku ile inayoitwa ‘rendition’.3 Pendekezo
langu ni kuongeza vipengele viwili kuweka wazi kwamba ni
marufuku raia wa Jamhuri (a) ‘kufungwa au kuwekwa kizuizini
nchi ya nje bila ya kufuata sheria ya nchi hiyo; na (b) ‘kuhojiwa
na maafisa wa ujasusi au usalama wa nchi za nje katika eneo la
Jamhuri’.4
Lakini suala ambalo linatatanisha ni: Hati hii nzuri ya haki za
binadamu ina uzito gani katika maeneo ya Washirika? Haki za
binadamu sio jambo la Muungano na Katiba ya Shirikisho sio Katiba
mama. Je, kama katiba za Washirika zikikosa vipengele vingine
vya haki au kuandikwa tofauti na kuwa na maana na tafsiri tofauti,
itakuwaje?5 Nitoe mfano. Katika kutekeleza haki ya mwananchi
kushiriki katika utawala, wagombea huru wanaruhusiwa na
19
Rasimu katika ngazi zote za utawala. Iwapo katiba za Washirika
hazina kipengele kama hicho, basi mgombea huru atakuwa na
haki ya kugombea uchaguzi katika ngazi ya Bunge la Muungano
na Urais wa Muungano tu, lakini hakuna mgombea huru atakuwa
na haki kugombea nafasi za serikali za mitaa au mabunge ya
Washirika au urais wa Tanganyika au Zanzibar.6 Huu ni mfano
mwingine wa wananchi kupewa ganda bila tunda.
Sasa nimefikia sehemu muhimu ya mhadhara wangu, muundo na
taasisi za muungano.
III. MUUNDO NA TAASISI ZA SHIRIKISHO
Hitimisho langu juu ya muundo wa muungano ni kwamba, mosi, ni
tegemezi na, pili, ni dhaifu kwa sababu umejengwa juu ya msingi
wa mchanga wa dhamira na nia nzuri badala ya msingi wa mawe
ya nguvu za kikatiba zilizowekwa na wananchi wenyewe. Ni kama
kwamba suala la Muungano ni ujirani mwema badala ya umoja
wa nchi. Nitalifafanua kwa kuchambua mifano ya maeneo kama
manane hivi.
A.Taasisi Kuu za Kusimamia Muungano
Muungano wa Jamhuri ya Muungano umeainishwa kama shirikisho
lenye serikali tatu (ib. 57(1), serikali ya muungano au shirikisho,
serikali ya Tanzania Bara na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.7
Kwa maoni yangu, kwa usahihi zaidi, hizi zingeitwa dola tatu kwa
sababu zote zina mihimili mitatu ya dola, yaani, serikali, bunge na
mahakama, na mamlaka yao ya utawala. Kwa kukwepa kuainisha
na kutaja kwa jina lake dhana inayokusudiwa, ina athari zake
za kutokuelewana na kuzaa mizozo isiokuwa ya lazima. Mfano
mzuri ni yale malumbano yaliyotokea juu ya Zanzibar kuwa nchi
au sio nchi.8 Inawezekana, kwa busara zake, Tume ilichagua kwa
20
maksudi msamiati uliozoeleka kuepuka malumbano juu ya maana
ya dola na nchi. Tuachane na hili, tuendelee.
Kuna taasisi mbili za mahusiano baina ya serikali hizi tatu -, Tume
ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali (ib.102(1) na Mawaziri Wakaazi
(ib. 64). Mawaziri Wakaazi watateuliwa na Washirika na watakuwa
na ofisi zao Makao Makuu ya Serikali ya Muungano. Eneo la Makao
Makuu halijulikani kama litakuwa katika eneo la Tanganyika
au Zanzibar, au litakuwa linahamahama kati ya Tanganyika na
Zanzibar. Vyovyote vile, itabidi serikali ya muungano iombe
serikali za Washirika kuipatia eneo lake la kujenga ofisi za makao
makuu pamoja na Ikulu ya Rais wa Muungano.9 Jukumu mahsusi
la hao Mawaziri Wakaazi ni kusimamia uhusiano baina ya serikali
za Washirika, kwa upande mmoja, na kati ya Serikali ya Muungano
na serikali ya Mshirika mhusika, kwa upande mwingine.
Tume ya Uhusiano ina wajumbe sita - makamu wa rais wa
Muungano, ambaye atakuwa mwenyekiti, marais wawili wa
Washirika, Mawaziri wawili Wakaazi na waziri mwenye dhamana
ya mambo ya nje ya Muungano (ib. 102(2). Jukumu na lengo kuu
la Tume ni kusimamia na kuweka taratibu na mazingira mazuri
ya mashauriano, mashirikiano, na utatuzi wa migogoro baina ya
serikali tatu (ib. 103-104). Kwa jumla, Tume ya Uhusiano sio
chombo cha utendaji (executive) isipokuwa tu kitahusika katika
utatuzi wa migogoro ambao nitauzungumzia hivi punde. Katika
hali halisi ya ulinganisho wa nguvu za kisiasa, sidhani kwamba
Tume inaweza kufanya maamuzi yanayobana pande zote husika,
bali, zaidi ni kufikia maelewano, ambayo pia huwezi kuwa na
hakika kwamba yatatekelezwa. Isitoshe, marais hawa watatu
wakitoka vyama tofauti (mbali na wagombea binafsi), vyenye sera
na mielekeo tofauti, hata kufikia maelewano inaweza kushindikana
na kusababisha mivutano na migogro isiyokuwa na mwisho.
Pili, katika usuluhishi na utatuzi wa migogoro, tume inaweza
21
kufanya uamuzi lakini upande wowote ambao haukuridhika una
haki ya kukata rufani katika Mahakama ya Juu na uamuzi wa
Mahakama unakuwa wa mwisho (ib. 104(1)(e) Kwa vyovyote vile,
Tume sio ngazi ya kwanza katika kutatua mgogoro kwa sababu
pande zote hazilazimishwi kuanzia mgogoro katika Tume bali zina
hiari ya kuanzia ama katika Tume au katika Mahakama.
Kwa kujumuisha, navyoona mie, chombo hiki kikuu cha kiungo
baina ya serikali tatu, kitakuwa na changamoto kama tatu hivi
ambazo zinaweza zikageuka kuwa matatizo.
Mosi, kuna suala la protokali. Marais kuwa chini ya uenyekiti
wa Makamu wa Rais ina utata. Katika hali ya kawaida, masuala
ya protokali yasingekuwa ya kuzingatiwa lakini kwa sababu
zisizoeleweka wakuu wa nchi zetu wanajali sana protokali, labda
kudhihirisha ukuu wao.
Pili, ambayo ni muhimu zaidi, hakuna uwiano wa nguvu za kisiasa
katika Tume. Kwa vyovyote vile, mwenye nguvu katika Tume
atakuwa Rais wa Bara - yeye ndiye mtawala wa eneo kubwa
lenye wananchi wengi, yeye ndio mwenye rasilimali nyingi,
yeye ndiye anatoa mchango mkubwa wa kuendesha serikali ya
muungano, ikiwemo gharama za Tume yenyewe. Kwa hivyo,
tupende tusipende, yeye ndiye atakuwa na sauti nzito. Isitoshe,
kutokana na muundo wa serikali tatu, rais wa Bara hataona aibu
kujitutumua kinyume na ilivyo katika serikali mbili wakati rais
mwenye dhamana ya Bara pia ni rais wa muungano.
Tatu, ikiwa Tume inataka kufanya uamuzi wowote, itakuwa vigumu
kwa sababu kila upande unawakilishwa na watu wawili wawili.
Nne, katika hali hiyo, mara nyingi, hasa katika masuala nyeti au
mazito ya kitaifa, hata kufikia maelewano itakuwa vigumu. Kati ya
Washirika, unaweza kukuta kila mara upande dhaifu ambao hoja
zake zinaelekea kutokubalika, ataomba kikao kiahirishwe ili arudi
22
kwake kushauriana na wenzake au kupata maoni ya wananchi
wake. Kwa wanasiasa, hii inakuwa ni mbinu ya kuahirisha
maafikiano, yaani, delaying tactics.
Kwa jumla, na bila kubeza, tathmini yangu ya Tume hii ni kwamba
haina tofauti ya msingi na zile kamati zisizoisha za akina Shekilango
juu ya kero za Muungano.
B. Bunge la Muungano
Mamlaka ya kutunga sheria juu ya mambo yote yanayohusu
Muungano yamewekwa chini ya Bunge la Muungano. Mambo ‘yote
yasiyo ya Muungano yatakuwa chini ya Bunge la Tanzania Bara
na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’ Bila shaka, mamlaka haya
yatatumika kwa mujibu wa Katiba zao. Kuhusu Bunge, nitagusia
mambo matatu yanayotatiza.
Moja, ni majimbo ya uchaguzi wa Bunge la Muungano. Kwa
mujibu wa ib. 105(3) ‘kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara
na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi’.
Wanahabari wetu waliobobea wamekwishapiga hesabu. Kuna
mikoa 25 Bara na wilaya 10 Zanzibar. Kwa kuwa watakuwepo
wabunge wawili kutoka kila jimbo, mmoja wa kiume na mwingine
wa kike (ib. 104(4), basi tutakuwa na wabunge 70, 50 kutoka
Bara na 20 kutoka Zanzibar. Pia watakuwepo wabunge watano
kuwakilisha kundi la walemavu ambao watateuliwa na Rais wa
muungano. Naona tunaweza kutabiri kwamba watatu watatoka
Bara na wawili watatoka Zanzibar ili kuwe na uwiano na idadi
ya watu. Jumla tutakuwa na wabunge wa Bara 53, ambayo ni
asilimia 71, na 22 kutoka Zanzibar, ambayo ni asilimia 29. Kwa
hivyo, uwiano wa Bara na Zanzibar ni asilimia 71 kwa asilimia 29,
Wabara wakiwa zaidi ya theluthi mbili ya wabunge wote. Uwiano
huu moja kwa moja unapingana na msingi wa kwanza kabisa
wa shirikisho. Shirikisho linasimama kwenye usawa wa kisiasa
23
(political equality) wa Washirika bila kujali ukubwa au idadi ya
watu wao. Kwa hivyo, uwakilishi wao hasa katika chombo cha
kutunga sheria unatakiwa kuwa sawa.
Lakini kuna jambo jingine la kutatanisha. Mikoa na wilaya ni
ngazi za utawala ambazo haziko chini ya mamlaka ya Muungano.
Ugawaji wa maeneo ya utawala ni mamlaka ya vyombo vya
Washirika, hususan Rais. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara 2A
ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Rais ndiye mwenye mamlaka ya
kugawa maeneo ya mikoa na wilaya. Sioni sababu ya Zanzibar
kukibadilisha kipengele hiki kwa sababu hawashurutishwi na
Katiba ya Shirikisho (Rasimu) kufanya hivyo. Isitoshe, hakuna
chochote katika Rasimu kumzuia rais au marais wa Washirika
kubadilisha mipaka na kuongeza idadi ya mikoa au wilaya katika
maeneo yao.
Tuchukue mfano. Kwa sababu zozote zile, rais wa Zanzibar
anaamua kugawa Zanzibar katika wilaya 20. Hii itamaanisha
kwamba kutakuwa na wabunge 40 kutoka Zanzibar, ikifanya jumla
ya wabunge kuwa 95 badala ya 75 katika Bunge. Mabadiliko haya
mara moja yatakuwa yamebadili uwiano kati ya Bara na Zanzibar
- asilimia 56 kutoka Bara na 44 kutoka Zanzibar. Na, je, jambo
hili likitokea katikati ya muda wa Bunge, kutakuwa na uchaguzi
mpya? Nimesema rais anaweza kufanya hivyo kwa sababu zozote
zile lakini pia anaweza kufanya hivyo kwa maksudi ili kujiongezea
uwakilishi katika Bunge la Muungano. Kwa lugha ya kimombo, hii
inaitwa gerrymandering. Vilevile, kwa upande wa Bara, rais wa
Tanganyika anaweza kuongeza idadi ya mikoa.
Pili, Rasimu inaruhusu wagombea huru na pia uwezo wa wapiga
kura kumuondoa mbunge wao hata kabla ya kipindi chake kwa
sababu zilizotajwa (right of recall) (ib. 124). Mambo haya yote
mawili yanahusika na wabunge wa Bunge la Muungano na
sio mabunge ya Washirika. Kwa hivyo, Washirika wanaweza
24
wakaamua bila kuvunja katiba ya Shirikisho kwamba katika
maeneo yao hawatakuwa na wagombea huru wala haki ya
wapigakura kuondoa wabunge wao. Na hii sio nadharia tu.
Viongozi watarajiwa wamekwishaanza kuonyesha wasiwasi wao
kuhusu mgombea huru na haki ya wananchi kuweza kumuondoa
mbunge wao kabla ya muda.
Jambo la tatu linawagusa wananchi kwa karibu sana. Ib. 107(2)(h)
inaeleza kwamba miongoni mwa madaraka ya Bunge ni ‘kujadili
na kuridhia mikataba yote inayohusisha rasilimali na maliasili
zinazosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.’ Jambo hili
ni jema kabisa na la kulifurahia, angalau mikataba hii izungumzwe
Bungeni kwa uwazi badala ya wananchi kuambiwa kwamba ni
siri ya kibiashara. Lakini, rasilimali na maliasili – ardhi, mafuta,
madini, gesiasilia, maji, mapori, n.k. – sio jambo la Muungano.
Rasilimali na maliasili ni chini ya mamlaka ya Washirika na
wao ndio watayasimamia. Katika hali hii, Serikali ya Muungano
itaingia kwenye mikataba ipi na kuhusu rasilimali gani? Ni mfano
mwingine wa wananchi kulishwa maneno matamu yasiyo na
uhalisia. Ni haki hewa.
Sasa niangalie taasisi nyingine nyeti na muhimu, jeshi la polisi.
C. Jeshi la Polisi
Nianze kwa kuweka wazi kwamba polisi haimo miongoni mwa yale
mambo saba ya Muungano kinyume na katiba ilioko (Nyongeza
ya Kwanza, jambo la nne). Pamoja na kutamka kwamba Jeshi la
Polisi ni chini ya mamlaka ya Muungano na jeshi ndilo litakuwa
na jukumu la ‘ulinzi wa watu na mali zao’ (ib. 227(1), Rasimu
inasema kwamba ‘Washirika … wanaweza kuanzisha vikosi vya
ulinzi vitakavyosimamia masuala ya usalama wa watu na mali
katika maeneo yao.’ (ib. 232(1) Bila kutafuna maneno, ibara hii
ni wazi na maana yake ni kwamba Washirika wanaweza wakawa
25
na majeshi yao ya polisi, ilimradi yasiitwe polisi kwa jina, ingawa
yana majukumu na muundo unaofanana kabisa na ule wa Jeshi la
Polisi. Kwa hivyo, utakuta kuna majeshi matatu ambayo majukumu
yao ni yale yale. Katika hali hii huwezi kuepuka migongano na
kama tujuavyo vikundi vyenye silaha vikigongana, unaoathirika ni
usalama wa wananchi. Bila shaka, waandishi wa Rasimu waliona
uwezekano huo; usuluhishi wao ni kuongeza kipengele kingine
kinachosema, ‘Vikosi vya ulinzi vya Washirika wa Muungano,
vitatekeleza majukumu yao kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi la
Jamhuri ya Muungano ili kuepusha mgongano wa mamlaka …
‘ (ib. 232(2). Tuwe wa kweli, jambo muhimu kama uwezekano
wa migongano kati ya majeshi unaweza kweli kuliachia nia na
dhamira njema ya kushirikiana? Tena kikatiba? Busara inahitaji
kwamba angalau kikatiba unaweka mazingira na masharti ya
kuepuka migongano, sio kuweka mazingira ya migongano na halafu
ukasema washirikiane ili kuepuka migongano. Haileti maana wala
haina mantiki. Ndio maana huwezi ukawa na vikosi vya usalama
zaidi ya kimoja vyenye majukumu yale yale wakifanya kazi katika
maeneo yale yale. Kama busara ingetumika, basi ‘polisi’ ingeweka
katika orodha ya mambo ya muungano na lingeundwa jeshi moja
tu la polisi la Jamhuri ya Muungano. Na ingekuwa marufuku mtu,
taasisi au serikali nyingine yoyote kuunda vikosi vya usalama
huru nje ya jeshi la Jamhuri.
Kwani wajumbe wazito wa Tume hawakuwa na busara au
hawakuliona hili? La hasha, wajumbe wengine katika Tume
wana busara tele, utaalam wa mambo ya kikatiba na tena wana
uzoefu wa kuendesha nchi kwa zaidi ya robo karne. Kwa hivyo,
ninashawishika kueleza vipengele hivyo kama maelewano, tena
zaidi ya maelewano, kuhalalisha kinachoitwa ‘idara maalum’
katika Katiba ya Zanzibar ilioko (Sura ya Kumi). Idara maalum
ya Zanzibar inajumuisha Jeshi La Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi
Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) na Chuo cha Mafunzo (cha
26
wahalifu) (ib. 121(2). Rais wa Zanzibar ana mamlaka kamili juu ya
idara maalum na tena kikatiba anaitwa ‘Kamanda Mkuu wa Idara
Maalum’.
Rasimu hii ikipita kuwa sheria kama ilivyo, mimi sitashangaa
ikiwa Zanzibar itarekebisha Katiba yao katika ibara ya 26(1)
ambayo ilivyo inasomeka: ‘Kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye
atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.’ Baada ya
marekebisho, ibara inaweza ikasomeka: ‘Kutakuwa na Rais wa
Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa nchi ya Zanzibar, Kiongozi
Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.’
Na hii haitakuwa kinyume cha Katiba ya Shirikisho kwa sababu,
moja, polisi sio jambo la muungano na, pili, Katiba ya Shirikisho
yenyewe inaruhusu.
Vilevile Tanzania Bara wanaweza likaufuata nyanyo na kuwa na
vikosi vyao vya usalama na ulinzi. Hali halisi ilivyo, vikosi hivyo
vya Bara au Tanganyika vitakuwa na uongozi wa kitaalam, silaha
za kisasa na nguvu zaidi kuliko Jeshi la Polisi la Jamhuri ambalo
litajikuta halina fedha za kujiendesha.
Nitatoa mfano mmoja wa kuonyesha migongano hatarishi
inayoweza kutokea katika hali halisi. Ingawa mfano huu ni wa
kudhania, sio kama hauwezekani kutokea. Rais wa Jamhuri kwa
tathmini yake anaona kuna hali ya hatari katika eneo mojawapo la
Bara ambao inahitaji kudhibitiwa mara moja. Kwa mujibu wa ib.
81, baada ya kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama wa Taifa,
kikao ambacho hakikuhudhuriwa na Rais wa Bara, anatangaza
hali ya hatari na kupeleka kikosi cha FFU kuidhibiti. Utangazwaji
wa hali ya hatari sio jambo la muungano (kinyume na Katiba
ilioko ambayo inasema mamlaka juu ya hali ya hatari ni jambo
la Muungano, Nyongeza ya Kwanza). Rais wa Bara pia anapeleka
27
kikosi chake cha usalama kudhibiti hali hii na kumtaka Rais wa
Jamhuri aondoe mara moja kikosi cha FFU. Rais wa Jamhuri
anakaidi ushauri huu. Kwa vyovyote vile, kutatokea mgongano kwa
sababu katika hali halisi vikosi vyote viwili vina hadhi sawa, kikosi
cha Bara kwa mujibu wa Katiba ya Bara na kikosi cha Jamhuri kwa
mujibu wa katiba ya muungano. Lolote linaweza kutokea katika
hali kama hii ambalo haliwezi kutabirika.
D. Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Juu
Mahakama katika ngazi ya Jamhuri ni mbili, Mahakama ya Juu
na Mahakama ya Rufani. Mahakama ya Rufani ni mahakama
inayosikiliza rufani kutoka mahakama kuu za Washirika kama
tulivyozoea isipokuwa sio ngazi ya mwisho. Uamuzi wa Mahakama
ya Rufani unaweza kupingwa katika Mahakama ya Juu na uamuzi
wa Mahakama ya Juu ni wa mwisho.
Mahakama ya Juu ndio mahakama mpya. Pamoja na kusikiliza
rufani zote kutoka Mahakama ya Rufani, ina majukumu mahsusi
ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua mambo matatu –
– kusikiliza na kuamua mara ya kwanza na mwisho mashauri
yanayohusu uchaguzi wa Rais wa Jamhuri;
– kusikiliza na kuamua mashauri kuhusu tafsiri ya Katiba
ya Shirikisho yanayoletwa na serikali yoyote kati ya tatu
zilizopo;
– kusikiliza na kuamua migogoro baina ya serikali hizo
inayoletwa na mmoja wao.
Pia ina mamlaka ya kutoa maoni ya kishauri kwa Serikali ya
Muungano au Serikali za Washirika. Rasimu haiko wazi kwamba
inatoa maoni pale tu inapoombwa au inaweza kufanya hivyo kwa
utashi wake yenyewe.
Mahakama ya Juu ina Jaji Mkuu na Naibu wake na majaji saba
28
wengine, jumla ya majaji wakiwa tisa. Mahakama ya Rufani ina
Mwenyekiti na majaji wengine 17. Kwa jumla kuna majaji 27 katika
Mahakama za Jamhuri (Sio mzigo mdogo huu!) Kuna vipengele
vinavyosisitiza uwiano wa uwakilishi kutoka pande mbili za
muungano.
Jambo la kutatanisha katika muundo huu ni hili. Mahakama
ya Juu na Mahakama ya Rufani sio miongoni mwa mambo ya
Muungano. Pamoja na ukweli huu, ib.158(3) inaweka mamlaka ya
kutunga utaratibu na sababu za rufani mikononi mwa Washirika
kwa mujibu wa katiba na sheria zao. Matokeo yake ni kwamba
Washirika wanaweza, wakitaka, kuamua mashauri yapi yaende
katika Mahakama ya Rufani ya Jamhuri na yapi yazuiliwe.
Kwa mfano, Katiba ya Zanzibar ya 1984 iliopo inazuia kesi zozote
zinazohusika na tafsiri ya Katiba ya Zanzibar, na kesi za Kiislamu
zilizoanzia katika Mahakama za Kadhi kusikilizwa na Mahakama
ya Rufani, hii pamoja na kwamba Mahakama ya Rufani ni jambo la
Muungano (nyongeza ya pili). Inawezekena kabisa kwamba baada
ya Rasimu kuwa sheria, katiba za Washirika zikasema kwamba –
– kesi zote za tafsiri za katiba zao;
– kesi zote za uchaguzi pamoja na uchaguzi wa marais wao;
– kesi zote za uhaini dhidi ya serikali zao;
– kesi zote sinazohusu ukiukwaji wa haki za binadamu au
maadili na miko ya viongozi; n.k.
hazitapelekwa katika Mahakama ya Rufani ya Jamhuri na badala
yake zitasikilizwa na kuamuliwa mara ya mwisho na mahakama zao
za rufani au na jopo la majaji (ya idadi iliyotajwa) wa Mahakama
Kuu yao. Isitoshe, wanaweza kwenda mbali zaidi kwa kusema
kwamba matokeo ya uchaguzi wa marais wao hayatapingwa katika
mahakama yoyote ile. Wakifanya hivyo, na hakuna sababu ya
kisheria kwanini wasiweze, hadhi ya Mahakama za Jamhuri, pamoja
na kazi yao, itapungua.
29
Sasa niangaze taasisi nyeti ya Muungano, na hii sio nyingine,
isipokuwa Benki Kuu.
E. Benki Kuu
Uchumi unaotegemea uuzaji na ununuaji wa bidhaa, fedha na
mzunguko wa sarafu na uhamishaji wa fedha unakuwa na nafasi
ya kipekee. Akiba inawekwa kupitia fedha; uwekezaji unahesabiwa
kwa fedha; rasilimali zinathaminiwa kwa fedha. Benki Kuu, angalau
kinadharia, ni taasisi nyeti inayosimamia fedha katika sura zake
mbalimbali. Majukumu muhimu ya Benki Kuu ni kutoa na kusimamia
sarafu na fedha na mzunguko na uhamishaji wake; kusimamia
ujazi wa fedha (money supply) na amana (bank deposits) katika
benki zote pamoja na za kibiashara; kutunga na kusimamia sera ya
kifedha (monetary policy); kuratibu, kudhibiti na kuhakiki mabenki
ya biashara na uwekezaji katika nchi; kudhibiti mfumuko wa bei,
ikiwemo bei ya fedha za kigeni (foreign exchange rate); na hatimaye
ni benki ya serikali. Kwa muhtasari basi Benki Kuu ni mtunzaji,
mlinzi, mwangalizi na msimamizi wa fedha za taifa pamoja na akiba
ya nchi, ikiwa akiba ya dhahabu au fedha za kigeni.
Kwa maoni yangu, katika nchi na uchumi kama wetu, na ili kuepuka
misukosuko ya fedha, hakuna budi Benki Kuu idhibiti na kuongoza
soko, badala ya kufuata soko. Benki Kuu ikifuata soko bila kuwa na
msimamo kwa mujibu wa sera ya fedha, na mtazamo wa maendeleo
wa nchi, basi litakuwa kama bendera inayopepea kwa kuelekezwa
na upepo badala ya kudhibiti mwelekeo wa upepo. Benki Kuu
inatakiwa kuwa kinu kinachonasa upepo ili kujijengea nguvu, sio
bendera inayoyumbishwa na upepo.
Kwa vyovyote vile, huwezi kuwa na Benki Kuu zaidi ya moja katika
nchi moja hata kama ni nchi ya shirikisho. Je, Rasimu inasema nini
kuhusu Benki Kuu?
Kwanza, ‘Sarafu na Benki Kuu’ ni jambo la Muungano. Hii ni tofauti
30
na Katiba ilioko inayosema kwamba, ‘Mambo yote yanayohusika
na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti);
mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za
mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika
na fedha za kigeni’ ni jambo la Muungano (nyongeza ya kwanza,
jambo la 12). Hii ni pana zaidi, inataja sio sarafu tu lakini mambo
yote yanayohusika na fedha, ikiwemo, bila shaka, sera za kifedha.
Pamoja na hayo inataja usimamizi wa fedha za kigeni.
Pili, Rasimu katika ib. 218 inasema Washirika wanaweza wakawa
na benki zao zitakazokuwa na jukumu la ‘kutunza akaunti ya fedha
za serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki za biashara
katika mamlaka zao.’ Nitarejea kwenye hii hivi punde.
Tatu, majukumu ya Benki Kuu yaliyotajwa katika Rasimu ni
manne –
‘(a) kutoa sarafu, kudhibiti na kusimamia mzunguko wa sarafu;
(b) kuandaa na kusimamia Sera na Mipango inayohusiana na
sarafu;
(c) kudhibiti na kusimamia masuala ya fedha za kigeni; na
(d) kusimamia Benki za Washirika wa Muungano.’
Aya (a) na (b) haina shida kwa sababu zinahusika na sarafu
ambayo ni jambo la Muungano. Lakini aya (c) na (d) sio mambo ya
Muungano. Kwa kuwa masharti ya Katiba ya Shirikisho, ambayo
hayahusiki na mambo ya Muungano, hayawabani Washirika,
inawezekana kabisa Washirika wasitilie maanani aya hizi na
wakafanya shughuli zao kupitia benki zao kama kwamba masharti
haya ya kusimamiwa na Benki Kuu, na fedha zao za kigeni
kudhibitiwa na Benki Kuu, yasingekuwepo.
Nitahitimisha na kujumuisha hoja yangu juu ya Benki Kuu kama
ifuatavyo:
31
Moja, Benki Kuu iliyotajwa katika Rasimu inakosa majukumu
muhimu ya Benki Kuu za kawaida.
Pili, benki za Washirika zina uhuru wa kutekeleza mamlaka yote
ya benki kuu isipokuwa kutoa na kudhibiti mzunguko wa sarafu.
Kwa hivyo, Benki Kuu ya Shirikisho ni Benki Kuu kwa jina tu.
Ukweli ni kwamba inafanana zaidi na baraza la sarafu, yaani
‘currency board’, kuliko Benki Kuu.
F. Mapato na Gharama za Muungano
Rasimu inataja vyanzo vinne vya mapato ya Muuungano (ib. 215).
Vyanzo hivyo ni –
‘(a) ushuru wa bidhaa;
(b) maduhuli yatokanayo na taasisi za Muungano;
(c) mchango kutoka kwa Washirika wa Muungano; na
(d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano.’
Aya (a) na (b) zimetajwa katika mambo ya Muungano. Ushuru
wa bidhaa una utata kidogo. Ninafikiri hii haimaanishi ushuru
wa bidhaa unaosimamiwa na idara ya forodha kwa maana ya
excise duty. Kwa hivyo labda inamaanisha ushuru au kodi kama
value added tax (VAT), sales tax, produce cess n.k. Kama hii ndio
iliyokusudiwa inahitaji ufafanuzi zaidi. Kwa vyovyote vile, ushuru
wa bidhaa unakusanywa mahali pa uzalishaji, uuzaji na ulaji. Kuna
masuala mawili hapa. Moja, Serikali ya Muungano itahitaji vyombo
na maofisi katika sehemu mbalimbali za maeneo yote mawili ya
Muungano kuweza kukusanya ushuru. Hii yenyewe inaweza ikawa
na gharama kubwa. Pili, ili kuziba nakisi katika bajeti yake, Serikali
ya Muungano itajikuta kila mara inaongeza ushuru huu, jambo
ambalo litawaongezea wananchi mzigo. Pamoja na kulipa ushuru
huu wananchi watakuwa wanalipa kodi na malipo mengine kwa
serikali zao.
32
Inaelekea ushuru wa bidhaa ndio utakuwa chanzo kikuu cha
mapato ya Serikali ya Muungano. Maduhuli inamaanisha karo
na malipo yanayolipwa serikalini kwa huduma mbalimbali (k.m.
pasipoti, hati ya uraia, visa, n.k.). Kuna idara moja tu katika mambo
ya Muungano ambayo inaweza kutoa mapato haya, nayo ni ‘uraia
na uhamiaji’. Kuna usajili wa vyama vya siasa pia lakini hii ina
walakin nitaozungumzia baadae.
Ninahisi kwamba mapato makubwa ya Muungano yatatokana na
mchango wa Washirika. Ni wazi kwamba Bara ndio itachangia
asilimia kubwa sana. Inanishangaza kwamba Rasimu haitaji
kabisa uwiano wa mchango kutoka kwa Washirika. Jambo hili ni la
awali kabisa kuandikwa katika rasimu yoyote ya Shirikisho.
Hili la mkopo kutoka nje na ndani sina hakika nalo. Serikali ambayo
haina chanzo chake huru cha mapato au sekta ya uzalishaji au
walipa kodi wakubwa, hususan mashirika, chini yake, itakuwa na
hali ngumu ya kupata mikopo.
Kwa jumla, kuna utatanishi na wasiwasi kwa upande wa mapato
ya Muungano. Kwa upande wa gharama, ni wazi kwamba
kuendesha serikali ya muungano kutakuwa na gharama kubwa.
Kazi inayofanywa na taasisi moja au idara moja katika muundo
uliopo sasa itahitaji taasisi mbili. Kwa mfano, badala ya kuwa na
Tume moja ya uchaguzi, sasa kutakuwa na tume mbili, moja ya
Muungano na nyingine ya Bara. (Ukiongeza ya Zanzibar kutakuwa
na Tume tatu za uchaguzi.) Na hivyo hivyo kuhusu tume nyingine.
Ukiangalia juujuu tu, licha ya taasisi na idara za kawaida katika
serikali, kuna tume karibu nane na mabaraza mawili yenye
wajumbe wazito ambao bila shaka watakuwa na mishahara
minono na marupurupu poa. Wananchi wamekwishaanza
kuonyesha wasiwasi wao kwa kuwaongezea mzigo wa kubeba
serikali kamili nyingine, zaidi ya hizi mbili tulizonazo.
33
G. Mambo ya Muungano
Kama tulivyoona, kuna mambo saba katika mambo ya Muungano.
Sina mengi ya kusema zaidi ya yale niliyoyasema kwamba polisi,
Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani na mambo yote yahusuyo
fedha na fedha za kigeni yangefaa kuwa mambo ya Muungano.
Kuna jambo moja la Muungano ambalo mimi binafsi sioni mantiki
ya kuwa kwenye orodha hii - ‘Usajili wa Vyama vya Siasa’. Ukiwa
umeshaweka muundo wa serikali tatu, jambo linalofuata ni juu
ya chama cha siasa chenyewe kama kinataka kugombea uchaguzi
katika eneo moja tu na sio lingine. Kwa hivyo, unaweza ukawa na
chama cha siasa ambacho kinagombea uchaguzi katika Zanzibar
tu, au Bara tu, au katika ngazi ya Muungano tu.
H. Michakato ya Katiba na Mengineyo
Kabla sijaenda kwenye sehemu yangu ya mwisho na kuhitimisha
ningependa kutahadharisha kuhusu michakato ya katiba za
washirika. Siku moja baada ya kuzinduliwa kwa Rasimu tulianza
kuwasikia viongozi wachache, na hata wahariri wa magazeti,
wakitoa maoni yao juu ya katiba ya Tanganyika. Wengine walidiriki
kusema wala hakuna haja ya kusuburi kupitishwa kwa Rasimu,
maandalizi yaanze mara moja. Wachache, wakiwemo viongozi
waandamizi, walinukuliwa wakisema wala hakuna haja ya kupata
maoni ya Watanganyika kwa sababu maoni yamekwishatolewa
kwa Tume ya Mzee Warioba. Na wakaongeza kwamba wajumbe wa
Tume ya Warioba kutoka Tanganyika wanaweza kugeuzwa kuwa
Tume ya Katiba ya Tanganyika. (Nisingeshangaa kama mwingine
angesema wala hakuna haja ya kuwa na Bunge la Katiba, Wabunge
kutoka Bara katika Bunge lililopo wanaweza wakajigeuza kuwa
Bunge la Katiba.) Kiongozi mmoja wa serikali, kutokana na
busara na uzoefu wake, amekaririwa akasema kwamba mchakato
wenyewe hautachukua muda. Kwamba ukianza mara baada
ya uzinduzi wa Katiba ya Muungano mwezi wa Aprili unaweza
34
ukamalizika Desemba 2014 na 2015 tukawa na uchaguzi wa
Bunge na Rais wa Tanganyika pamoja na uchaguzi wa Bunge la
Muungano na Rais wa Muungano. Mimi binafsi nilibaki kuduwaa
kuona jinsi tulivyomeza mwendo wa fastafasta!
Kwanza, sio sahihi hata kidogo kuzumguzia jambo ambalo hatuna
uhakika nalo hata kidogo. Kwa nini tuwachukulie wananchi wetu ni
kama mbumbumbu ambao watakubali chochote wanachoambiwa
pamoja na rasimu hii? Mabaraza hayajaijadili; wananchi wenyewe
hawajaijadili ingawa wameanza kutoa maoni yao, pamoja na
hisia zao za hofu na wasiwasi. Rasimu ya pili haijatoka; hatujui
marekebisho yatakayofanyika. Bunge la Katiba halijaketi. Hatujui
kwamba litapitisha rasimu hii bila mabadiliko, tena makubwa.
Kura za maoni bado.
Pili, nani ameamua kwamba mchakato wa kupata katiba ya
Tanganyika, ikiwa muundo wa serikali tatu utapita, utafanana
na ule wa katiba ya Muungano? Mchakato wa kupata katiba ya
Tanganyika unaweza ukawa tofauti kabisa; unaweza ukawa bora
zaidi na wa demokrasia pana zaidi. Inawezakana kabisa kwamba
mchakato wa katiba mpya ya Tanganyika usianze na tume bali na
mkutano wa kitaifa wa kujenga mwafaka.
Tatu, sio sahihi kisiasa au kimantiki, kusema kwamba wananchi
wamekwishatoa maoni yao, kwa hivyo hakuna haja ya kurudi kwao.
Walipotembelewa na Tume ya Warioba maoni waliyokuwa wakitoa
ni juu ya katiba ya Muungano, sio ya Tanganyika wala Zanzibar.
Mfano uliokuwa mbele yao ulikuwa wa katiba ya Muungano, sio
wa Tanganyika. Labda zaidi ya asilimia 95 wala hawajui kwamba
tuliwahi kuwa na Katiba ya Tanganyika. Ni kweli kabisa, maoni
yaliyotolewa mbele ya Jaji Warioba yalikuwa ni manunguniko na
matakwa yao. Sasa Tume inasema haiwezi kushughulikia mambo
mengi ya msingi, kama vile rasilimali na madaraka ya umma, kwa
hoja kwamba katika muundo waliopendekeza mambo haya ni ya
35
Washirika na sio ya Jamhuri ya Muungano. Je, nani anajua kwamba
wananchi wameridhika na hoja hiyo? Je wananchi wakisema
kwamba Rasimu irejeshwe kwenye Tume ili Tume ifanye kazi ya
ziada kuutafuta muundo ambao utashughulikia kikatiba mambo
yao ya msingi?
Ukweli ni kwamba, kuna mengi hatujui wala hatuwezi kutabiri,
kiasi kwamba kuanza mjadala wa mchakato mwingine wakati huo
uliopo wenyewe haujafikia tamati, ni sawa na kupiga ramli. Na, nne,
kuna hatari katika kufanya hivyo. Ni sawa na kuwapotoshea lengo
wananchi kwa kuanza mjadala mwingine kabisa na kuwafanya
waache kujadili hili ambalo liko mbele yao. Sina haja ya kuongeza
zaidi juu ya suala ambalo ni wazi.
Kabla sijahitimisha nigusie, angalau kwa muhtasari, matumaini ya
wananchi ya Tanzania Mpya.
IV. MATUMAINI YA TANZANIA MPYA
Tulipoanza mchakato wa katiba mpya, wengi wetu, pamoja na
wananchi wa hali ya chini, tulikuwa na matumaini kwamba
tutajadili na kujiwekea hatma mpya ya nchi yetu yenye matumaini
na mwelekeo unaojali walio wengi, hususan wavujajasho. Maoni
mengi yametolewa na wananchi, mengi yakiwa manunguniko,
matatizo na hali ngumu ya maisha kwa jumla. Ilikuwa ni juu ya
wajumbe wa Tume, kwa busara zao, na utaalam wao, kufanya
uchambuzi, kuyaainisha maoni na kutafsiri matakwa ya wananchi
katika lugha na dhana ya katiba.
Haraka haraka tunaweza kusema kwamba maoni mengi ya
wananchi yalijikita kwenye maeneo matatu ya msingi yanayogusa
maisha yao kwa karibu. Moja, ni demokrasia kwa maana ya
madaraka ya umma - demokrasia itakayowawezesha wananchi
36
vijijini na mitaani kuweza kujiamulia mambo yao wenyewe. Pili, ni
udhibiti, usimamizi na uangalizi wa rasilimali na maliasili za taifa
ili utajiri huo uweze kuwanufaisha wananchi na vizazi vijavyo.
Tatu, ni mpango, mazingira na taratibu zitakazotoa kipaumbele
kwa huduma za lazima na bora kwa wananchi waliowengi,
kama elimu, afya, maji safi, makazi bora, hifadhi ya uzeeni, na
ajira stahiki kwa vijana. Kwa jumla, ilitegemewa kwamba Tume
ingependekeza mfumo na muundo wa siasa, utawala, uchumi, na
mazingira utakaokidhi matakwa haya.
Kwa mfano, madaraka ya umma, kwa maana ya mfumo wa serikali
za mitaa kuanzia ngazi za chini kabisa kama kijiji, shehia, mtaa
na kuendelea, hayajawekewa masharti ya kikatiba. Rasimu
haikuzungumzia kabisa serikali za mitaa, isipokuwa ibara
ndogo moja ambayo inasisitiza kwamba serikali za Washirika
‘zitawajibika kustawisha mamlaka ya wananchi kwa kugatua
madaraka kwa serikali za mitaa zitakazoanzishwa’ kwa mujibu
wa Katiba za Washirika. Hili halina uzito wa maana kwa sababu
inawaachia Washirika mambo muhimu ya kuainisha mfumo
wa demokrasia. Hoja ya Tume ni kwamba jambo hilo, pamoja
na lile la rasilimali na huduma za elimu, afya n.k. sio mambo ya
Muungano na ni juu ya Washirika kuyashughulikia katika katiba
zao jinsi wanavyoona inafaa. Ni vigumu kuikubali hoja hii kwa
sababu Katiba ya Shirikisho, inatakiwa, kama katiba mama,
kuweka misingi ya mfumo na miundo ya mambo haya ya msingi.
Kitakachofanyika na katiba za Washirika ni kufafanua, kwa mujibu
wa hali yao halisi, bila kuivunja misingi iliyowekwa na katiba ya
Shirikisho. Haieleweki kwa nini, kwa mfano, haki za binadamu
zimewekwa kwa ufasaha mkubwa katika Rasimu wakati haki za
binadamu sio jambo la Muungano. Kwa nini, kwa mfano, tunu,
malengo n.k. yame rudiwarudiwa katika rasimu wakati hizi
zinaweza zisitiliwe mkazo katika Katiba za Washirika? Na papo
hapo hoja inatolewa kwamba madaraka ya umma na usimamizi
37
wa rasilimali sio jambo la Muungano na kwa hivyo hayakuguswa
na rasimu. Hoja hii, kwa heshima, haina mshiko.
Inaelekea tulitarajia mlima, tukapewa kichuguu. Hata hivyo, labda
hatujapoteza yote. Hii ni rasimu ya kwanza, bado kuna nafasi
ilimradi tuhakikishe kwamba mijadala juu ya rasimu haiharakishwi
na inakuwa huru bila kuingiliwa, na wananchi kutishwatishwa.
Wananchi waielewe vizuri rasimu na maana yake halisi kwa undani
ili waweze kuijadili na kuitafakari kikamilifu na kwa kina.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha mhadhara wangu nitarejea kwenye udhani
au hypothesis yangu. Nilisema kwamba ninavyodhani mimi,
masharti mengi ya Rasimu yalikuwa maamuzi ya maelewano kwa
maana ya compromise na sio mwafaka kwa maana ya consensus.
Baada ya uchambuzi wangu, ninadiriki kusema kwamba muundo
wenyewe wa serikali tatu uliopendekezwa ni compromise kati ya
wale waliosimamia serikali mbili na wale waliopigania muungano
wa mkataba, kwa maneno sahihi, kuuvunja muungano. Wanaserikali
mbili waliona afadhali kuwa na Muungano, hata kama ni
wa serikali tatu, badala ya kuuachia uvunjike; wakajifariji kwa
matumaini ya dhamira ya wananchi na nia ya viongozi.
Wana-mkataba wakaona kuwa kwa wakati huu wakubali serikali
tatu wakijua fika kwamba muundo wa serikali tatu hautadumu na
vyovyote vile utavunjika.
Nilisema pia kwamba compromise inazaa uamuzi legelege.
Compromise juu ya muundo, kwa maoni yangu, imezaa muundo
wa muungano legelege. Kuna maeneo mengi nimechambua
na kudhihirisha kwamba yatazaa migogoro ambayo hatimaye
inaweza kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea,
safari hii kutoka pande zote mbili.
38
Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika,
awe wa Tanganyika au wa Zanzibar. Tuna mifano mingi ya hivi
karibuni. Shirikisho la Sovieti liliposambaratika, likazaa migogoro
na vita vya wenyewe kwa wenyewe – mgogoro wa mpaka kati ya
Uzbekistan na Krygistan; mgogoro kuhusu maji kati ya Uzbekistan
na Tajikistan; vita vya Chechnya visivyoisha; vita kati ya Azerbaijan
na Armenia, n.k. Waliofaidika ni mashirika ya kibeberu ambayo
walitua kama tai kupora rasilimali za Urusi.
Shirikisho la Yugoslavia lilipogawanyika likazaa vita katika eneo
lile kiasi kwamba mpaka leo halijatulia. Wanasiasa wenye uchu
wa madaraka wakisukumwa na nchi za Magharibi, wakatumia
uhasama wa jadi kati ya makabila na dini kushawishi mgawanyiko.
Makabila na dini zilizofanya kazi kwa pamoja, kwa kiasi fulani, chini
ya uongozi wa Rais Tito, na mfumo wa Shirikisho, yakagawanyika.
Leo hii nchi ambayo ilikuwa na amani kwa zaidi ya miongo mitatu
imegawanyika katika nchi kama saba (Croatia, Serbia, Bosnia,
Macedonia, Montenigro, Kosovo na Slovenia). Na vita bado
vinaendelea. Waliofaidika ni nchi za Magharibi kupitia NATO yao.
Mwandishi mmoja anaweka wazi maslahi ya nchi za Magharibi
katika kusambaratisha Yugoslavia. Nimnukuu kwa sababu mfano
huu una mengi ya kutufundisha:
Beginning in 1990 Germany and the United States
sought and achieved the breakup of Yugoslavia
in two stages—1992-1995 and 1998-1999. The
German government aimed at this division because
it wanted to include as territory of its “vital interest”
Slovenia and Croatia, the most economically
developed states of the Yugoslavian confederation. …
Through them Germany would achieve access to the
Adriatic Sea.
39
The United States was interested in the more recently
established states (Bosnia, Serbia, the former Socialist
Republic of Macedonia), which controlled the only
route from east to west and from north to south through
the Balkan mountains. The Balkan area, along with
Romania, Bulgaria, Turkey and the Arab nations, forms
a European-Middle East bloc, which the United States
wants to control (including the former states of the
Soviet Union—Kazakhstan, Azerbaijan, Turkmenistan,
Tajikistan) for the complete exploitation of the great oil
resources of the Caspian Sea.10
Na hapa, karibu na nyumbani, Sudan ya Kusini ilipojitenga
kumekuwa na migogoro juu ya mafuta, ambayo bado inaendelea.
Nimewahi kusema na ninarudia. Suala la Muungano sio letu tu.
Kuna nchi za kibeberu zina maslahi makubwa ya rasilimali pamoja
na ya kijeshi katika eneo letu, hasa Bahari ya Hindi. Tukibeza
mambo haya nyeti kwa sababu tu ya uchu wa madaraka ya viongozi
wachache, tutawapeleka watu wetu kwenye hali mbaya.
***
Tume imesema, ingawa hatujaiona taarifa yao rasmi bado, kwamba
wananchi wengi walitaka serikali tatu. Lakini, kwa heshima,
ningependa kuhoji msimamo huu. Jukumu la Tume halikuwa tu
kukusanya maoni na kuhesabu nani amesema nini. Jukumu la
Tume lilikuwa ni kupokea maoni, kuyaainisha na kuyachambua
ili kupata kiini chake na sababu zake. Wajumbe walipoambiwa na
wananchi wa eneo moja kwamba wajengewe india ndogondogo,
haikumaanishwa hivyo, bali wananchi walikuwa wanadai hospitali;
kwa kuwa viongozi wanapelekwa India kupata huduma za kiafya,
basi wao pia wakataka wajengewe hospitali bora katika maneneo
yao na wote, viongozi na wananchi, watibiwe humohumo nchini.
40
Hatimaye, ukiangalia kwa undani kero za Muungano, kwa
mfano, suala lenyewe sio idadi ya serikali bali ni la demokrasia.
Wazanzibari kwa muda mrefu tu wamedai haki yao ya kujiamulia
mambo yao wenyewe; kushirikishwa katika maamuzi muhimu;
kutokudhalilishwa, na kupewa heshima ya mshirika huru. Madai
haya ni halali. Hoja yangu kwa muda mrefu ni kwamba tusiangalie
suala la Muungano kwa jicho la idadi ya serikali bali kwa mtazamo
wa demokrasia. Na tukifanya hivyo tunaweza kubuni muundo
wa kipekee kutokana na historia yetu na hali halisi ya Washirika
kutokuwa na uwiano wa uchumi, eneo au idadi ya watu.
Muundo wa serikali tatu, au shirikisho kama unaoainishwa,
unajikita kwenye usawa wa kisiasa (political equality). Kwa msingi
huu, uwakilishi, hususan katika vyombo vya kuchaguliwa, hauna
budi uwe sawa bila kujali idadi ya watu. Lakini katika hali yetu
ya uchumi, mchango wa Washirika katika gharama za shirikisho
hauwezi ukawa sawa, wala sio haki, kwa sababu hatuna usawa wa
kiuchumi. Kwa vyovyote vile, Tanzania Bara itachangia asilimia
kubwa ya gharama za Shirikisho. Hatimaye, anayelipa mpiga
zumari ndiye anayechagua wimbo.
Kwa maoni yangu, kama tungekuwa na mtazamo wa kidemokrasia
tungeweza kubuni muundo ambao unakidhi matakwa ya pande
zote mbili bila hatari ya kuuvunja Muungano. Mimi binafsi
nimewahi kutoa pendekezo la muundo mbadala. Mara ya kwanza
niliwasilisha pendekezo langu kwa Baraza la Wawakilishi kama
miezi michache iliyopita. Kwa muhtasari, nilipendekeza dola
kamili mbili, la Zanzibar na la Muungano. Bunge la Muungano
litakuwa na mabaraza mawili, Baraza la Wananchi na Baraza la
Nchi. Wajumbe wa Baraza la Wananchi watachaguliwa moja
kwa moja na wananchi wa pande zote mbili kutoka majimboni.
Baraza la Nchi litakuwa dogo lenye, tuseme kama wajumbe 30,
15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar wakichaguliwa na Bunge
41
la Zanzibar na wabunge kutoka Bara katika Baraza la Wananchi
ilimradi wasiwe wajumbe wa bunge lolote lile. Na nilipendekeza
orodha tatu – moja ya mambo ya muungano, nyingine ya mambo
ya kushirikiana (concurrent matters) na orodha ya tatu ni juu
ya mambo ya pamoja (joint interest). Kutokana na muda siwezi
kufafanua; nia yangu ni kudhihirisha kwamba muundo mbadala
unawezekana.
Rasimu imezinduliwa. Imeanza kujadiliwa. Tuchukue nafasi hii
kuijadili kwa makini ili hatimaye malengo na matumaini ya walio
wengi yatimizike.
Makamu Mkuu wa Chuo, wanakigoda wenzangu, rafiki zangu na
wageni waalikwa. Mhadhara huu ulikuwa ni mchango wangu wa
mwisho katika wadhifa wangu wa Nyagoda wa Mwalimu Nyerere
lakini, nikiwa na uzima wa afya, hautakuwa mchango wangu wa
mwisho katika mijadala ya kitaifa.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Ahsanteni na kila la heri.
42
MAREJEO
Mahairas, Evangelos ‘The Breakup of Yugoslavia’,
http://www.iacenter.org/folder02/hidden_em.htm
(nilitembelea 16/06/2013)
Nwabueze, Ben. 2003. Constitutional Democracy in Africa. Ibadan:
Spectrum Books.
Seervai, H. M. 1997. Constitutional Law of India: A Critical
Commentary. 4th edn., Mumbai: Universal Book Traders.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Toleo la 2010.
Shivji, Issa G. 1990/2009. The Legal Foundations of the Union. Dar
es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Singh, Mahendra P. 1994. V. N. Shukla’s Constitution of India. 9th
edn., Lucknow: Eastern Book.
Tanzania, Jamhuri ya Muungano. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2013. Dar es Salaam:
Mchapishaji wa Serikali.
Tanzania, Jamhuri ya Muungano. Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya Mwaka 1977. Dar es Salaam: Mchapishaji
wa Serikali.
Wheare, K. C.. 1966. Modern Constitutions. London: Oxford
University Press.
43
(Endnotes)
1 http://www.tzaffairs.org/2012/05/tanzanias-exclusive-economiczone/
2 Rasimu haitumii neno Tanganyika, bali Tanzania Bara.
3 ‘Rendition’ ni mazoea ya mashirika ya ujasusi ya Marekani
kumkamata mtu anayeshukiwa kuwa gaidi katika nchi moja na
kumpeleka kuhojiwa katika nchi nyingine.
4 Jambo hili sio geni kwetu. Watu wa FBI (Federal Bureau of
Investigation) ya Marekani wamekwishaanza kuingia nchini kuhoji
na kuwasumbua wananchi wetu wasio na hatia.
5 Na hili limewahi kutokea. Bunge la Muungano lilipopitisha sheria ya
Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora, mamlaka ya Zanzibar
waliwakatalia wajumbe wa Tume kufanya shughuli zao Zanzibar kwa
hoja kwamba haki za binadamu sio jambo la Muungano. Hatimaye,
walifikia maelewano kwa Baraza la Wawakilishi kupitisha sheria
yao ya kutambua Tume kwa masharti.
6 Mfano huu sio wa kinadharia tu. Baadhi ya waheshimiwa
wamekwishaanza kuonyesha wasiwasi wao kuhusu mgombea huru
kuruhusiwa kugombea chaguzi zote kutoka ngazi za chini mpaka juu.
7 Sielewi kwa nini rasimu inaendelea kutumia lugha hii ya ‘mapinduzi’
na ‘Baraza la Wawakilishi’. Hatujui kwamba ama katiba mpya,
au hiyo itakayorekebishwa, ya Zanzibar itatumia msamiati huo.
Inawezekena kabisa, kwa mfano, wakiite chombo chao cha kutunga
sheria Bunge la Zanzibar.
8 Tukiendelea na msamiati wa serikali tatu tutaingia kwenye
malumbano yaleyale ya kama Zanzibar ni nchi au sio nchi. Kwa
maelezo zaidi juu ya dhana ya nchi, taifa na dola, angalia makala
yangu katika gazeti la Tanzania Daima, Julai 20, 2008.
9 Marekani, Mexico, na India wana maeneo maalum ya Makao Makuu
ya Serikali ya Shirikisho ambayo yanaitwa Eneo la Shirikisho.
10 Evangelos Mahairas, ‘The Breakup of Yugoslavia’,
http://www.iacenter.org/folder02/hidden_em.htm

No comments:

Post a Comment