Wednesday, June 12, 2013

Nimejichimbia bado naisoma rasimu ya katiba mpya....

Ndugu zangu,

Wamejitokeza watu wengi sana kujadili rasimu ya katiba mpya, lakini nami naahidi nitajitokeza kujadili kwa mkabala wa jinsia na hali zote. Nataka kuijadili nikiwa mtoto, mwanamke, mwanamme, kijana, mzee, muislamu, mkristo ama nisiye na dini.

Kifupi nataka kuijadili katiba nikiwa mtanzania ninaeguswa na hali zote. Maana wapo watoto ambao hawajui kusema wala kudai haki zao, wapo mabinti ambao hawajui kusoma wala kujieleza, kadhalika wapo vijana ambao hata hawajui maana ya rasimu ya katiba mpya seuze katiba yenyewe.

Hivyo nimejichimbia, naisoma kwa kina kipengele hata kipengele ili kuweza kuibuka na kitu kamili ambacho kitaweza kuisaidia jamii. Hakuna kitu kibaya katika maisha kama kukurupuka.

Sina taaluma ya sheria, lakini nitaijadili kwa mkabala wa kujua haki zangu, vipengele vyote vipo wazi. Nitazungumza kwa kuguswa na haja ya kuweza kuwa mmoja wa wadau wa nchi hii changa.

Nafahamu tunaingia katika sura mpya ya mkataba wa kijamii (social contract) ambao unahitaji uangalifu wa hali ya juu kuujadili mkataba huu kwa maslahi ya kila mmoja. Hatupaswi kuwaacha wachache wakaona wanaonewa ama kuwasusia wengi wakaona wana haki zaidi ya keki ya taifa.

Sote inatuhusu na tutaijadili kwa pamoja.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
12 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIANo comments:

Post a Comment