Tuesday, June 18, 2013

MTANZANIA APEWA ITC ACHEZE YEMENShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira nchini Yemen.

 Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.

 TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen.KLABU THAILAND YASAKA WACHEZAJI TANZANIA

Klabu ya Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine barani Ulaya.

 Kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo.

 Wachezaji wenye nia ya kufanya majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji (player passport).

Wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).

 MECHI DHIDI YA IVORY COAST YAINGIZA MIL 500/-

Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kundi C, Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) imeingiza sh. 502,131,000 kutokana na watazamaji 57,203.

 Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 76,596,254.24 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,809,104.

Asilimia 15 ya uwanja sh. 62,658,846.26, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 83,545,128.35 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 20,886,282.09.

Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 250,635,385.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 12,531,769.25 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.

 Mechi iliyopita ya Stars dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) kwenye uwanja huo iliingiza sh. 226,546,000.

 TAIFA STARS KAMBINI TENA JULAI 4

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameiita tena kambini timu hiyo Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inavunja kambi leo (Juni 17 mwaka huu) baada ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, kundi C Kanda ya Africa dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kim amesema wachezaji watakaoitwa kambin ni wote walioko kwenye timu hivi sasa isipokuwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika klabu ya TP Mazembe Englebert.

Wachezaji hao ni Juma Kaseja, Aishi Manula, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

 Mechi hiyo namba 37 dhidi ya Uganda (The Cranes) itachezwa jijini Dar es Salaa kati ya Julai 12 na 14 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika wiki mbili baadaye katika Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.

RWIZA KUHUDHURIA SEMINA YA MAKAMISHNA CAF

Kamishna Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri.

Semina hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014.

Rwiza ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu nchini  Msumbiji.

CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.


Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Juni 18, 2013

No comments:

Post a Comment