Thursday, June 13, 2013

Mugabe kugombea tena Urais Zimbabwe.... Mwezi ujao?

Mzozo wa kisiasa umeibuka nchini Zimbabwe baada ya rais Robert Mugabe kutoa agizo kuwa uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika tarehe 31 Julai mwaka huu.

Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, ametoa taarifa muda mfupi tu baada ya agizo hilo la rais, akisema kuwa rais Mugabe amekiuka sheria kwa kutoshirikisha bunge na ameapa kupinga uamuzi huo.


Katika kikao na waandishi wa habari, Tsvangirai, amemshutumu Bwana Mugabe kwa kukiuka mkataba wa ugavi wa mamlaka uliosainiwa miaka mitano iliyopita, baada ya mzozo kuhusu matokeo ya kura kusababisha ghasia nchini humo.

Tsvangirai ametaka uchaguzi huo kuhairishwa hadi mageuzi ya kikatiba yafanyike ili kuhakikisha zoezi hilo la uchaguzi linafanyika kwa njia huru na haki.

Bunge la nchi hiyo bado linajadili mswada wa sheria ambao utaruhusu vyama vyote vya kisiasa kupewa nafasi sawa katika shirika la habari la serikali wakati wa kampeini.

Lakini wiki mbili zilizopita mahakama ya kikatiba nchini humo iliagiza kuwa uchaguzi huo ni sharti ufanyike kabla ya mwisho wa Julai.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment