Thursday, June 20, 2013

Serikali iingilie kati kunusuru vifo vya vijana.

                             Ndugu jamaa na marafiki wakiaga mwili wa mpendwa wao Langa Kileo.

M 2 The P, mwenye kofia akiaga mwili wa rafiki yake Albert Mangweha ambaye alikufa nchini Sfrika Kusini, Mangweha na M2 The P ni wasanii wa kizazi kipya ambao walikutwa hawajitambui chumbani nchini humo. Walipowahishwa hospitali Mangweha alifariki dunia lakini mwenzake alibaki katika hali mbaya mpaka baada ya siku tatu aliporuhusiwa.

Wiki hii mwanamuzi mwingine wa bongofleva Langa Kileo, amezikwa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inakuwa ni tofauti ya wiki moja tu tangu mwanamuziki Albert Mangweha kuzikwa mjini Morogoro.

Kwa nyakati tofauti enzi za uhao wao wanamuziki hawa walikuwa wakihusishwa na matumizi ya dawa za kulevya, hakuna taarifa za daktari zinazothibitisha vifo vya wanamuziki hao kusababishwa na matumizi ya dawa za kulevya lakini inawezekana kwa namna moja ama nyingine kudhoofika afya zao kulisababishwa na janga hilo.

Nchini Marekani idadi ya vifo vinavyosababishwa na matumizi ya madawa ya kulevya kwa wanamuziki inaongezeka siku hadi siku, lakini takwimu zinasomeka tofauti kwani asilimia kubwa ya wanamuziki wanaokutwa wamekufa vyumbani mwao ni wale ambao wamepata mafanikio makubwa kwa nyakati fulani na kuporomoka kiuchumi ama kisanaa.

Lakini kwa Tanzania asilimia kubwa ya vijana wanajitumbukiza katika janga hilo ili kuondokana na msongo wa mawazo kutokana na kuibiwa kazi zao na wamiliki wa vituo vya radio, mameneja wao au wasambazaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2011 kutoka tume ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya, inaonyesha kuwa mwaka 2011 kilo 264.3 ya Heroin ilikamatwa wakati mwaka 2010 zilikamatwa kilo 185.8 ya dawa hizo ambapo ni ongezeko la asilimia 42.

Mwaka 2011 zilikamatwa kilo 126 za Cocaine nchini wakati mwaka 2010 zilikamatwa kilo 63 ambapo hilo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 100 ndani ya mwaka mmoja. Wakati kutokana na taarifa hiyo iliyotiwa saini na waziri wa nchi sera uratibu na bunge, William Lukuvi inaeleza kuwa umri wa watumiaji wa dawa za kulivya unaanzia miaka 12 mpaka 35. 

Katika Afrika nchi iliyopata kuweka rekodi ya kusafirisha dawa hizo ni Cape Verde ambapo mwezi Octoba 2011 zilikamatwa tani 1.5 zikitokea nchi za Marekani ya Kusini. 

Aidha wanamuziki wengi mbali ya kutumia dawa hizi pia wanatumika kuzisafirisha kutoka bara la Ulaya, Asia na Marekani ya kusini. Zipo kesi nyingi za wasanii wa bongofleva kuhusishwa na usafirishaji na uingizaji wa dawa hizi nchini.

Langa kabla hajaaga dunia alikuwa na mipango ya kuanzisha 'NGO' ya vijana kupinga matumizi ya dawa hizo, kwa bahati mbaya ndoto zake hazikutimia lakini bado wapo wasanii ambao wanaweza kuenzi mchango wake kwa kuendeleza mawazo hayo chanya.

Serikali kupitia Wizara ya kazi maendeleo ya vijana na ajira, inabidi kulifikiria mara mbili suala la dawa za kulevya hasa kwa wanamuziki wetu ambao kwa kiasi kikubwa wanapendwa na kufuatwa kwa karibu na vijana wenzao.


HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
20 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment