Profesa Saida Yahya Othman akiwakaribisha wageni kabla ya ufunguzi ukumbi wa Nkrumah leo. |
Kutoka koshoto Mzee Joseph Butiku, Profesa Ibrahim Lipumba na Mzee Kingunge Ngombale wakifuatilia mada ya profesa Shivji leo.
Profesa Mukandala ambaye ni makamu mkuu wa chuo cha Dar es Salaam akizindua kitabu cha Profesa Thandika ambaye alikuwa profesa mwalika katika kigoda cha Mwalimu mwaka huu. |
Dk. Bashiru Ally akighani shiri la kumuaga profesa Shivji leo. |
Miongoni mwa wanaharakati naye akizungumza mawili matatu juu ya mustakabali wa Tanzania. |
Mwakilishi wa wanaharakati wa haki za binaadamu Bi Angela Kijo Bisimba akichangia mada leo. |
Akizungumza katika tamasha hilo Chuo kikuu cha Dar es Salaam katika ukumbi maarufu wa Nkrumah leo mchana profesa Shivji ameeleza kwa kina juu ya utatanishi na ukimya katika rasimu ya katiba mpya ya Tanzania hasa katika kipengele cha muungano na matumaini ya Tanzania mpya.
"Niliposimikwa mnamo tarehe 18 Aprili, 2008 kuwa profesa wa kigoda cha Mwalimu Nyerere katika umajumui wa Afrika, nilitoa mhadhara wa uzinduzi juu ya 'Umajumui wa Afrika katika Fikra za Mwalimu'. Sasa ninakaribia kumaliza muda wangu hapo tarehe 31 Agosti, 2013 nimeona si vema nikiondoka bila kutoa mhadhara wa kuaga kigoda, wanakigoda na wanachuo wenzangu na wale wote waliokuwa pamoja nasi katika shughuli na mijadala yetu," alisema profesa Shivji.
Aidha alipozungumzia katiba mpya alisema watanzania wengi walipokuwa wakitoa maoni walikuwa wanatoa katika mfumo wa malalamiko wakiamini mambo yatakuwa mazuri baada ya katiba mpya kuja. Hivyo si busara katiba ikaja kinyume na matarajio ya watanzania maskini ambao ndiwo wengi.
Profesa Shivji aliongeza kuwa matokeo ya rasimu hiyo ni mivutano katika tume ya mabadiliko ya katiba baada ya wajumbe kutofautiana mitazamo, hivyo kwa maslahi ya taifa wameamua maelewano na si kupatana. Kwani kila mmoja ametoka katika chumba cha mikutano huku amenuna lakini lengo ni kuhakikisha katiba inapatikana kwa wakati.
"Usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba rasimu hii ni maelewano kwa maana ya 'compromise' na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus. katika maelewano au 'compromise' pande zinazokinzana hatimaye zinakubali kwa shingo upande ili kutokukwamisha maamuzi. Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili. Kwa hiyo maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi. Maelewano au 'compromise' yanazaa uamuzi legelege.
"Mapatano au 'consensus' kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi," alisema Profesa Shivji.
Katika hatua nyingine Professa Shivji alizungumzia suala la serikali tatu na kuweka wazi msimamo wake kuwa hakuna haja ya kuangalia muungano utakuwa wa serikali ngapi bali cha kuzingatia ni muundo wa namna gani utasaidia kuleta ahueni ya kimaisha na kuwa na demokrasia safi.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
21 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment