Thursday, June 13, 2013

TIKETI MECHI YA STARS NA IVORY COAST KUANZA KUUZWA KESHO



Wakati timu ya Ivory Coast inatarajiwa kuwasili leo usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, tiketi kwa ajili ya mechi kati yake na Taifa Stars itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa zinaanza kuuzwa kesho mchana (Juni 14 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.



Vituo vitakavyotumika kwa mauzo hayo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.



Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, sh. 7,000 viti vya rangi ya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.



Pia viti 100 vilivyo katika sehemu ya Wageni Maalumu (VVIP) vitauzwa kwa sh. 50,000 kila kimoja. Tiketi hizo zitauzwa katika ofisi za TFF, na watakaonunua watapewa kadi maalumu zenye majina yao, majina ambayo pia watayakuta katika vita watakavyokaa. Kwa maana hiyo hakutakuwa pasi maalumu (free pass) za kuingia VVIP.



PONGEZI KWA RAIS MPYA WA ZFA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amempongeza Rais mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous Faina aliyechaguliwa katika uchaguzo mdogo uliofanyika hivi karibuni.



Amesema ushindi aliopata Faina unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA walivyo na imani naye katika kuhakikisha maendeleo ya mpira wa miguu visiwani humo.



Rais Tenga amesema ni imani yake kuwa Rais Faina ataendeleza ushirikiano uliopo kati ya TFF na ZFA kwa ajili ya ustawi wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumtakiwa kila kheri katika wadhifa wake huo mpya.



WAAMUZI WATATU WAFUNGIWA MIEZI MITATU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefungia miezi mitatu waamuzi watatu walioshindwa kuchezesha mechi namba 32 ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Mpwapwa Stars ya Dodoma na Machava FC ya Kilimanjaro iliyokuwa ichezwe Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.



TFF kupitia Kamati yake ya Waamuzi iliyokutana katika kikao chake cha Juni 12 mwaka huu kupitia taarifa mbalimbali za waamuzi wa RCL ilibaini makosa yaliyofanywa na baadhi ya waamuzi na kuyatolea uamuzi.



Waamuzi hao waliofungiwa ambao wanatoka mkoani Singida ni Jilili Abdallah, Amani Mwaipaja na Theofil Tegamisho. Wamefungiwa kwa kutoripoti katika kituo walichopangiwa (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma) na kutoa taarifa ya uongo kwa kushirikiana na Kamishna wa mechi hiyo.



Kanuni iliyotumika kuwafungia ni ya 28 kifungu (d) na (g) ya Ligi za TFF, na adhabu hiyo imeanza Juni 13 mwaka huu. Waamuzi hao pamoja na kamishna badala ya kwenda Uwanja wa Jamhuri, wao walikwenda kwenye Uwanja wa Mgambo ulioko Mpwapwa na kuandika ripoti iliyoonesha kuwa timu ya Machava FC haikufika uwanjani wakati wakijua kuwa mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa katika Uwanja wa Jamhuri.



Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Juni 13, 2013



No comments:

Post a Comment