Sunday, June 16, 2013

Mwenyekiti Maggid Mjengwa azungumzia serikali tatu.... na suala la historia.

Muungano wa nchi MBILI unapaswa uzae nchi MOJA. Hivyo, Serikali MOJA pia. Tanzania ni muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hata hivyo, Zanzibar kuna Serikali ya Mapinduzi tangu mwaka 1964. Tanganyika hakuna, na jina pia halitumiki.

Tuukubali ukweli, kuwa katika kilichoanishwa hapo juu, ni vigumu kuzungumzia Muungano wa Serikali MBILI badala ya MOJA au TATU.

Haiyumkini kuwa Majaji wetu na tume zao, kuanzia Jaji Nyalali, Kissanga na sasa Warioba, wameliona tatizo ambalo halipo na kuwa mapendekezo yao hayastahili kupewa uzito na kufanyiwa kazi.

Ikumbukwe, kuwa Tume ya Jaji Warioba inaundwa na watu wenye hekima na busara nyingi akiwamo Mzee Salim Ahmed Salim na Jaji Mstaafu Augustine Ramadhani. Ni juzi tu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji Mark Bomani ameweka hadharani, kuwa muda wa kuwa na Serikali Tatu umefika.

Naam, umefika wakati wa kuukubali ukweli, kuwa kwa muundo huu wa Muungano tulio nao sasa, siku zote kutakuwa na manung’uniko. Kuukataa ukweli huu ni sawa na kufagilia takataka chini ya jamvi. Iko siku jamvi lazima liinuliwe na uchafu huo utaonekana tu.

Majuzi tu, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia alizungumzia Rasimu ya Katiba kama jitihada za ubunifu katika kufikia mwafaka wa mazungumzo kuhusiana na kero za Muungano.

Balozi Mahiga anasema, kuwa ingawa Serikali Tatu zina gharama zake, lakini kisiasa ina manufaa yake kutokana na mijadala ya muda mrefu kuhusiana na muundo wa Muungano. Balozi Mahiga anazidi kunukuliwa akisema, kuwa iwapo Rasimu hiyo itapitishwa na Watanzania, ni wazi kwamba Tanzania itakuwa imerekebisha kasoro za Muungano unaotimiza miaka 50 mwakani, kwa njia ya mazungumzo. ( Mwananchi, Jumapili, Juni 9, 2013, Uk 2)



Tafsiri yangu?

Aliyoyasema Balozi Mahiga yana uzito mkubwa sana. Ni maneno yaliyojaa hekima na busara nyingi kutoka kwa Mtanzania na Mwanadiplomasia mzoefu. Mahiga kwenye mazungumzo yake ametanguliza masilahi mapana na ya muda mrefu ya taifa.

Nakubaliana na Balozi Mahiga kwenye usahihi wa njia ya Jaji Warioba na Tume yake kuhusiana na Serikali Tatu.

Maana, njia ni ile ile tuliyokuwa tukihangaika kuifuata huku kukiwa na kero nyingi za njiani. Ni kwa vile njia ilikuwa nyembamba mno, alichofanya Warioba na Tume yake ni kuipanua njia hiyo ili hata malori yaweze kupita.

Katiba Mpya ina maana pia ya Mabadiliko Makubwa. Ninachokiona mimi ni hofu ya mabadiliko kwa baadhi yetu. Kwa wengine ni hofu inayotokana na sababu binafsi zenye kuambatana na kupoteza fursa hata nafasi za kimamlaka katika mabadiliko yanayokuja. Hivyo, ni sababu za kibinafsi zaidi na pengine hata kimakundi.

Ni hulka ya mwanadamu pia kuogopa mabadiliko yanapotokea. Hata kwenye nyumba yako tu. Siku ukirudi nyumbani ukakuta mfanyakazi wako wa ndani kapangua fenicha na kuziweka katika utaratibu mpya , basi, utaanza kwanza kuyaogopa mabadiliko yale. Huenda akili yako isitulie pia. Kidogo kidogo utaanza kuyazoea.

Hili la Serikali Tatu kwa historia tu inabidi tupumue kwa akina Jaji Warioba kuja na ubunifu huu. Maana, imekuwa ni kero sugu iliyoundiwa hata Wizara. Hatuwezi kuendelea na hali hiyo mwaka hadi mwaka.

Maana, hata mimi binafsi, ningeulizwa mwaka 2000 juu ya muundo wa Muungano, basi, chaguo langu la kwanza lilikuwa Serikali Moja, pili, Serikali Mbili na tatu Serikali Tatu.

Lakini, miaka 13 baadaye na kwa kusoma alama za nyakati. Ukiniuliza leo swali hilo, jibu langu liko wazi kabisa, kuwa tuwe na Serikali Tatu; Ya Muungano, Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika). Hii si heshima tu tutakayoipata kimataifa, bali, itachangia kwa watu wa pande mbili hizi za Muungano kuheshimiana na kushirikiana zaidi.

Tusisahau historia, kuwa Kamati ya Jaji Robert Kissanga mwaka 2000 ilikuja na mapendekezo kama haya ya Serikali Tatu. Nakumbuka Rais Mkapa pale Diamond Jubilee akiongea na Wazee wa Dar es Salaam alionyesha dhahiri kuwa Serikali haikuyapenda mapendekezo yake.

Kukawa na hata mjadala kama Kamati inaweza kuja na mapendekezo au la, maana, ikasemwa kuwa ya Kissanga haikuwa Tume. Rais Mkapa akawashambulia pia wanahabari kwa kutaka kuishinikiza Serikali kuyakubali mapendekezo hayo. Kitu ambacho hakiwezekani, maana, Serikali hata siku moja haiwezi kushinikizwa na wanahabari kama haikubaliani na inachoshinikizwa nacho. Lakini huo ulikuwa ni mwaka 2000 na sasa ni 2013. Wakati umebadilika.

Naam na tuendane na wakati unaobadilika. Tusiwe watumwa wa historia. Tuwe na ujasiri wa kuzipa mgongo fikra za ukale. Katiba Mpya inaweza pia kuchangia tuondokane na mambo ya ovyo ovyo na yenye kutuvunjia heshima kama taifa.

0754 678 252, http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment