Tuesday, June 18, 2013

Kozi ya makocha Dar kufungwa Jumanne



KOZI ya makocha wa ngazi ya pili (Intermediate) inayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), inatarajiwa kufungwa Jumanne ijayo baada ya kudumu kwa wiki nne.
Kozi hiyo ilianza Juni 3 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Harbours Club, uliopo Kurasini chini ya Mkufunzi Rogasin Kaijage, ambaye ni Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ ambapo makocha mbalimbali pamoja na wachezaji wa zamani wamejitokeza kushiriki.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo alisema kozi hiyo imekuwa na mafanikio na wanatarajia makocha walioshiriki katika kozi hiyo watakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mpira wa miguu katika mkoa wa Dar es Salaan na Taifa kwa ujumla.
“Hadi sasa tunashukuru kuona tunafanikisha kozi hii ambayo wengi wameitikia wito, mwisho wa kozi hii ndio mwanzo wa kozi nyingine.
“Lakini haya ya kozi ya makocha ni moja ya majukumu ya Kamati ya Ufundi ya DRFA yaliyoainishwa katika Katiba, hivyo hili ni moja ya shabaha yetu na mengine mengi mazuri yanafuata,” alisema Mharizo.
 Kozi hiyo ni ya kwanza kuendeshwa na DRFA tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya wa chama hicho Desemba 12, chini ya Mwenyekiti wake Almas Kassongo.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com

No comments:

Post a Comment