Tuesday, June 18, 2013

Sudan pamekuwa salama kwa michuano ya CECAFA...

Moja ya viwanja ambako michuano ya CECAFA itachezwa Kadugli.
Katibu mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye
Kinyang'anyiro cha kuwania kombe la shirikisho la CECAFA au kilabu bingwa Afrika Mashariki na kati, kinaanza leo katika jimbo la Kordofan Kusini licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu hali ya usalama.

Baadhi ya vilabu vimegoma kwenda kwa michuano hiyo ikiwemo Yanga ya Tanzania wakieleza wasiwasi kuhusu usalama wao kwenye michuano hiyo ambayo pia inachezewa katika jimbo la Darfur.

Katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alikwenda Kordofan siku ya Jumapili na kukutana na maafisa kutoka Khartoum waliohakikisha kuwa michuano inaendelea bila wasiwasi wowote.

Maafisa wamewataka wananchi kuunga mkono michuano hiyo kwani usalama katika mviwanja vyote umedhibitiwa vilivyo.

Nia ya CECAFA ni kuonyesha kuwa maisha yanaendelea kama kawaida katika jimbo la Darfur na Kordofan Kusini licha ya mgogoro unaoendelea katika maeneo hayo.

Lakini raia wengi wa Sudan wameshangazwa sana na uamuzi wa michauano kuandaliwa katika majimbo hayo.

Moja ya viwanja ambako michuano ya CECAFA itachezwa Kadugli

Musonye pia alisema kuwa timu ya Al Nasr kutoka Sudan Kusini ilijaribu kubatili uamuzi wake wa awali, kukosa kushiriki lakini ombi lao lilikuja kuchelewa.

Kwa sasa kuna mgogoro mkubwa katika jimbo la Kordofan Kusini na katika mji mkuu wa jimbo hilo Kadugli, ambako mechi ya ufunguzi itachezwa katika uwanja ambao umewahi kushambuliwa kwa makombora mwaka uliopita.

Mzozo tofauti uliibuka katika jimbo la Darfur mwongo mmoja uliopita, na eneo hilo bado lina makundi ya watu waliojihami pamoja na makundi ya wapiganaji.

Mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, Fasher, ambao ni mwenyeji wa michuano kadhaa, ni makao kwa kikosi cha umoja wa mataifa kinachoshirikiana na muungano wa Afrika ambao wanajribu kuleta utulivu kwa eneo hilo.

Hata hivyo wakaazi wa mji mkuu Kadugli wanajiandaa kwa mechi ya kwanza ya kimataifa kuwahi kufanywa mjini humo.

Maafisa wa michuano pamoja na marefa waliwasili Jumapili mwishoni mwa wiki na kumtembelea gavana wa jimbo hilo, Ahmed Harun nyumbani kwake.

Musonye pia alikutana na Harun pamoja na kamati ya maandalizi ya michuano hiyo.


BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment