Tuesday, June 25, 2013

Shindano la urembo lilete matumaini kwa wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mshiriki wa shindano la Miss Tanzania akipita jukwaani katika hoterli ya Kilimanjaro mwaka 1967, mwaka mmoja kabla ya shindano hilo kupigwa marufuku Tanzania.
Shindano la kusaka mrembo wa Tanzania (Miss Tanzania) limeanza kupoteza umaarufu tofauti na miaka ya nyuma ambapo watu wa kila rika walivutiwa na mchakato mzima kuanzia mikoani mpaka mrembo anapokabidhiwa zawadi.

Kwa sasa warembo wanaopatikana hufanya mambo tofauti na utamaduni wa kiafrika kuanzia mavazi, kashfa za ulevi na kuvunja ndoa za watu kwa maana ya kujitumbukiza katika mahusiano mabaya ya kingono. Ama warembo wengine baada ya kurudi kutoka shindano la urembo duniani hujitumbukiza katika mambo ya uanamitindo wakitupilia mbali shughuli za kijamii.

Yupo mrembo mmoja tu ambaye ameitendea haki nafasi yake kwa kufanya shughuli za kijamii kusaidia watanzania na waafrika wanaoishi katika mazingira magumu, Heyce Temu ambaye ameshinda taji la urembo Tanzania mwaka 1999 amefanya mambo mengi kuisaidia jamii kwa sasa anaendesha kipindi cha 'Mimi na Tanzania' kwenye kituo cha luninga, Channel Ten.

Kipindi hicho cha luninga kinaangazia mambo ya kijamii hasa hali duni ya watanzania waishio vijijini, kinaonyesha uwezo wa hali ya juu namna Hoyce Temu alivyojitoa kuisaidia jamii ambayo ndiyo kazi kubwa ya shindano la urembo.

Mwaka 1951 Eric Morley kutoka Uingereza alianzisha shindao la urembo wa dunia, ambapo lengo lilikuwa kutafuta msichana mrembo zaidi duniani na mrembo wa kwanza alitoka Sweden, Kicki Hakansson alivalishwa taji akiwa amevali kichupi (Bikini). Ila mwaka mmoja baadaye wanaharakati wa jinsia walipinga uvaaji wa vichupi kwenye shindano hilo, ndipo mwaka 1952 May Louise, pia kutoka Sweden alivalishwa taji akiwa na nguo ya kutokea usiku.

Baadaye mwaka 1980 shindano hilo lilifanya mabadiliko makubwa likaanza kuijali jamii na kuja na kauli mbiu isemayo; Urembo na sababu (Beauty with Purpose) wakaanzisha utaratibu wa kupima uwezo wa mshiriki katika masuala ya kijamii, siasa, uchumi na kuanzia hapo warembo wakaanza kutumika kama mabalozi wa amani katika mataifa yenye hali duni ya uchumi na zenye vurugu za kisiasa.

Katika kusisitiza mabadiliko makubwa kwenye shindano la urembo mwaka huu hakutakuwa na kipengele cha uvaaji wa vichupi (Bikini) kwani ulimwengu unataka kuhakikisha shindano la urembo linakuwa nadhifu kadiri inavyowezekana ili mshindi anapopatikana aweze kutumikia jamii katika picha sahihi ya mwanamke mwenye heshima.
 Hoyce Temu akikabidhiwa taji lake la kuwa Miss Tanzania mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.

Hoyce Temu akiwa katika shughuli zake za kila siku kusaidia jamii hasa maeneo ya vijijini kwenye matatizo.

Tanzania shindalo hilo lilikuja rasmi mwaka 1960, lakini miaka minane baadaye baraza la umoja wa vijana la chama cha TANU lilipitisha azimio la kuzuia shindano hilo kwa hoja kwamba linakwenda kinyume na maadili ya mtanzania, ndipo mwaka 1968 ikawa mwisho wa shindano hilo.

Mwaka 1994 likarudi tena na mrembo wa kwanza akawa Aina Maeda, ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa kutokana na kukosekana maadili kwenye shindano hilo lakini jamii ililazimishwa kuamini kuwa kushiriki shindano la urembo si uhuni. Tangu mwaka 1994 mafanikio makubwa Tanzania iliyowahi kupata ni mrembo Nancy Sumari mwaka 2005 kushika nafasi ya sita katika shindano hilo na kuwa Miss World Africa.

Hashim Lundenga ambaye ni mratibu wa Miss Tanzania, kila siku akiulizwa na wanahabari juu ya maadili mabaya ya warembo wanaopatikana katika shindano hilo mara zote anasema hana mamlaka ya kubadili tabia za warembo kwani hakai nao kambini kwa muda mrefu, warembo wanatoka mikoani wakiwa na tabia zao Miss Tanzania haina uwezo wa kuwabadili. Bila ya kukumbuka lengo la mashindano hayo ni kuleta matumaini kwa jamii, jamii haiwezi kukubali kuwa na balozi asiyejitambua na ndiyo maana mpaka sasa Miss Tanzania wangu atabaki kuwa Hoyce Temu.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
26 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment