Friday, June 14, 2013

Tanzania International University hakina uwezo wa kutoa shahada: TCU.

Ofisa habari mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo asubihi katika ukumbi wa idara ya habari (MAELEZO).


Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imekitaka chuo kikuu cha kimataifa cha Tanzania (TIU) kuacha mara moja kutoa shahada mpaka watakapopata ruhusa kutoka kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi katika ukumbi wa idara ya habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam ofisa habari mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku amesema awali walishawapa onyo TIU kuacha kutoa shahada mpaka hapo watakapopata ithibati kutoka katika tume hiyo lakini inaonekana wamekuwa wagumu kuelewa.

"Tarehe 12 Aprili, 2013 TCU ilitoa taarifa kuwa chuo cha kimataifa cha Tanzania (TIU) hakiruhusiwi kupokea wanafunzi wa shahada mpaka watakapomaliza taratibu za TCU kuhusiana na masuala ya kitaaluma. Mbali ya kuwataka kusitisha huduma hiyo pia tuliwaambia warudishe ada za wanafunzi waliojiunga kwa shahada chuoni hapo kutokana na chuo hicho kukosa vigezo.

"Taarifa ilikuwa wazi kwa mlengwa na tulihakikisha inawafikia, lakini cha kusikitisha mpaka sasa hawajatekeleza agizo la tume hii ni dharau," alisema Mkaku na kuongeza "Tunataka kuuarifu umma kuwa TIU ni chuo binafsi chenye uhalali wa kutoa elimu na halali kilichosajiliwa TCU. Usajili wake ni No.CR1/082 kwa leseni hiyo ya mpito TIU kinaruhusiwa kutoa elimu ngazi ya cheti, stashahada (diploma) na kozi fupi lakini si shahada."

Alipoulizwa na kidojembe juu ya hatua zitakazochukuliwa na TCU ikiwa chuo hicho kitakaidi agizo la kusitisha kutoa shahada hasa ikizingatiwa agizo la kutofanya hivyo lilitolewa tangu mwezi wa nne lakini bado TIU hawajatekeleza kwa maana ya kusitisha huduma ya shahada.

Mkaku alijibu "Ni mapema mmno kusema tutatoa adhabu gani, maana tunaamini watatusikiliza hakuna haja ya kuwahukumu wao ni waungwana na tutegemee mrejesho mzuri."

Aidha kwa mujibu wa ofisa huyo chuo ili kitimize vigezo vya kutoa shahada ni lazima TCU wajiridhishe kuwa kuna madarasa ya kutosha, walimu wanaotambulika na elimu zao zimepatikana katika vyuo vinavyotambulika kidunia, maabara na maktaba za kutosha pamoja na mazingira rafiki kwa mwanafunzi kusoma.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA
14 June, 2013  

No comments:

Post a Comment