Tuesday, June 4, 2013

Vijue vifaa vinne vilivyotua Coastal Union kwa msimu ujao.

Haruna Moshi 'Boban' akipeana mkono wa pongezi na kocha mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco baada ya kusaini kuichezea timu hiyo kwa mwaka mmoja kuanzia msimu ujao.
Hemed Morocco akiwa na Abdallah Othman kutoka timu ya Jamhuri ya Pemba ambapo msimu ulioisha alikuwa mchezaji bora wa michuano. Othman ni winga ya kushoto ambaye anategemewa kuleta faraja katika timu ya Wagosi wa kaya.
Said Lubawa golikipa kutoka JKT Oljoro akiwa na makamu mwenyekiti wa Wagosi wa Kaya Steven Mnguto, baada ya kukubali kuichezea timu hiyo kwa msimu ujao.
Beki wa kushoto kutoka JKT Oljoro, Marcus Ndehele akiwa na kocha Hemed Morocco mara baada ya kumwaga wino kuikabia Coastal Union kwa msimu ujao.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi wa wagosi wa kaya Nassor Mohammed Binslum, kocha mkuu wa timu hiyo ndiye anayesimamia usajili baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita kinyume na malengo yao ya kushika nafasi za tatu za juu.

"Halafu mkae mkijua usajili wote huu anaufanya Morocco mwenyewe, mimi napewa maagizo tu lete huyu naleta," alisema Binslum katika ukurasa wa facebook wa Coastal Union Supporters leo asubuhi.

Aidha Coastal Union ambao ni mabingwa wa soka Tanzania mwaka 1988 walipotea katika ramani ya soka lakini walirejea tena katika msimu wa mwaka 2009 na kuonyesha soka la hali ya juu mpka kumaliza nafasi ya tano katika msimu wa mwaka 2010/11, wakajiwekea malengo katika msimu wa 2012/13 wamalize katika nafasi tatu za juu lakini matokeo yake wamemaliza nafasi ya sita ambayo imeonekana kuwaumiza wapenzi wengi wakiwemo viongozi.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
June 4, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment