Tuesday, June 4, 2013

Kesi ya Makamu wa Rais Kenya, William Ruto kusikilizwa Septemba.

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetangaza kuwa kesi zinazowakabili washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya, naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang zitasikilizwa mwezi Septemba.
Mahakama hiyo pia imependekeza baadhi ya vikao vya kesi hiyo kufanyika Tanzania au Kenya.
Ruto anakanusha kuwahi kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007 nchini Kenya, sawa na Rais Uhuru Kenyatta.
Mahakama ya ICC pia imesema kuwa ushahidi uliotolewa dhidi ya aliyekuwa rais wa Ivory Coast , Laurent Gbagbo, hautoshi kuhimili kesi dhidi ya mshukiwa.
Matangazo hayo mawili, yanakuja baada ya wiki kadhaa za shinikizo kutoka kwa nchi kadhaa za Afrika kuwa mahakama hiyo itupilie mbali kesi hizo dhidi ya Kenyatta na Naibu wake.
Mataifa ya Muungano wa Afrika yalisema kuwa mahakama ya ICC ina ubaguzi wa rangi kwa kuwa inawawajibisha viongozi wa Afrika pekee , madai ambayo yamekanushwa na kiongozi mkuu wa mashtaka Fatou Bensauda.
Daima Fatou Bensouda amekuwa akisisitiza kuwa washukiwa ghasia za Kenya lazima wawepo katika mahama hiyo wakti kesi zao zikisikilizwa.Lakini majaji wameamua kuwa haki huenda ikatendeka zaidi ikiwa wataruhusu kesi za washukiwa wawili hao kusikilizwa Kenya au Tanzania.
Upande wa utetezi pia huenda ukalazimika kutoa ombi hilo kwa niaba ya mshukiwa Uhuru Kenyatta.
Lakini pigo kubwa zaidi kwa kiongozi wa mashtaka ni ambavyo umeshughulikia ushahidi dhidi ya Laurent Gbagbo,kwani mahakama inasema hautoshi kuweza kuhimili kesi.
Mahakama inataka hilo kurekebishwa kabla ya kusikiliza tena kesi hiyo mwezi Novemba. Gbagbo amekaa ICC sasa kwa miaka miwili huku kesi yake ikiwa bado haijasikilizwa.
Moja ya sababu ya kuundwa kwa mahakama ya ICC ni kuonyesha kuwa hakuna ambaye anaweza kuhujumu sheria bila kuwajibishwa.
Kwa sasa jukumu kubwa la viongozi wa mashtaka ni kuonyesha ushahidi wa kutosha utakaoweza kuwashawishi majaji kuwa bwana Gbagbo ana kesi ya kujibu.
Kesi dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi Ujao.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment