Thursday, June 13, 2013

Langa Kileo, afariki jioni hii.


Wiki moja baada ya kuzikwa msanii maarufu wa kizazi kipya (bongo fleva) Albert Mangweha, leo jioni msanii mwingine aliyewika katika tasnia hiyo Langa Kileo ametangazwa kuaga dunia kutokana na maradhi.

Kwa mujibu wa kituo cha Radio Clouds FM, Langa ambaye aliwika na kikiundi cha Wakilisha amefariki leo jioni katika Hospitali ya rufaa Muhimbili jijini Dar es Salaam katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Taarifa hiyo haikuweka wazi msanii huyo alifariki kwa maradhi gani lakini kwa muda mrefu Langa aliweka wazi kuathiriwa na matumizi mabaya ya dawa za kulevya ambazo zilifanya kushusha kiwango chake kiusanii kutokana na kudhoofika afya.

Naye ofisa habari wa hospitali hiyo Eminiel Eligaesha, amethibitisha kifo cha msanii huyo kwa kusema, "Ni kweli amefariki saa 11 jioni leo, hilo ndilo ambalo naweza kusema kwa sasa ila saabu za kifo chalke na mambo mengine inabidi msubiri taarifa ya daktari."

Kidojembe ipo karibu na vituo vya habari ili kuweza kujua sababu za kifo cha msanii huyo ambaye atakumbukwa sana kutokana na kipaji cha hali ya juu katika muziki huo wa hiphop bongo.

Aidha, langa mtoto wa mfanyakazi wa Serikali aliibuka katika usanii mara baada ya kumaliza elimu ya kidato cha nne mwaka 2004, ambapo katika mwaka huohuo alikuwa miongoni mwa wasanii watatu Sara na Witness walioshinda Coca Cola Popstars wakaenda Afrika Kusini na kurudi ndipo wakaunda kikundi cha Wakilisha.

Baada ya mwaka mmoja waligawanyika kutokana na sababu za kimaslahi lakini tayari walikuwa na nyimbo mbili zilizokuwa kali moja ikiwa ni 'Unaniacha Hoi.' Baada ya hapo Langa alitoa ngoma kali iliyomtambulisha vema amabyo ni 'Matawi ya Juu' na nyingine nyingi alizoimba peke yake na alizoshirikishwa na wasanii wengine.

Baada ya kupata umaarufu mwanzoni mwa mwaka 2008 alijitumbukiza katika matumizi ya dawa za kulevya, lakini baada ya kuona hakuna faida aliamua kuweka wazi juu ya hali yake na kuchukia kutumia dawa hizo. Ambapo kwa wakati ho alikuwa msanii wa kwanza wa kizazi kipya Tanzania kutangaza kuwa mwathirika wa dawa za kulevya.

Kidojembe inaungana na ndugu wa familia pamoja na wasanii wote hasa kwa wiki mbili hizi ngumu kwa kupoteza wasanii wawili ambao wote wanahusishwa na matumizi ya dawa za kulevya. 

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali panapostahil.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment