Thursday, June 13, 2013

Wasomi waanza kutilia shaka ujio wa obama.


Dar es Salaam.  Ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama bado imeendelea kuwatia kiwewe Watanzania wakiwamo wasomi na wanasiasa.

Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba  jana alisisitiza kwamba Rais huyo anakuja nchini kuchunguza masuala ya madini hususan urani.

Lakini nao  wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamepata hofu  wakisema wana wasiwasi Tanzania itakachofaidika kwa ziara hiyo. Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Kitengo cha Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Sabatto Nyamsenda alisema hofu kubwa iliyopo inatokana na ubovu wa sera za Serikali katika masuala ya uwekezaji.

Nyamsenda aliongeza kuwa viongozi wa Serikali wamesharidhia uporaji wa rasilimali zake kupitia sera na mikataba mibovu isiyomnufaisha Mtanzania.

Profesa Robert Mabele kutoka kitengo cha uchumi chuoni hapo alisema pamoja na uhusiano ambayo Rais Kikwete amejitahidi kuujenga miongoni mwa nchi kubwa duniani, lakini hatuwezi kufaidika endapo hatutakuwa na sera nzuri za uwekezaji. Dk Jehovaness Aikaeli wa kitengo cha uchumi chuoni hapo alisema ujio wa rais huyo hautaweza kuleta mabadiliko yoyote kama inavyodhaniwa na Watanzania wengi.

Maoni hayo yanatolewa wakati juzi Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt alitaja sababu za Obama kuja Tanzania kwamba  ni kutokana na sifa nzuri za Tanzania. Sifa hizo zilizomvuta Rais Obama ni utawala bora, demokrasia  na mazingira bora ya uwekezaji yanayosabisha kukua kwa uchumi.

Balozi wa Marekani alisema Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani, utulivu kwa muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

‘‘Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za Watanzania katika kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji  na pia amevutiwa na ukuaji wa uchumi,’’ alisema Lenhardt.

No comments:

Post a Comment