Tuesday, June 25, 2013

Ulaya bado hawafurahii kombe la Dunia kuchezwa mabara mengine.

                                           Waandamanaji wakiwa barabarani kudai haki zao.

Vurugu zinazoendelea katika miji ya Brazil zimeonekana kupata mashiko sana katika vituo vya luninga na magazeti ya Ulaya kuliko michuano ya soka Kombe la Mabara inayoendelea katika nchi hiyo.

Lengo ni moja tu, kutaka kuidhihirishia dunia kuwa Brazil si mahali salama kwa michuano mikubwa ya soka hasa ikizingatiwa imebaki miezi michache kuanza michuano ya kombe la dunia mwezi Juni 2014.

Ni wazi ile kampeni iliyoanzishwa na Rais wa shirikisho la soka duniani (FIFA), Sepp Blatter kuhakikisha uandaaji wa fainali za kombe la dunia unasambaa mabara yote katika dunia, imepokelewa kwa shingo upande na nchi za Ulaya ambao kwa muda mrefu wametawala michuano hiyo.

Kitendo cha kulileta kombe la Dunia barani Afrika kimeonekana cha kipekee sana lakini kilimgharimu Sepp Blatter, mpaka kutaka kukosa kura za kukitetea kiti chake mwaka 2011, kama hiyo haitoshi katika utawala wake kwa mara ya kwanza michuano hiyo yenye hadhi ya kipekee duniani mwaka 2002 ilifanyika barani Asia katika nchi za Japan na Korea tangu 1930 ilipoanzishwa nchini Uruguay.

Wiki iliyopita katika jiji la Sao Paulo nchini Brazil waandamanaji walikusanyika katika ukumbi wa manispaa ya mji huo kwa lengo la kuishinikiza Serikali kushusha viwango vya nauli kwa usafiri wa umma ambavyo vimepanda kwa asilimia 7. Lakini hiyo ilikuwa ni sababu tu kwani baada ya waandamanaji kupata upinzani mkubwa kwa vikosi vya kutuliza ghasia siku iliyofuata vilizuka vikundi vipya vikiwa na madai mapya.

Wafanyakazi wa shirika la reli waligoma na kuzima mitambo wakilalamika hali ngumu ya maisha kutokana na tatizo la mfumuko wa bei kufikia asilimia 6.5, yakazuka malalamiko mengine kama ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha.

Meya wa Sao Paulo, Fernando Haddad amesema haoni kama madai ya waandamanaji hao yana msingi kwani tayari Serikali ilishatoa punguzo la kodi kwenye sekta ya usafiri wa umma, na atahakikisha hatozungumza na waandamanaji mpaka watakapoacha vurugu na kuharibu mali.

Wananchi wa Brazil wanapaswa kutambua kuwa kuandaa michuano mikubwa kama kombe la dunia hakuiletei tu nchi sifa bali uchumi unakua pamoja na kutangaza utamaduni kimataifa, vurugu zao ni faida kwa wengine wakitaka kujua wawaulize Libya baada ya kukosa nafasi ya kuandaa michuano ya CHAN 2011 kutokana na vurugu za kisiasa michuano ikapelekwa Afrika Kusini.

Blatter mzaliwa wa Uswissi aliingia madarakani Juni 1998 akichukua nafasi ya Joao Havelange kutoka Brazil ambaye alikuwa Rais wa FIFA tangu mwaka 1974. Blatter amebadili mchezo wa soka na kuufanya kuwa wa wote, mathalan Brazil kwa mara ya mwisho kuandaa kombe la dunia ni mwaka 1950 ambapo kwa wakati huo ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza nje ya Ulaya kuandaa michuano hiyo, baada ya miaka 30 yaani 1986 michuano hiyo ikarudi tena Marekani ya Kusini maandalizi yalifanyika Mexico.

Ndani ya miaka saba ya utawala wa Blatter michuano ikaenda bara la Asia kwa mara ya kwanza katika nchi za Japan na Korea kusini, baada ya miaka saba mingine michuano ikaja Afrika kwa mara ya kwanza katika nchi ya Afrika Kusini. Michuano itarudi tena Asia mwaka 2022 nchini Qatar, hakika hii kampeni inahitaji kuungwa mkono.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
26 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment