Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lina imani kuwa mazungumzo kati yake, Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
yatamaliza tatizo la kushikiliwa akaunti ya TFF kutokana na malipo ya kodi ya
mishahara ya makocha wa kigeni.
Rais
wa TFF, Leodegar Tenga alizungumza na waandishi wa habari jana juu ya uamuzi
wa TRA kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB kukata sh.
157,407,968 ikiwa ni malipo ya Kodi ya Mapato ya Mshahara wa Mfanyakazi
(P.A.Y.E) ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake.
Katika
mzozo huo wa muda mrefu, TFF imejitetea kuwa haiwezi kulipa kodi hiyo kwa
kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo mlipaji wa
mishahara ya makocha hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete
ya kulipia makocha wa michezo tofauti, ukiwemo mpira wa miguu.
“Hili
ni suala nyeti ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya pande
zote. Ninataka kuwahakikishia kuwa suala hili linazungumzwa na tayari
nimeshafanya mazungumzo na maofisa wa Wizara na tumekubaliana kukutana na
pande zote wakati wowote; iwe leo jioni au kesho.
“Ni
matumaini yangu kuwa suala hili litakwisha na jana nimetoka Kampala (Uganda
kwenye Kombe la Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na viongozi wa
Wizara na wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza suala hili.
“Nimezungumza
na wenzetu wa Serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Fedha zilizokamatwa
si zetu; ni fedha za klabu na zimetolewa na mdhamini ambaye tumekubaliana
namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa ajili ya kulipia kodi. Lakini
TRA wanazishikilia kwa sababu Premier League iko chini ya TFF,” amesema Rais
Tenga.
Tenga
amesema TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi na hivyo
wana haki ya kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, mwajiri ndiye
anayetakiwa kukata kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi.
“Hivyo
hatuwezi kuilaumu TRA kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini pia hatuna
uwezo huo wa kulipa fedha hizo kwa sababu, kwanza hatuna na pili sio sisi
tunaolipa mishahara ya hawa makocha,” amesisitiza Rais Tenga.
Akizungumzia
historia ya suala hilo, Tenga aliishukuru Serikali kwa msaada ambao imekuwa
ikiutoa katika mpira na kwamba ahadi ya Rais Kikwete ya kusaidia kulipa
makocha wa timu za taifa imeusogeza mpira wa miguu karibu na Serikali na
karibu na Rais.
“Rais
Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani (mwaka 2005) anajua kuwa kuna
tatizo kwenye mpira na akatoa ahadi ya kulipa walimu wa mpira. Ahadi hiyo
imefanya ukaribu uliopo sasa kati ya mpira na Serikali; kati ya mpira na Rais
sasa kuwa mkubwa. Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kwenye mpira, yaani
kulipa walimu.
“Sasa
sisi ni administrators wa hawa walimu. Tunachofanya ni kuandaa mikataba
ambayo ni standard duniani kote kwa mujibu wa taratibu za FIFA (Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu). Kwa kawaida makocha wa kigeni huwa
wanatayarishiwa mikataba ambayo ni tax free (isiyo na kodi). Baada ya kuingia
nao mikataba, huwa tunaipeleka wizarani ambao ndio wanawalipa makocha moja
kwa moja kwenye akaunti zao,” amesema Rais Tenga.
Katika
mkutano huo na waandishi, Rais Tenga pia aliipongeza timu ya taifa ya
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa kuanza vizuri mashindano ya Kombe la
Chalenji, akisema ushindi huo ni ishara nzuri hasa kutokana na ukweli kuwa
kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi na akataka Watanzania
waendelee kuiunga mkono.
Tenga
pia alisema kumekuwepo na malalamiko kuhusu makato ya mechi na kwamba suala
hilo ni la muda mrefu na kwamba TFF imepiga hatua kubwa tangu ilipoanza
kulishughulikia.
|
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment