Na Daniel Mjema
WIZI wa vitu mbalimbali kwenye magari madogo ya kifahari
unaofanywa na watu wasiojulikana wanaovunja vioo vya magari kwa kutumia
kemikali, umeanza kuutikisa mji wa Moshi.
Hata hivyo habari za uhakika zilizopatikana jana na
kuthibitishwa na polisi zilisema wengi wa waliobiwa kwa njia hiyo hawatoi
taarifa polisi japo matukio hayo yanaongezeka.
Watu wanaoendesha vitendo hivyo kwenye maegesho ya magari
wanadaiwa kumwaga kemikali kama mafuta ya nywele za wanawake aina ya Curl
ambayo hupasua kioo na kukiacha kama
chengachenga.
Kikundi hicho kinadaiwa kulenga zaidi vifaa vya thamani kama kompyuta mpakato(Laptop),Kamera, fedha taslimu, simu
za mikononi na pochi za wanawake ambazo kwa sehemu kubwa huwa na vito vya
thamani na fedha.
Mthamini wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Hugo Michael ni
mmoja wa waathirika wa tukio hilo
ambaye alisema, binafsi aliibiwa mfuko uliokuwa na Laptop, Kamera na nyaraka
mbalimbali za ofisi.
Alisema Jumatatu iliyopita aliegesha gari eneo la maegesho ya
hospitali ya Rufaa ya KCMC na kwenda kumuona mgonjwa lakini aliporejea alikuta
kioo cha gari yake kimepakwa mafuta na kusambaratika.
Mhandisi wa mradi mkubwa wa jengo la kibiashara la mfuko wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF) karibu na Halmashauri naye alikumbwa na tukio kama hilo na
kuibiwa Laptop na nyaraka mbalimbali.
Mbali na wizi huo ,eneo la Soko la Mbuyuni, nako kumeibuka wimbi
la wizi wa vitu mbalimbali kwenye magari yanayoegeshwa eneo hilo ambapo wezi hao hufungua milango na vioo
vya magari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema
matukio ya wizi wa kutumia kemikali bado hayajamfikia lakini ya wizi katika
soko la Mbuyuni wana taarifa nayo na wanaendelea na uchunguzi.
Alisema polisi wamefanikiwa kukamata watuhumiwa wachache
wanaodaiwa kuhusika na wizi huo lakini wanashindwa kuwafikisha mahakamani kwa
kukosa ushirikiano kutoka kwa wanaoibiwa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment