Wanahabari wakisikiliza kwa makini maelezo ya Mudhihiri katika ofisi za bodi ya korosho nchini.
Hafidh Kido
Bodi ya korosho Tanzania
imeamua kuzima maandamano ya wakulima wa korosho yaliyopangwa kufanyika leo
baada ya wakulima hao kulalamika kukaa na mazao hayo bila ya serikali kuyanunua
na hata walipojaribu kuyauza kwa njia wanazozijua wao walikamatwa.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo asubuhi makamu mwenyekiti wa bodi hiyo mbunge wa zamani wa jimbo la
Mchinga Mudhihiri Mudhihiri, amesema ingawa msimu wa ununuzi wa korosho
ulifunguliwa mwezi wa tisa mwaka huu lakini vyama vinavyohusika na ununuzi wa
zao hilo vilikosa mkopo kutoka katika mabenki hivyo kushindwa kukamilisha zoezi
hilo.
“Msimu wa ununuzi wa korosho
ulifunguliwa rasmi 20/09/2012 kwa vyama vya msingi kuanza kukusanya korosho kwa
wakulima, kwa kawaida vyama hivi hupata mkopo kutoka katika mabenki ili
kuwalipa malipo ya awali na baada ya kuziuza huwalipa malipo ya pili.
“lakini mwaka huu vyama
vimechelewa kupata mikopo hivyo kuchelewa kukusanya korosho za wakulima kwa
wakati muafaka, kuchelewa kuanza ununuzi wa korosho kumewaathiri sana wakulima hata sisi
tunafahamu,” alisema Mudhihiri.
Aidha mnamo mwezi wa kumi na
moja mwaka huu waziri wa kilimo, chakula na ushirika Christopher Chiza,
aliitisha kikao maalum mjini Dodoma
ili kujadili suala hili. Ambapo watu waliohudhuria kikao hicho ni bodi ya
korosho, bodi ya leseni ya maghala, wizara ya viwanda na biashara, benki kuu na
benki za CRDB, NMB, TIB pamoja na chama cha ushirika.
“Kikao kile kilijadili mambo
kadha ikiwemo mkanganyiko wa bei dira, madeni ya msimu wa 2011/2012 na kutafuta
suluhisho la matatizo yote, kulikuwa na mafanikio makubwa maana kikao kilifikia
maazimio yafuatayo:- bei dira ibaki Tsh 1,200 kwa kilo ya korosho daraja la
kwanza, na Tsh 960 kwa daraja la pili.
“Ili
kumpunguzia mkulima mzigo wa riba ya deni mabenki yatakopesha vyama vya msingi
malipo ya awali kwa riba ya asilimia 50 badala ya asilimia 70 msimu uliopita.
Tafsiri ya badiliko hili ni kuwa bei ya awali ya malipo kwa kilo ya korosho
daraja la kwanza itashuka kutoka Tsh 800 mpaka Tsh 600. manufaa yake ni kuwa hakutakuwa
na riba kwa malipo ya pili na yale ya
majaliwa,” aliainisha Mudhihiri.
Makamu mwenyekiti huyo wa
bodi ya korosho nchini alieleza kwa mwaka huu wanatarajia kununua tani 160 za
korosho kutoka kwa wakulima na kusisitiza kuwa zile korosho zilizokamatwa siku
kadhaa zilizopita zilikuwa zinakwenda kuuzwa bila ya utaratibu hivyo serikali
haiwezi kukubali kuendelea kupata hasara kama
waliyoipata msimu uliopita ambapo walipoteza kodi zaidi ya bilioni 100.
Wiki kadhaa zilizopita
wauzaji wa korosho kutoka wilaya ya Tandahimba mkoa wa Mtwara, baada ya kuona
korosho zao hazinunuliwi waliamua kujikusanya na kuzisafirisha kutoka
mashambani na kuenda kuzibangua Kibaha mkoa wa Pwani ambapo magari yao yalikamatwa maeneo ya
Vikindu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam yakiwa na tani 15 za korosho.
Akizungmzia sakata hilo mudhihiri alisema “Zile korosho tumeamua kuzikamata
kwasababu zinatakiwa kuuzwa kwa mfumo wa mnada na si kwa njia ya kiholela kama walivyotaka wao. Zikiuzwa kiholela tutakosa kodi, na
kutokana na kutofahamu tumezipima tumeona zimechanganywa daraja la kwanza na la
pili.
“Hata unyevu ni 12, hivyo
bado ni za hivi karibuni lakin tumeamua tutaziachia ikiwa tu watakubali kufuata
taratibu za kuziuza kwa kutumia mnada. Tuna mpango wa kuanzisha viwanda vya ndani
vya ubanguaji korosho ili tuache kupeleka korosho zetu India zikiwa ghafi.”
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
kidojembe@gmail.com
No comments:
Post a Comment