WEDNESDAY, NOVEMBER 7, 2012
Katika kipindi cha ziadi ya wiki tatu nchi imekuwa katika
matatizo makubwa ya upungufu wa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli hali
yenye athari kwa uchumi wa nchi na usumbufu na gharama za ziada kwa wananchi.
Katika kipindi hicho viongozi na watendaji wa
Wizara ya Nishati na Madini wakiwemo Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na
taasisi zilizochini ya Wizara hiyo hususan Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (EWURA) wamekuwa wakitoa taarifa zenye mkanganyiko kuhusu matatizo
yanayoendelea.
Hivyo, nasisitiza Waziri Mkuu kwa madaraka
yake ya ibara ya 51 ya katiba ya udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa
shughuli za siku hata siku wa kazi za Serikali na kiongozi wa Shughuli za
Serikali Bungeni badala ya kutoa tu kauli bungeni aagize Waziri wa Nishati na Madini
awasilishe hoja ya taarifa ya Serikali juu ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge
kuhusu mafuta na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali juu ya matatizo ya
mafuta yanayoendelea.
Uamuzi huu utaliwezesha bunge kutumia
vizuri mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ya kuishauri
na kuisimamia Serikali katika kipindi hiki ambacho hatma ya Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini haijulikani hata baada ya Spika kukabidhiwa ripoti ya “Kamati
ya Ngwilizi”.
Iwapo Serikali itawasilisha tu kauli bungeni
kwa mujibu wa kanuni ya 49 Bunge litafungwa na kanuni kwa kuwa kauli hizo za
mawaziri hazipaswi kujadiliwa wakati kuna masuala muhimu ambayo yanapaswa
kujadiliwa hata baada ya hatua zilizochukuliwa tarehe 02 Novemba, 2012 na Waziri wa
Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alipokutana na makampuni yanayohusika
na biashara ya mafuta na yenye maghala ya kuhifadhia mafuta nchini.
Serikali ieleze hatua
zilizochukuliwa za kuwawajibisha watendaji wa wizara, taasisi zake na makumpuni
yaliyohusika kusababisha hali hii kutokana na uzembe, udhaifu na uhujumu wenye
athari kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi na bunge lipitishe maazimio ya
hatua za ziada za kuchukua iwapo matatizo haya yatajirudia tena katika taifa
letu.
Bunge lijadili hatua iliyochukuliwa ya kuagiza asilimia hamsini
(50%) ya mafuta yaliyokuwa yanakwenda nje ya nchi (Transit fuel) yauzwe ndani
ya nchi iwapo ilitekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya nchi
kitaifa na kimataifa.
Bunge lipewe taarifa ya kina iwapo meli za Miss Marelina
iliyokuwa ikishusha mafuta (ikiwa na MT 22,039 za diseli na MT 14,925 za
Petroli) na Meli ya Eskden inayoendelea kushusha mafuta (yenye MT 32,000
za dizeli) kuhakikisha mafuta yake yanasambazwa kwa uwiano na kwa wakati
mikoani kutokana na upungufu uliopo hususan katika maeneo ya vijijini.
Serikali kupitia kwa Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari
(TPA) kueleza sababu za kuchelewa kujengwa kwa Boya kubwa la kupakulia mafuta
(SBM) toka mwaka 2011 na kueleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha kwamba boya
hilo linaanza kazi katika kipindi kisichozidi wiki moja kuanzia sasa kama jambo
la dharura.
Sababu za Serikali kutochukua hatua dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi
wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (Petroleum Importation Cordinator-PIC)
iliyokuwepo toka mwanzoni mwa mwaka ilipolalamikiwa na wadau na hatua
zinazochukuliwa kwa haraka kufanya marekebisho ya kanuni kukidhi mahitaji ya
Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja ikiwemo mfumo mpya wa uundaji wa bodi.
Serikali itoe maelezo ya hatua iliyofikiwa katika uanzishwaji wa
Mpango wa Hifadhi ya Akiba ya Mafuta ya Taifa (Strategic Petroleum Reserve –
SPR) ambao ungekuwa kinga ya nchi pale panapojitokeza upungufu katika uingizaji
wa mafuta au hujuma za mafuta kufichwa katika maeneo mbalimbali na
wafanyabiashara wasio waaminifu.
Serikali kupitia Bunge iombe radhi kwa wananchi kutokana
na athari zilizojitokeza kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana
na matatizo ya mafuta kujirudia tena.
Wakati huo huo, natoa mwito kwa
EWURA pamoja na kutangaza bei mpya elekezi ieleze hatua ambazo mamlaka hiyo
imechukua mpaka sasa katika kuwafutia Leseni wafanyabiashara wote ambao wana
leseni za kuagiza mafuta lakini hawafanyi kazi hiyo na kutaja orodha ya
makampuni hayo kwa umma.
Pia EWURA ieleze sababu za Serikali
kuzidiwa nguvu na wafanyabiashara ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya
Nishati na Maji (EWURA) inapotoa bei elekezi za kushuka huficha mafuta
kwa kisingizio cha kulalamikia kanuni ya kupanga bei safari hii wakitarajia
kupanda kwa bei jumatano ya kwanza ya mwezi tarehe 7 Novemba 2012.
Kutokana na hujuma hizo tatizo la upungufu
wa mafuta nchini limeongezeka kutokana na udhaifu kwa kuzingatia kuwa taarifa
za ndani ya maghala makubwa ya kuhifadhia mafuta zinadhihirisha
kwamba pamoja za uzembe wa uchelewaji uliotokea nchi isingekuwa katika matatizo
makubwa ya mafuta ikiwa hali hiyo ingedhibitiwa kwa Serikali kusimamia
utawala wa sheria kulinda maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Izingatiwe kwamba EWURA ilitoa taarifa
katika vyombo mbalimbali vya habari tarehe 5 Novemba 2012 kukanusha kuhusu
mkanganyiko uliopo Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekiri bungeni kuwepo kwa
kutofautiana kwa kauli baada ya kutakiwa kutoa majibu na Spika kufuatia
muongozo nilliomba wa kutaka Serikali itoe kauli bungeni.
Nilieleza kwamba pamoja na kauli ya Naibu
Waziri Simbachawene tarehe 2 Novemba 2012 bungeni kuwa matatizo yamemalizika
hali bado ni tete hususan mikoani hatua ambayo ilimfanya Spika amtake Waziri
Mkuu atoe majibu ambaye aliahidi kwamba Serikali itatoa kauli kabla ya kuisha
kwa shughuli za Bunge katika mkutano unaoendelea. Hivyo, nitaendelea kuisimamia
Serikali kuchukua hatua zinazostahili kwa kadiri matatizo haya yatakavyoendelea.
Imetolewa tarehe 6 Novemba 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini
No comments:
Post a Comment