Na Hafidh kido
Tofauti na matarajio ya wengi
kuwa mkuu mpya wa wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu angeanza uongozi wake kwa
kutazamia mambo makubwa kama kukuza uchumi ama
usafi wa mji lakini nguvu zake zote amezilekeza katika kampeni ya ‘niache
nisome’.
Raia Mwema iliamua kufanya
ziara wilayani humo ili kuangalia mapambano hayo na mwandishi wetu hakufanya
papara ya kukutana na kiongozi yeyote bali aliingia mitaani na kusikiliza maoni
ya wakazi juu ya utendaji wa mkuu mpya wa wilaya yao inayotajika kuwa nyuma
kimaendeleo katika wilaya za mkoa wa Tanga.
Ilichobaini Raia Mwema ni
kuwa ndugu Muhingo hataki mchezo katika suala la mtoto wa kike, na wakazi wa
Handeni hasa wale wanaopenda utamaduni huo wa kuoa vitoto vya shule inawawia
vigumu sana
kumpa ushirikiano. Katika vijiwe vya waendesha bodaboda, wauza kahawa, sokoni
na vijiwe vya wacheza bao sehemu zote hizo wanazungumza kampeni ya niache
nisome.
“Huyu mkuu wa wilaya ni mkali
kweli, yaani hataki mchezo watoto wetu wenyewe anatupangia muda wa kuwaozesha.
Hajui kama maisha ni magumu na hatuwezi kuwasomesha mabinti zetu au yeye aje
atusaidie kulipa ada,” hayo ni baadhi ya mzungumzo ambapo mwandishi wetu
alikwenda kushiriki kunywa kahawa bila ya kujitambulisha.
Niache nisome ni nini.
Hii ni kampeni iliyoanzishwa
na ndugu Muhingo ili kumwokoa mwanafunzi wa kike kwa kumpa ujasiri wa kuwa na
sauti ya kishujaa kumjibu mzazi ana mtu anaemtaka kimapenzi kwa kumwambia
‘niache nisome’. Lengo ni kumfanya ajitetee mwenyewe ili afikie malengo
aliyojiwekea.
“Mbali ya taaluma ya uandishi
wa habari lakini niliwahi kuwa mwalimu wakati fulani, nilipoteuliwa kuwa mkuu
wa wilaya hii na Rais Kikwete nilikuta chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA
wakifanya utafiti juu ya hali ya elimu wilayani humu na wakagundua watoto wengi
wa kike wanashindwa kumaliza masomo yao kutokana na mimba na ndoa za mapema,”
anaanza kueleza Muhingo.
Wakati mwandishi wetu
akifanya mazungumzo haya hafla simu ya mkuu wa wilaya ikaita, alikuwa ni mzazi
akitoa taarifa juu ya mwalimu mkuu anaetembea na wanafunzi. Baada ya kukata
simu akapokea ujumbe mfupi kuna mwanafunzi mwengine anaolewa katika kata ya
Kabuku.
Muhingo, akamgeukia mwandishi
na kumwambia, “Nadhani habari yako inazidi kunoga maana umejionea hali halisi
namna tatizo hili lilivyokuwa kubwa na watu wa Handeni tayari wameshakuwa
tayari kutoa ushirikiano.”
Akaendelea na maelezo “Nilipoteuliwa
katikati ya mwaka huu kitu cha kwanza nilipitia taarifa za wakuu wenzangu
waliopita, sifa kuu ya wilaya hii ni maendeleo duni hasa katika nyanja ya elimu.
“Nikakuta mwaka 2011
wanafunzi wapatao 900 waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali nyingi
zikiwemo kuolewa na ujauzito. Niliumia sana,
kitu cha kwanza baada ya kuingia ofisini nilijifanya mtu wa kawaida nikaanza
kukaa vijiwe vya kahawa, nikaenda kukaa katika foleni za hospitali kusikiliza
matatizo ya wananchi na hata sokoni nilipitapita mpaka walipoanza kunijua
nikaamua kuacha lakini nilishapata taarifa nyingi sana kuhusiana na wilaya hii,” Muhingo.
Malengo ya kampeni
Niache nisome, ni kampeni
aliyoinzasha akishirikiana na mkewe ambae anasoma shahada ya uzamivu katika
mambo ya jamii kwenye chuo kimoja nchini China. Ambapo waliwashirikisha
wanafunzi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam,
wakafanya utafiti na kukusanya taarifa za kutosha juu ya tatizo hilo.
Utafiti wao ulibaini kuwa
wazazi nao huumia wanapoona binti yao
amepata ujauzito akiwa shule, lakini kwa kiasi kikubwa binti hubaki peke yake
pale anapozuiliwa kisheria kuendelea na masomo.
Awali kabla ya kukutana na
mkuu wa wilaya Raia Mwema lilifika ofisi ya afisa maendeleo ya jamii wilayani
humo ambae amehusika kwa kiasi kikubwa kusimamia kampeni hiyo ya niache nisome.
Ndugu Julius Mhando, afisa
maendeleo ya jamii alianza kuelezea tatizo la utoro na mimba kwa watoto wa kike
kutoka kwa wazazi ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia tatizo hilo.
“Unajua miaka ishirini
iliyopita handeni kulikuwa na shule
mbili tu za sekondari, hivyo utaona ni kwa kiasi gani kizazi cha kuanzia
mwishoni mwa miaka ya thamanini hawakusoma. Na hawa ndiwo wazazi wa mabinti
tunaoshughulika nao sasa.
“Wazazi hawajui umuhimu wa
elimu, na Handeni asilimia 75 wanaishi katika umasikini uliotopea, hivyo zipo
taarifa nyingi zinakuja ofisini kwetu wazazi wanawaficha watoto wao waliofaulu
wasiende sekondari kwa kuwa hawana uwezo wa kuwasomesha. Unadhani mtu huyo
binti yake akimaliza darasa la saba akija mtu anataka kuoa atakataa, au binti
awe kidato cha pili ama tatu na anasoma katika mazingira magumu mzazi atakataa
vipi posa ya binti huyo ikiwa binafsi hawezi kumsomesha wala kumuhudumia na
isitoshe mwenyewe hajui umuhimu wa elimu kwani hakusoma,” alieleza kwa uchungu
Mhando.
Aidha Mhando alifafanua kuwa
sababu kubwa za mabinti kupata ujauzito wakiwa shule ni kutojitambua wala
kutojithamini kama msichana, tama isiyolingana
na uwezo wao pamoja na baadhi ya mabinti kujipa majukumu ya wazazi kwa kuwalea
wadogo zao kwani wazazi wana hali mbaya kimaisha.
“Takwimu za idara yangu ya
maendeleo ya jamii kwa wilaya hii ya Handeni inasema kwa mwaka 2012 mpaka
kufikia mwezi huu wa kumi wanafunzi wa shule ya msingi walioacha shule
kwasababu mbalimbali nyingi ikiwemo ujauzito na kuolewa ni kama ifuatavyo; darasa
la nne 3%, darasa la tano 6%, darasa la sita 39%, wakati darasa la saba ni
52%,” alifafanua.
Kwa upande wa idara ya elimu
wilayani humo ofisi ya afisa elimu ya sekondari imempokea mkuu wa wilaya mpya
kama mkombozi na msaidizi mwema kwa tatizo hilo la utoro shuleni hasa kwa watoto wa
kike.
Afisa taaluma kwa shule za
sekondari wilayani humo Basil Mrutu, alizungumza kwa niaba ya afisa elimu na
kueleza kuwa tatizo kubwa wanalokumbana nalo kwa upande wa sekondari ni idadi
kubwa ya wanafunzi wanaofaulu kutoka shule za msingi kushindwa kuripoti kwa
kidato cha kwanza.
“Kwa sasa wilaya kwa
sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne ina wanafunzi wapatao 13688, kwa
mwaka huu ufaulu kutoka darasa la saba ilikuwa ni asilimia 73, lakini kutoka
januari mpaka octoba wanafunzi 241 hawajaripoti wasichana 139 na wavulana 102,
sababu kubwa ikiwa ni hali duni ya maisha.
“Kwa upande wa mamba mwaka
huu tu tuna taarifa za mamba zipatazo 23. tunamshukuru sana mkuu wa wilaya
tangu aanze kampeni hii miezi miwili iliyopita tatizo linaonekana kupungua
lakini itachukua mud asana kuisha kabisa maana wakazi wa Handeni wanaona ni
kama utamaduni wao kuozesha watoto wakiwa na umri mdogo nadhani ni kutokana na
kushindwa kuwahudumia kimaisha,” alieleza Mrutu.
Kwa upande wake Mrutu nae
aliungana mkono na afisa maendeleo ya jamii wilayani humo kuhusu tatizo la
wazazi kutosoma kutokana na uhaba wa shule miaka ya nyuma.
“Ni kweli wilaya hii ilikuwa
nyuma sana kielimu kwasababu ilikuwa na idadi
ndogo sana ya
shule za msingi na sekondari, mathalan kabla ya mwaka 2005 wilaya ilikuwa na
shule mbili tu za sekondari lakini hivi tunavyozungumza wilaya ina sule 30 za
serikali na binafsi,” alizungumza kwa sauti ya ushindi Mrutu.
Alipozungumzia tatizo la
ujauzito Mrutu alisema “Mara nyingi wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shule
ukichunguza maendeleo yao
ni mabaya hata kitaaluma,nah ii inasababishwa na malezi mabaya waliyoyapata
kutoka ngazi ya familia.
“Utakuta mtu aliempa mimba ni
jirani ama ndugu wa karibu hivyo hata wazazi huwakingia kifua na kutaka tatizo
limalizwe kifamilia mara nyingi tulikuwa tunaishia kuwafukuza shule halafu
basi. Lakini tunashukuru mkuu wa wilaya wa sasa hataki mchezo anampeleka polisi
kila kijana aliehusika na ujauzito wa mwanafunzi.
“Kampeni hii lazima uingwe
mkono na wazazi wa Handeni kwani inakata minyororo ya ujinga, elimu ndiyo
mzunguko pekee wa kuondoa umaskini, watoto wa kike wanatakiwa kupewa kipaumbele
katika elimu kuliko wa kiume. Niache nisome, itamfanya motto wa kike ajitambue
na kuhimili kupambana na mazingira hatarishi,” alisisitiza afisa taaluma huyo
wa wilaya.
Raia Mwema halikuishia hapo
lilikwenda kuonana na mkuu wa operesheni ya kukamata watu wanaohusishwa kuoa
ama kuwapa ujauzito wanafunzi, huyu ni mkuu wa upepelezi wa jeshi la polisi
wilaya ya Handeni ASP Juma Jumanne.
“Nimekuja handeni miezi
michache iliyopita hazidi miwili kwa utafiti wangu mdogo nimegundua wilaya hii
haina uhalifu mkubwa bali ni udokozi mdogomdogo, kazi kubwa ninayoifanya ni
kushirikiana na mkuu mpya wa wilaya ndugu muhingo kuhakikisha watoto wa kike
wanapata haki ya elimu bila bughudha,” alianza kumuelezea mwandishi.
ASP Jumanne alisema kuwa
kampeni hii ya niache nisome haijawahi kufanyika katika historia ya wilaya ile,
kwa maana katika taarifa ya ofisi yake ya upepelezi wala ofisini kwa bosi wake
mkuu wa polisi wa wilaya OCD, hajaona kesi iliyoonyesha mtu au watu walikamatwa
kwasababu ya kumpa mamba mwanafunzi ama kumuoa hali mambo hayo yalikuwa
yakifanyika tena kwa kiwango cha juu.
“Tatizo ni kubwa sana kuliko unavyofikiri bwana mdogo, katika jeshi la
polisi nimetembea wilaya nyingi sana lakini
sijaona wilaya inayoongoza kwa mambo haya kama
handeni. Haiwezekani kwa wiki tunapokea kesi sita mpaka saba (6-7) maana yake
kwa siku wastani wa kesi moja ya ujauzito ama ndoa, huwezi kuamini tangu nianze
kusimamia kesi hizi mpaka sasa kuna kesi 60 hapa kituoni zinazongoja kuenda
mahakamani.
“Na mahakamani kuna kesi 20
zinazongoja hukumu, hivyo kufanya kesi 80, ndani ya miezi mitatu. Mbali ya zile
ambazo hatujazikamata, unadhani tatizo hili ni kubwa kiasi gani,” alihoji ASP
Jumanne.
Hata hivyo jeshi la polisi
limelalamika changamoto wanazokutana nazo katika zoezi hilo kiasi kulifanya kuwa gumu kuanzia
utekelezaji mpaka kusimama mahakamani.
Mathalan, wameeleza kuwa
kitengo cha upelelezi kina askari 13 tu wilaya nzima, ni idadi ndogo kuliko
wilaya yoyote nchini, kadhalika wilaya nzima ina gari moja tu la polisi
ukiachia gari ya OCD, na vifaa vingine vya kiintelijensia.
“Wilaya ina uhaba wa askari
wa upelelezi, vifaa ikiwemo silaha na gari
tena hasa mafuta ya gari. Maana ingawa gari tunayo moja wilaya nzima lakini
ukosefu wa mafuta ya kutosha nalo ni tatizo kubwa maana kampeni hii inahitaji
tuwepo eneo la tukio mara tu tunapopigiwa simu. Sasa mathalan kwa siku
tukipokea simu tano za mabinti wanaoolewa ukichanganya na uhalifu mwingine wa
kila siku mafuta tutapata wapi,” alihoji ASP Jumanne.
Changamoto nyingine
wanayokumbana nayo katika operesheni hiyo ya kukamata watu wanaowapa ujauzito
watoto wa shule ni sheria inayoonyesha kuwakingia kifua ‘mabazazi’ hao. Maana
kwa mujibu wa sheria ya nchi kifungu cha 133 na 134, vinasema wai kuwa motto ni
mwenye miaka 16, hivyo mtu yeyote mwenye umri unaozidi miaka hiyo akiolewa ama
kushiriki mapenzi kwa ridhaa yake basi hakuna kesi hata akipata mamba.
Lakini wakati huohuo kwa
kidato cha pili, tatu na nne wapo mabinti ambao wana umri wa mika 19 mpaka 20,
maana yake wakipata ujauzito watu waliowapa hawatakiwi kupelekwa mahakamani
maana sheria ya nchi inasema huyo si motto na ikiwa hakushurutishwa bali
ameridhia tendo hilo
hakuna kesi ya kujibu.
Majibu ya mkuu wa wilaya
Baada ya mwandishi wetu
kuzunuka kote huko na kupata kilichojiri aliamua kurudi ofisini kwa mkuu wa
wilaya na kumpa mrejesho wa watendaji wake wanavyopambana katika kumsaidia
kuhakikisha mabinti wanapata haki yao
ya elimu.
Kuhusiana na haba wa mabweni
kwa wasichana Muhingo alisema uhaba wa mabweni si tatizo, maana kunaweza kukawepo
mabweni na wanafunzi wakaambiwa wakae bure, lakini hakuna maji wala chakula na
hili ndilo linalowafanya wakahangaika.
Hivyo ofisi yake kwa
kushirikiana na baadhi ya mashirika ya kijamii wameamua kuhakikisha wanachimba
visima katika kila shule ili kuwa na uhakika wa maji. Baada ya hapo wilaya
itaanzisha utaratibu wa kuwa na mashamba ya shule, ambapo kwa kuanzia wamepata
matrekta saba (7), ambayo watayasambaza katika shule zitakazokuwa tayari
kutenga ekari za kutosha kuweza kulima.
“Hili la kurudisha kilimo
mashuleni ni wazo ambalo wanafunzi wenyewe wamelipokea vizuri, maana tayari
tumeshazungumza na wakuu wa shule na wapo waliokubali kutenga ekari za kutosha
kuweza kulima mahindi na mbogamboga mazao yatakayotumika kwa chakula cha shule.
Pia wanafunzi watakaokuwa tayari watafundishwa kuendesha matrekta na wengi
wameonekana kulifurahia hili.
“Haya matrekta saba
tutayasambaza katika tarafa zote saba kila tarafa trekta moja, na huko
yatatembea katika mashule na kulima kwa ada ndogo ya mafuta ya kuendeshea trekta
na kumlipa dereva ama msimamizi, kimsingi tunataka kuwajengea uwezo wa
kujitegemea wanafunzi wote wa kike na wa kume,” Muhingo.
Kuhusu sheria kusema motto
anaishia miaka 16, Muhingo aliitaka serikali kurekebisha hiyo sheria maana
inawapa mwanya watu wabaya kuwaharibu wanafunzi. Na akasisitiza mtoto ni mtoto
tu madhali anasoma, akishamaliza ama akifika chuo kikuu hapo watajuana wenyewe.
“Hali ni mbaya sana Handeni katika vita
hii, najua huko mitaani wananichukia lakini wengi wa wanaonichukia ni wale
wabaya lakini nikwambie ukweli wengi wameshaanza kukubali kutoa ushirikiano.
Awali masheikh tuliwakuta wanaozesha tukasema na wao tukiwafunga haitosaidia
bali niliwaita baadhi yao
na wenyeviti wa vijiji nimezungumza nao na sasa wananipa ushirikiano wa kutosha.
“Kwa upande wa jeshi la
polisi kuwa na uhaba wa vitendea kazi ni kweli, nililiona hilo na tayari nimeshazungumza na IGP Said
Mwema, ila sitaki kuwaambia mpaka huo msaada utakapokuja. Maana kiukweli
Handeni ilisahauliwa, hata idara ya maendeleo ya jamii hawana gari hata moja
safari yao ya
kwanza kuenda vijijini walitumia gari yangu ni hatari kweli,” alieleza.
Kampeni hii ya ‘niache
nisome’ imevutia watu wengi hata mkuu wa mkoa wa Tanga Chiku Galawa, ameipenda
na kuamua Handeni iwe ni wilaya mfano (pilot area) ili kampeni ikionyesha
mafanikio iwe ni ya Mkoa na ikiwezekana nchi nchima.
Kwa kuthibitisha hilo Mkuu huyo wa mkoa
atashiriki wiki ya elimu itakayofanyika wilayani humo hivi karibuni ambapo
itakuwa ndiyo ya kwanza kufanyika tangu wilaya hiyo ianzishwe.
Hafidh kido
Handeni Tanga
No comments:
Post a Comment