Na Mwandishi Wetu
Serikali imetangaza vita na waganga wa
kienyeji waliobandika mabango sehemu mbalimbali za nchi na watu wengine kuwa
wanatibu ugonjwa wa Ukimwi.
Akizumgumza katika
mkutano wa Tacaids uliofanyika jijini Dar
es Salaam jana na kuhudhuriwa na wadau
mbalimbali wa mashirika ya dini, taasisi binafsi na watu wanaoishi na virusi
vya Ukimwi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Paniel Lyimo, alisema mpaka
sasa hakuna dawa ya ugonjwa huo.
Alisema dawa ikipatikana itatangazwa na
serikali na kwamba wanajitangazia kufanya kazi hiyo ni kinyume cha taratibu na
wanastahili kushughulikiwa.
Alisema sehemu kubwa ya Watanzania
hawajaathirika na kushauri wajikinge na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi
(VVU).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza
la Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (Nacopha), Vitalisi Makayula, alisema
tatizo la dawa feki za Ukimwi ni njama ya watu wanaotaka kujipatia fedha lakini
kisayansi tiba ya ugonjwa huo haijapatikana.
Alisema zaidi ya aina 60 ya dawa zilizopo ni
za kupunguza makali ya Ukimwi na wataalamu wanaendelea na utafiti.
Aliongeza kuwa dawa hizo feki zinapotosha
jamii na pia serikali hupata hasara kwani hutumia gharama kubwa kwa ajili ya
kununua dawa lakini watumiaji hukiuka kwa madai kuwa dawa ya Ukimwi
imepatikana.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tacaids, Dk. Fatma
Mrisho alisema yapo makundi yanayopata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi
kwa kasi na kushauri kujikinga zaidi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment