· Mkutano wa Kumi na Saba wa Baraza la Mawaziri wa Sekta za Afrika Mashariki na Mipango wamalizika kwa mafanikio;
· Mfumo wa Majadiliano baina Jumuiya, Sekta binafsi na Wadau wengine waidhinishwa;
· Itifaki ya Utawala Bora ya Afrika Mashariki kusubiri kukamilika kwa utekelezaji wa hatua za awali za mtangamano;
Mkutano wa Kumi na Saba wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki na Mipango umekamilika jijini Kampala tarehe 9/11/2012; ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt Abdulla Juma Sadalla (MB).
Katika mkutano wa siku tano, Tanzania ilifanikiwa kusimamia maslahi ya Nchi na Jumuiya kwa kukamilisha mfumo bora wa majadiliano baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi na Asasi za kiraia.
Mfumo huu utawezesha wadau hao kutoa michango yao katika masuala mbalimbali ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kukamilika kwa mfumo huo kunadhihirisha dhamira ya Nchi Wanachama ya kushirikisha wadau mbalimbali katika mtangamano wa Afrika Mashariki ili kuwa na mtangamano shirikishi na wenye maslahi kwa wote.
Aidha, imeelekeza kuwa, majadiliano kuhusu Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaongozwe na utekelezaji wa hatua za awali za mtangamano. Kwa kuzingatia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa hatua za awali za Mtangamano wa Afrika Mashariki yaani Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, ni vyema jitihada zakaelekezwa katika kufanikisha hatua hizo ili Wananchi waanze kunufaika na fursa zitokanazo na hatua hizo za awali na hivyo kuwapa shauku ya kuendelea na hatua zinazofuatia.
Masuala ya Utawala Bora yanahitaji uwiano wa mifumo ya utawala na kijamii, na kwa kuzingatia kuwa mifumo ya Nchi Mwanachama ya Utawala Bora inatofautiana; ikiwemo mihula ya Urais na Ukomo wa Urais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ni vyema kwa sasa, kila Nchi Mwanachama ikatekeleza masuala ya Utawala Bora kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi zao.
Aidha, Mkutano huo ulikubaliana kuhusu uzinduzi rasmi wa ofisi mpya za Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha Tanzania utakaofanyika mwezi Novemba, 2012 na Barabara ya Arusha – Namanga – Athi River kama sehemu ya mkutano wa kilele wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Novemba, 2012. Mambo mengine yaliyojadiliwa ni majadiliano ya Eneo Huru la Biashara la Utatu litakalojumuisha nchi 30 za Afrika, pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa hatua za awali za mtangamano.
Imetolewa na:-
KATIBU MKUU
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
No comments:
Post a Comment