Friday, November 16, 2012

Anaemshauri Mwenyekiti wa CCM ni msomi wa hali ya juu..


Philip Mangula

Hapa Mangula akimwaga ushauri kwa makatibu wakuu wa CCM waliopita Yusuph Makamba na Wilson Mukama.


Ingawa kwa sasa vyama vya upinzani vimeanza kupata wafuasi wengi lakini bado chama cha mapinduzi CCM kina watu wengi sana wanaokifuatilia kwa karibu kila wanachofanya.

Ambae anasema CCM imenilea sidhani anapotoka ama kusema maneno yasiyo na maana, hakika wanasiasa wengi kama si wote kwa wakati mmoja ama mwingine waliwahi kuwa wanachama wa CCM ama familia yao ina wafuasi wa chama hicho.

Na ndiyo maana kila kikao cha mkutano mkuu kinapokutana macho na masikio ya watanzania wengi huwa mjini Dodoma. Unaweza kusema hufuatilii, lakini mara nyingine unaweza kujikuta unafuatilia ili ukosoe; bila kutarajia unajikuta umo kundini.

Kitu kilichotarajiwa katika mkutano wa mwaka huu ni kuona wabaya wa mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete ndani ya chama wanamdhalilisha kwa kumpa kura ya hapana ama kwa kisiasa kura za maruhani ili adhalilike. Kwa kawaida mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa hana mpinzani, hivyo hupigiwa kura ya ndiyo ama hapana. Ingawa katiba ya chama haikatazi mtu kujitokeza kugombea nafasi hiyo lakini kiutaratibu wanaamua kumpa heshima mwenyekiti ambae mara nyingi ndie anakuwa Rais wa nchi.

Lakini kutokana na ‘umafia’ ama kuwatanguliza sana watu wa usalama katika shughuli zake mwenyekiti alihakikisha suala hilo halipati nafasi. Hawezi kudhalilika mbele ya wanachama zaidi ya 2000. Hivyo wakati wa upigaji kura ilibidi utaratibu ubadilishwe, badala ya wajumbe wote 2397 kupiga kura katika kapu moja ilibidi wajumbe wapige kura kwa mikoa. Yaani kila mkoa upige kura halafu zikusanywe kwa kuhesabiwa.

Ujanja huu ungemwezesha mwenyekiti kujua ni mkoa gani umempigia kura za maruhani. Na mkoa uliokuwa ukitajwatajwa sana kuhusika na hujuma hizo ni Arusha na Tabora wanapotoka waziri mkuu wa zamani Edward Ngoyai Lowasa na mbunge wa zamani wa Igunga Rostam Aziz anaewakilishwa na kada Hussein Bashe. Ambapo katika uchaguzi wa NEC ngazi ya mikoa kambi zao zilitajwa kufanya vizuri hivyo wakaamini hata katika mkutano mkuu wataendeleza ubabe unaoongozwa na mikakati ya Bashe kutoka Tabora.

Zipo taarifa zilizosambaa kuwa Bashe anaeongoza kampeni za kumsafisha Lowasa ili awe na njia rahisi kugombea urais mwaka 2015, alihusika kwa asilimia kubwa kutaka kumuangusha waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Benard Membe ambae alikuwa akigombea nafasi kumi za halmashauri kuu ya chama hicho. Mpaka hali ilipokuwa mbaya ilibidi mwenyekiti Kikwete aiagize familia yake kuingilia kati mchezo huo mchafu ndipo mke wa Rais mama Salma na mwanawe Ridhiwani walipoamua kumkingia kifua na kupita kwa wajumbe wote usiku kumsafishia njia Membe ambae hatimae alishinda kwa ushindi finyu ingawa alifanikiwa kuingia katika nafasi kumi.

‘Umafia’ wa pili uliofanywa na mwenyekiti ni kubadili tarehe ya uchaguzi, uchaguzi ulifanyika jumapili iliyopita tarehe 11 mwezi huu siku mbili nyuma ya tarehe iliyopangwa. Hili liliwaduwaza wapinzani wa mwenyekiti kwani hawakupata muda wa kutosha kujipanga kufanya hujuma zao.

Zengwe jingine lililozungumzwa sana katika mkutano ni uteuzi wa makamu mwenyekiti bara mzee Philip Mangula, na hili ndilo lililonifanya kuandika makala haya. Mzee huyu aliwahi kuwa katibu mkuu wa CCM kipindi cha Rais Mkapa ambapo alipokelewa na mzee mwenzie Yusuph Makamba, kabla ya kuja Wilson Mukama.

Mzee Mangula alipita kwa asilimia 100 kama alivyopita makamu mwenyekiti Zanzibar Dk Shein kwa asilimia hizohizo ingawa wapinzani wa Kikwete walifanikiwa kutia doa ushindi wake kwa kumnyima kura mbili. Hivyo tofauti na wasaidizi wake yeye alishinda kwa asilimia 99.92.

Tatizo wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wanahabari wengi waliokuwa mjini Dodoma walimzungumzia Mzee Mangula kama silaha iliyokwishatumika. Kwa sasa haina kazi tena maana CCM ya wakati huu si ile ya wakati wake.

Binafsi napingana na kauli hizo, CCM ya sasa inahitaji sana watu namna ya Mangula. Hakuna haja kukumbatia watu aina ya Stephen Wassira ambae anaonekana kukubalika sana na wajumbe maana katika nafasi kumi za juu alipata nafasi ya kwanza kwa kura nyingi, akafuatia Mwigulu Nchemba wote ni wapayukaji.

Sidhani wanaccm wametosheka na busara za wazee aina ya Mangula, kuwa hawataki tena watu wenye busra badala yake wapate watu wanaozungumza hovyo na kujinasibu wao ni ‘mwarobaini’ wa wapinzani. Hilo linanipa wakati mgumu sana kulielewa na kuliafiki. Ni imani ya kipuuzi sana.

Ikumbukwe mzee Mangula si tu ni mwanasiasa mkongwe lakini alipata kuwa mwalimu wa siasa katika chuo cha kigamboni. Wanasiasa wengi hasa wa CCM walipata kwa wakati mmoja ama mwingine kufunzwa siasa na nguli huyu. Hivyo kwa mawazo yangu CCM imemleta nguli huyu katika nafasi muafaka kwa wakati muafaka.

Wapo waliosema hatoweza kusikilizana ama kuendana na baadhi ya wanachama aina ya Nape Nnauye ambae ana sifa ya kupayuka, ama kulumbana na wafuasi wa upinzani wanaozungumza maneno ya hovyo kutokana na siasa za ushindani zilizozuka nchini.

Jibu ni rahisi, kwa siasa za Tanzania kubadilika zikawa za ushindani wa hovyo haimaanishi kila mwanasiasa anaetaka kufanikiwa basi nae awe wa hovyo. Unaweza kuweka busara penye ujinga na upuuzi bado ukashinda. Unataka kunambia Mwalimu Nyerere leo angekuwa hai basi nae angetumia maneno ya kukashifiana na siasa za majukwaani ili kuirudisha CCM mahala pake? Kamwe…

Nina imani nafasi nne za juu zina watu makini na wenye busara watakaokiongoza chama kuelekea mahala pazuri na kuachana na siasa za matusi ambazo hazina maana yoyote zaidi ya kupoteza lengo la upinzani. Kikwete ni mtu makini na asiependa kukurupuka, makamu visiwani Dk Shein ni mkimya lakini mtendaji asiependa kusifiwa, makamu bara Mangula, ni mwanasiasa mkongwe alierithi mikoba ya Mwalimu Nyerere atakaekisaidia chama kwa mawazo ya kizalendo na ujasiri. Katibu mkuu abdulrahman Kinana, ni mchapakazi, mzalendo na hapendi majungu.

Kwa safu hiyo sioni CCM ikiyumbishwa na chama chochote cha upinzani achilia mbali baadhi ya wana CCM ambao wanapanga kukihujumu chama kwa kuunda makundi ili kujisafishia njia ya kuteuliwa kugombea urais uchaguzi ujao.

Kwa leo sina mengi ila turidhike kuwa mshauri wa mwenyekiti Kikwete anahitaji pongezi za hali ya juu kwa namna alivyoweza kuwadhibiti wasaliti wa chama ambao wanaumiza vichwa kuhakikisha wanamkomoa ili aonekane hafai katika chama na wananchi.

Maana kwa sasa CCM wapinzani wake si Chadema na CUF tu bali hata makundi ndani ya chama ni wapinzani wakubwa wanaokidumaza chama na kushindwa kusonga mbele.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
15/11/2012

No comments:

Post a Comment