Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa
Zanzibar; Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara; Mwenyekiti
Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa; Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu; Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu; Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama; Ndugu Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM; Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini; Waheshimiwa Mabalozi, Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
2
Kama ilivyo
ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa
kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma , siku ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa
Nane wa Chama cha Mapinduzi. Ndugu Wajumbe; Karibuni Dodoma. Karibuni
Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika
salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru
wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma ,
wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa
ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo
Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu. Ndugu Wajumbe; Napenda kuchukua nafasi
hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya
Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson
Mukama na Kamati zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni na
asanteni sana .
Ndugu Wajumbe; Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya
kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu
kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia. Tumechelewa
kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio yetu. Kwanza tulipata
kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM). Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja
kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha
3
kutosha.
Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho kinakidhi sifa
za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma . Tumekiafiki na
matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi
kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta
ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa. Wageni
Karibuni Ndugu Wajumbe; Kama mjuavyo Chama cha
Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko duniani. Tumekuwa na mazoea
ya kualikana katika mikutano mikuu yetu. Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa
niaba yenu niruhusuni niwashukuru sana
wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa kukubali mwaliko
wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha
udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi
kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa
Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki
nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu. Ndugu Wajumbe; Tunawakaribisha
kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa
nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa
CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama
si uadui. Wamethibitisha jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na
kukomaa hapa nchini. Nawashukuru sana
pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi. Kuwepo
kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na
kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio na kuwafanya wale wote
wasiokiombea mema Chama chetu watahayari na kufadhaika. Karibuni Diaspora
4
Ndugu
Wajumbe; Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama
chetu waliopo nje, Marekani, Italia ,
India na
Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu
kuja kushiriki nasi. Hawa wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha
bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu. Agenda ya
Mkutano Ndugu Wajumbe; Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha
Mapinduzi ina mambo makuu manne. Kwanza
kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo
yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe
11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya
mageuzi hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa
Wilayani badala ya Mikoani. Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya
Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo
kutumika. Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu
wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba. Ndugu Wajumbe; Jambo la pili
litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa.
Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama
kwa miaka mitano iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa
Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania Bara. Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa
wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili taarifa ya kazi
za Chama na zile za
5
utekelezaji
wa Ilani. Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC
ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa
hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma,
wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu Ndugu Wajumbe; Katika hotuba yangu ya kushukuru
baadaya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 20067, pamoja na
kuzungumzia mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa
maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika
ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya hivyo kwa
sababu hilo
ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na
kila mwanachamawa CCM. Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha
Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa
ustawi na uhai wa Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada
kuimarisha Chama chao.
Ndugu
Wajumbe; Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu
Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha
Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi za Chama
tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na kila
kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa
kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum
uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa
6
vipengele
mbalimbali vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo. Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM,
kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo, Mradi wa
Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo. Ni kazi ya kudumu na wala siyo
tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku
alipostaafu. Tuongeze Wanachama Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu
katika uhai wa Chama cha Mapinduzi. Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani
ya Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya
kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati wote tuwe tunaingiza
wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba
ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli na
wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu Wajumbe; Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima
Chama chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea
na kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama
chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa
dola. Pia wanachama ni nyezo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi
hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma.
Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya kushawishi wananchi kupigia kura
wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi za uhakika. Tuwe na Viongozi
Wazuri Ndugu Wajumbe;
7
Kazi ya
kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala
siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea. Lazima Chama chetu kiwe na
viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema sera za
Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa
kuelimisha wanachama na wananchi. Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa
kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake.
Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni
maamuma. Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri
kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama hapana
budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa
na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na
kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya
vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba.
Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme,
tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu
Wajumbe; Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima
wanachama na jamii imuone hivyo. Chama chetu kinashindania kushinda akili na
mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye
katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma. Lakini, ili kiongozi
wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu muhimu.
Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama jamii inamuona kuwa si mtu
muadilifu itakuwa taabu sana
kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo ndugu zangu, lazima
tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa balaa na
hasara kwa Chama. Ndugu Wajumbe;
8
Baada ya
kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza
programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi
hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza na kukamilisha kazi ya ukarabati na
upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada
na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha
CCM cha Kivukoni na vyuo vyake vya kanda. Ndugu Wajumbe; Bahati nzuri vyama vya
ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika vimekubaliana kuwa
Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada wa vyama vyao pia. Ni
heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa
kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa. Tuko tayari
na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria. Vikao Vifanyike
Ipasavyo Ndugu Wajumbe; Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi,
kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa
vizuri na ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni
muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba
mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na
jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana
kuimarisha CCM. Watendaji Mahiri Ndugu Wajumbe; Kwa Chama chetu kuwa na
watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala. Lazima tuwe na watendaji ambao
ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa
mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea.
Pia, wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao
ya utendaji, kwa mujibu wa
9
shughuli
zao wanazozifanya. Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa
kazi hizo. Ni muhimu sana tukayazingatia haya
kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara.
Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi
kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama. Tumetimiza ahadi hiyo. Leo
nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri
uwezo utakavyoruhusu. Tujitegemee Ndugu Wajumbe; Lazima Chama chetu kiwe na
uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha. Kiwe na fedha za kutosha na
vitendea kazi. Hivi sasa hatuko hivyo. Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi
za kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku au hakuna. Jambo hili sasa liwe ni la
kufa na kupona kwetu kuhakikisha linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi
zote. Kila mmoja afikirie nini cha kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia ni
kufanya shughuli halali. Fursa zipo tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye azma
kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM. Lazima tushinde. Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo
tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari nzuri na
imara. Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi ujao bila ya
taabu. Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari iko mbioni. Kila
Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu. Jumuiya za Chama Ni wajibu wa
kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake zinaimarika na kutimiza
ipasavyo wajibu wake.
10
Jumuiya
ndiyo mkono mrefu wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa
wale ambao si wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa
wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya ni fursa
nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili wakati wa
uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya lazima zihakikishe
kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii adhimu.
Ndugu Wajumbe; Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa
kuimarisha Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu wa kila
mmoja kufanya. Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa ajili hiyo na rai
yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na kila kiongozi anatimiza
ipasavyo wajibu wake. Mageuzi Ndani ya Chama Ndugu Wajumbe; Kwa dhamira ya
kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa
tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kuanzisha mchakato
na kufanya mageuzi ndani ya Chama. Lengo kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama
chetu kuwa na taswira inayovutia katika mitazamo na hisia za wanachama wake na
wananchi. Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee
kupendwa na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania . Tunataka wanawake na
wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye nguvu waone
kuwa CCM ndiyo kimbilio lao. Ndugu Wajumbe; Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya
Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:1. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi
kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
11
2.
Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele
kwa kasi maendeleo ya taifa letu; 3. Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo
wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na
wananchi; 4. Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze
kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima; 5. Kukiwezesha Chama
kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na
kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao ;
6. Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda
chafu za vyama vya siasa; na 7. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na
maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe; Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa
kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama
utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka mtakumbuka
kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya.
Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika muundo wa Chama na moja ya
matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka
wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa na zile za taifa zikapunguzwa.
Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi
wakuu wa Chama wastaafu. Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na
viongozi wake. Ndugu Wajumbe; Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na
Jumuiya zifanyike mwaka mmoja. Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka
12
kujipa muda
wa kutosha wa kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola.
Uamuzi huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa uchaguzi.
Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana na
mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe. Lengo ni
kuziwezesha ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi vizuri zaidi.
Ndugu
Wajumbe; Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa sana kwa sababu ya
umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya jamii na wanachama wake. Pia,
kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha wanachama na wananchi cha kutaka
tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo katika jamii kuwa ni Chama
kisichokerwa na rushwa. Hicho ni kilio cha dhati kwa watu wenye nia njema na
CCM: Chama chao, wanachokipenda na kukiamini. Chama ambacho bado hakina badala
yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake. Halmashauri Kuu ya Taifa
iliamua mambo mawili yafanyike. La kwanza, mfumo mzima wa kushughulikia masuala
ya usalama na maadili katika Chama utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama
kichukue hatua na lazima kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na
wanachama wasiokuwa waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke
mbele ya jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo
vikao husika katika Chama vichukue hatua. Ndugu Wajumbe; Hayo ni baadhi tu ya
mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama.
Utekelezaji wake umeanza. Yapo yaliyokamilika na yapo yanayoendelea
kutekelezwa. Yapo mambo mengi ambayo ni endelevu kama
vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi kuendelea kulikemea na kusimama
kidete kupambana na tatizo hili mpaka likomeshwe.
13
Ni kwa
maslahi na heshima ya Chama chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka
tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari kwa uhai wa Chama chetu. Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe; Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa
tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi na Dkt.
Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Pia tulipitisha Ilani ya
Uchaguzi ya 2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa
ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya
Rais wa Zanzibar .
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa taifa
letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wengi
zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo, tumeunda Serikali zote mbili
za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri. Ndugu
Wajumbe; Kwa upande wa Zanzibar ,
tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mambo yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga
mkono na kuwatakia heri Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad na Makamu wa
Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd. Tunawapongeza sana kwa mafanikio yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na
umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali ya Umoja
wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi. Ndugu Wajumbe; Uchaguzi uliopita kwa upande wa
Tanzania Bara ulikuwa na changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa
nazo. Zinaelezea matokeo tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini
zaidi katika uchaguzi ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja
lililo dhahiri ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo
uliotuwezesha
14
kukabili
changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo, mbinu hasi
zilizotumika zingetufanya tushindwe. Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa na
mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na
watakaochaguliwa katika Mkutano huu. Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius
Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami
napenda kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni Ushindi. Ndugu Wajumbe; Nawaomba
wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke na kuzingatia Umoja.
Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke. Tuimbe Umoja kimoyo moyo na tubainishe
wazi wazi kwa kauli na matendo yetu kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu!
Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa
kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana na tulioshikamana. Nataka tuondoke katika
Mkutano sote tukivuta kamba upande mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie
kukabiliana na kauli, matendo au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja
ndani ya Chama chetu na miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano
huu uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa watu tunaovutana
na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala kuwatafutia ushindi
wagombea wa Chama chetu. Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao: “vita
vya panzi furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama
chetu kiwe hivyo. Ndugu Wajumbe; Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta
uongozi ndani ya Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa
ndiyo chanzo kikuu kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama
chetu. Hili ndugu zangu siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya
msingi ya mwanachama na raia wa Tanzania .
Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki yake hiyo? Kwa
nini afanyiwe vitimbi,
15
vitendo
viovu au njama za kuhujumiwa? Nani mwenye haki zaidi ya mwanachama ama raia
mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na msingi. Ni ubinafsi na uchu wa
madaraka uliopitiliza mipaka. Watu wa namna hiyo ni hatari sana
kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama chetu kizuri kama
tamaa zao zisipokidhiwa. Ndugu Wajumbe; Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi
wale wote wanaochukiana kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao . Wafanyayo siyo
sahihi, wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa za
ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba wahusika watoe
ushirikiano wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki katika uchaguzi,
walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya rushwa, wakumbuke
kuwa Chama chetu kina utaratibu wa kushughulikia malalamiko yao . Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya
vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika vyombo vya
habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta ufumbuzi. Ndugu
Wajumbe; Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya
kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya
kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni haki ya
raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia ni kufanya
vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu. Kuwalazimisha au kuwashinikiza
kujiunga na kundi fulani siyo sawa. Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au
amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya
demokrasia iwe haina maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni
kutumia fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au
kumuunga mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni
utovu wa
16
maadili
usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita kwa nguvu zetu
zote. Naomba wote tushirikiane katika mapambano haya kwa heshima ya Chama
chetu. Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Ndugu Wajumbe; Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa Serikali zetu zote mbili. Taarifa
zitakazotolewa na Waziri Mku, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali
ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali
Idd kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu.
Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo yahusuyo
shughuli za Serikali. Nchi Iko Salama Ndugu Wajumbe; Napenda kuanza kwa
kuwahakikishia kuwa Tanzania
iko salama pamoja na kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama.
Hakuna tishio lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi uko
salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili kutofautiana
wapi ulipo mpaka halali. Hakuna jambo lo lote linalofanywa upande wa wenzetu
ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi yetu kuwa hatarini. Kwa
sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza Majeshi yetu mpakani na anayesema
tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na kushushuliwa. Ndugu Wajumbe; Tumeendelea
na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa
kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita. Lengo letu ni kukuza
nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake kivita. Hali
kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na
ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa raia, yaani maisha na mali zao,
matukio ya uhalifu yanaendelea
17
kupungua.
Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za
kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia
kazi. Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi
ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama. Ndugu Wajumbe; Pamoja na
kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la kigaidi, wakati wote
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya tahadhari kuepuka
kushtukizwa. Kama mnavyokumbuka mwaka 1998
Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza
maisha. Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya. Aidha, tuko
katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari Kuu ya
Hindi. Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa nyara meli
katika bahari yetu . Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari. Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini yanasikitisha na
kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu ya kuheshimiana na
kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini, kabila rangi au maeneo
tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali haitawavumilia au kuwaonea
muhali wale wote wanaohusika na kuchochea vurugu hizo. Tumechukua hatua na
tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi
na wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia
umuhimu wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana. Tusipofanya hivyo nchi
yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo. Ndugu Wajumbe; Inatia
moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi. Kwa sababu hiyo pamoja na
jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi yetu hawajafanikiwa kuwagawa
na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba Watanzania wenzangu
18
tuwe na
moyo huo huo na sisi katika Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote
anayetaka kutuvurugia amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake. Ndugu
Wajumbe; Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote
asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala bora,
kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria. Kadhalika
tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola.
Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri. Muungano Imara Ndugu
Wajumbe; Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo la
kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini hasa kule Zanzibar . Jambo
linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na ghasia ili kuwalazimisha
watu kuwaunga mkono. Njia hizo hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba. Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu,
yatapokelewa na kupimwa. Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili
inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya kazi nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu analo jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe
kwa wahusika litashughulikiwa. Hali ya Uchumi Ndugu Wajumbe; Katika Mkutano
Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio tuliyoyapata na
changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kupunguza
umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea kupambana na changamoto
zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana na hali ya
19
kuyumba kwa
uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano(2011/12 – 2015/16). Mpango huu ni wa kwanza
kati ya mitatu katika safari yetu ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka
2025. Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia ifikapo mwaka 2025 nchi yetu
itaondoka katika kundi la nchi maskini sana
duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani tunataka pato la wastani la
Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za
Kimarekani 3,000. Lengo hilo
ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa Serikali na sekta
binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya viongozi na wananchi wa Tanzania . Ndugu
Wajumbe; Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla
katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni
Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu
na ushindani kimataifa. Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa
kipaumbele katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya
umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa kwani
lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya watu. Vijana ni
walengwa wakubwa. Mwelekeo wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi
iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu.
Mauzo yetu ya nje yanazidi kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa
dola za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya
fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1
inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8. Ndugu Wajumbe;
20
Changamoto
kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua kutoka asilimia 19.8
Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua huko ni
kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko
wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana
EWURA kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta. Kwa kuwa bei
za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa mfumuko wa bei na
kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa
kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi. Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika
kuendeleza mageuzi ya kilimo ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata
ziada kubwa ya kuuza nje. Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika
ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo
kwa wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini. Mapato na Matumizi ya
Serikali Ndugu Wajumbe, Tunazidi kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa
ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti
2012, kwa mfano, yalifikia shilingi bilioni 554.8 ikilinganishwa na makusanyo
ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi
za dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo
na taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo. Kwa sababu ya
kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi
trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo
linaloleta faraja ni kuwa mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao
umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka
huu. Utegemezi wa wahisani nao
21
unaendelea
kupungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21. Ndugu Wajumbe; Sambamba na
kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za umma
vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na kada ya uhasibu
katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia ni matokeo ya kazi nzuri
inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma. Hati Chafu katika idara za Serikali
zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi kila mwaka. Hivi sasa
tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika na kazi
iliyofanyika au huduma iliyotolewa. Uwekezaji Ndugu Wajumbe, Serikali imechukua
hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara hapa
nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuongeza vitega uchumi
nchini na kupanua biashara ndani ya nchi na kati ya nchi yetu na nchi nyingine
duniani. Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka
pale ambapo uwekezaji unaongezeka. Takwimu zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa
ukiongezeka mwaka hadi mwaka katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini,
fedha, ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa gesi na mafuta. Tumepata mafanikio
makubwa katika utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa
wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani
ya dola za Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000. Haya
ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi. Tutaendelea kutumia
fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa
lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Ili kufanikisha
22
hayo,
tutaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege
na teknohama. Miundombinu Ndugu wajumbe; Moja ya vipaumbele vya juu vya
Serikali ya CCM ninayoiongoza ni kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini,
majini na angani nchini. Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya
Serikali ambapo miundombinu ni ya pili baada ya elimu. Mwaka huu ni shilingi
trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na
elimu yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 2.4, na afya yenye shilingi
trilioni 1.5 sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa
kutambua mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu
wake. Usafiri unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua,
shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo zinaimarika. Ni kichocheo kikubwa
cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na
kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini. Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko wakati mwingine wo
wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara zenye urefu wa kilometa
11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu mbalimbali nchini.
Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami na barabara zote
kuu ziwe za lami. Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri.
Tumeanza kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki
kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni,
2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma ,
Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa
ujenzi wa barabara katika Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo
na kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni mashahidi. Karibu
23
tunafikia
ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma. Ndugu Wajumbe; Inafurahisha
zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa barabara
tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe. Aidha, uwezo wa Mfuko wa Barabara
(Road Fund) nao umeongezeka sana
kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430. Hali hiyo
imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara mbalimbali nchini. Kwa
ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye Halmashauri zote nchini. Ndugu
Wajumbe; Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari
na usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika utekelezaji wa
lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za ujenzi na ukarabati wa
miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na uwezo wetu. Tunaendelea kuchukua
hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu Ndugu wajumbe; Tumefanikiwa kupanua sana
fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika ngazi zote. Kuna watoto wengi
katika elimu ya awali, na kwa elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri
wa kwenda shule wamejiandikisha. Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia
asilimia 100 ifikapo mwaka 2015 kama
ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari,
wananchi na wadau wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na
shule ya sekondari. Kwa sababu hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya
2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka
kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu. Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi
sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya
166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa mwaka
24
2005. Ili
kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
ili iwape wanafunzi wengi mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka
kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu.
Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005.
Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe; Upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua
changamoto mbalimbali kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto hizo kuwa
ni pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa vifaa
vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini.
Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo. Tumeongeza
vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu. Bajeti ya
elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu,
maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi
karibuni nilipokuwa Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote
nchini kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya sayansi katika
miaka miwili ijayo. Afya Ndugu wajumbe; Suala la afya ya Watanzania tunalipa
umuhimu mkubwa sana .
Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi
trilioni 1.5 mwaka huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera mpya
ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa
kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia Watanzania
huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa tano. Vile vile, ni
kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
25
Katika
mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa madaktari, wauguzi na
wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu hao katika vyuo vyetu
hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na tutaendelea kujenga vyuo vipya,
wakati huo huo tukipanua vilivyopo. Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana na
maradhi makubwa yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi
yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya
kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana. Maambukizi ya
virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana
na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar
tunakaribia kutangaza kufutika kwa maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu
maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa
kuchunguza na kutibu maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa
maradhi tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari
ni hatua, naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri. Umeme na Maji Ndugu
wajumbe; Tunaendelea kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini.
Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji.
Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya mawe.
Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo iko mbioni. Pamoja na hayo
tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili
mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
26
Hivi majuzi
tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam . Litakapokamilika nchi yetu
itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa
mgao na upungufu wa umeme nchini. Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa
umeme nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4
Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo
la asilimia 30 ifikapo 2015. Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi
maji safi na
salama zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza ni ule ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi
yetu hayana vyanzo vya maji karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame.
Katika maeneo ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha kujenga miradi ya
maji ya bomba kutoka masafa marefu. Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo
wa kifedha kwa miradi mingi inayohitaji pesa nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kufuatia utekelezaji ulio makini wa
programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya
watu wa mijini wanaopata maji safi
na salama. Ni matumaini yangu kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la
upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia 90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati
nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali
nchini na itapokamilika tutafikia lengo letu au hata kulivuka. Pongezi kwa
Kuchaguliwa Ndugu Wajumbe; Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu
Mwenyekiti wa Zanzibar
na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Tanzania Bara
watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi
zao. Napenda kuchukua nafasi hii kwashukuru kw dhati Rais Amani
27
Abeid
Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza
Chama chetu. Wamekifanyia Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi
kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa
mambo mengi ya Chama na nchi. Nawashukuru sana .
Sote tuwatakie afya njema na maisha marefu. Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke
kuandika ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe wengi kwa miaka
mingi ijayo. Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe,
nirudie kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa magumu ya uchaguzi
mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga Chama. Tibuni
majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba nyufa za uchaguzi na
migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi. Kumbukeni wosia wa Baba wa
Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni
Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa
maslahi ya Chama chetu na nchi yetu. Hitimisho Ndugu Wana-CCM; Kwa kuhitimisha
naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ujenzi wa
Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Bado
kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote hayo mawili. Tunaitambua na tunayo
mipango thabiti ya kutekeleza majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi
kikubwa katika kufikia malengo yetu. Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja
ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa
Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi. Mungu Ibariki Afrika! Mungu
Ibariki Tanzania !
28
Kidumu
Chama cha Mapinduzi Asanteni sana
kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment