Kombe la Mataifa ya Afrika lililoanzishwa mwaka 1957 limeongezeka umaarufu
katika macho ya wapenda soka si barani Afrika tu bali dunia nzima, kwani vilabu
vya mpira wa miguu hasa barani Ulaya hutumia michuano hii kuchukua wacheaji wa
kuwasaidia kwenye timu zao.
Kombe hili lilianza kwa kushirikisha timu tatu tu nchini Sudan lakini sasa kuna timu 16 zinazowania kombe
hilo linaloshikiliwa na timu ya Zambia
lililobeba kwa mara ya kwanza mwaka 2012.
Nchi ya Misri ndiyo ya kwanza kunyanyua kombe hilo nchini Suda baada ya
kuwafunga Ethiopia magoli 4-0 katika fainali, na hiyo imekuwa kama nyota njema
kwa nchi ya Misri kuendeleza ubabe wa soka barani Afrika kwa kuchukua kombe
hilo mara saba tangu kuanzishwa kwake mwaka huo wa 1957.
Orodha ya timu zilizochukua kombe la mataifa ya Afrika ni kama ifuatavyo:
1957: katika timu nne zilizothibitisha ushiriki Afrika Kusini ilijitoa
katika mashindano na kuzibakisha timu tatu za Misri,
Sudan na Ethiopia. Misri wakawa mabingwa wa
kwanza wa kombe hilo kwa kuwachapa Ethiopia
4-0 katika fainali.
1959 : Misri walichukua ushindi kwa mara ya
pili mfululizo wakiwa nyumbani katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu tatu tu
za Sudan, Ethiopia na wenyeji Misri. Katika
fainali Ethiopia
walikubali uteja kwa mara ya pili kwa kulazwa 4-0.
1962 : Ethiopia waligoma kugeuzwa kichwa
cha mwendawazimu na Misri kwa kutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kuichapa
Misri 4-1 katika muda wa nyongeza baada ya dakika tisini za kawaida kuisha kwa
suluhu. Mchezaji wa Ethiopia Menguistu Worku, ndie alieiwezesha nchi yake ya Ethiopia
kuwa wafalme wa soka barani Afrika kwa mara ya kwanza kwa kuingiza magoli
mawili peke yake katika dakika za nyongeza. Tunisia
na Uganda
zilishiriki kwa mara ya kwanza na kufanya idadi kutoka tatu mpaka tano
1963 : Wenyeji Ghana waliutumia vema mji wa Accra
kwa kunyakua kombe hilo mara ya kwanza kwa
kuichapa 3-0 Sudan
katika fainali. Mwaka huo timu ziliongezeka na kufikia sita,
Kadhalika fainali za mwaka hu rikodi ya mabao 6-3 iliyowekwa na
Misri dhidi ya Nigeria
ndiyo idadi kubwa ya magoli iliyowahi kufungwa katika mechi moja ya michuano
hiyo ya kombe la Afrika mpaka sasa.
1965: Ghana waliendeleza ubabe kwa kuwaaibisha wenyeji
Tunisia
kwa mabao 3-2 kwenye fainali katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 za
kawaida kuisha kwa suluhu. Mwaka huu wa 1965 timu mbili za DRC Congo na Ivory Coast
ziliongezeka.
1968 : Congo
DRC walinyakua ubingwa wa Afrika kwa mara ya kwanza nchini Ethiopia kwa kuifunga Ghana
walioingia kwenye hatua ya fainali kwa mara ya tatu mfululizo tangu kuanza
kushiriki mwaka 1963, bao pekee la Pierra Kalala ndilo lililozamisha ndoto za Ghana kuchukua kombe hilo mara ya tatu mfululizo.
1970: Kwa mara nyingine tena Ghana walinyang’anywa tonge mdomoni na Hassabou
el Saghir katika fainali iliyoisha kwa Ghana kulala bao 1-0. Hii
ilidhihirisha kuwa kwa kipindi hicho Ghana ndiyo ilikuwa timu bora ya
Afrika inayocheza soka la hali ya juu mpaka kufanikiwa kuingia fainali za
Afrika mara nne mfululizo na kufanikiwa kushinda mara mbili mfululizo, yaani
mara ya kwanza waliposhiriki na mara ya pili kushiriki
1972: Kwa mara ya kwanza na mwisho nchi ya Congo
Brazzaville kuchukua kombe la Afrika ni mwaka huo wa 1972 nchini Cameroon katika mji wa Yaounde
ambapo mchezaji wa Congo Brazzaville Micahel M’Bono alitumbukiza wavuni mabao
matatu peke yake na kuitoa kichwa chini Mali kwa mabao 3-2.
1974: Huu ndiyo mwaka pekee katika historia
za michuano ya kombe la Afrika mchezo wa fainali kurudiwa, ambapo katika mchezo
wa kwanza DRc Congo
walifungana 2-2 na Zambia
nchini Misri, kutokana na sababu zisizozuilika mchezo uliahirishwa na kuchezwa
siku mbili baadae.
Katika mchezo wa pili Zambia walilala kwa mabao 2-0 hivyo DRC Congo
kuwa mabingwa kwa mara ya pili tangu walipochukua kwa mara ya kwanza mwaka 1968
nchini Ethiopia.
Mchezaji wa DRC Congo Mulamba Ndaye ndie alieibuka kidedea kwa kuweza kuifungia
mabao yote ya usindi katika mechi zote mbili, yaani ile ya kwanza iliyoisha kwa
2-2 na ya pili iliyorudiwa ya mabao 2-0.
1976: Haya ndiyo mashindano ya pili na
ya mwisho kuamuliwa kwa mfumo wa ligi na Morocco
kushinda kwa point moja mbele ya Guinea
baada ya timu hizo kutoka suluhu ya 1-1 katika mechi ya mwisho nchini Ethiopia.
1978: Ghana
walichukua kikombe kwa mara ya tatu nyumbani kwao Accra,
baada ya mchezaji wao Opoku Afriyie kutumbukiza mabao mawili katika fainali
dhidi ya Uganda
walioingia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza hivyo kuoshia nafasi ya pili kwa
kufungwa 2-0.
1980: Nigeria walitumia vema uwanja wa
nyumbani kwa kuichapa Algeria mabao 3-0 katika fainali iliyotawaliwa na
mchezaji wa Nigeri Segun Odegbami kufunga mabao yote matatu, na kuwa washindi
wa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Itakumbukwa katika mwaka huu Rais wa TFF Leodger Tenga aliongoza
kikosi cha Taifa Stars nchini Nigeria
kushiriki kwa mara ya kwanza na mara ya mwisho michuano hii.
1982: Ghana
walifanikiwa kuchukua kombe hili kwa mara ya nne dhidi ya Libya kwa mikwaju ya penalt 7-6 na
kuweka historia kuwa fainali za kwanza
za kombe la Afrika kuamuliwa kwa mikwaju ya penalt. Katika fainali hizo
ndipo jin ala Abedi Pele alietokea ‘benchi’ na kuonyesha kipaji cha hali ya juu
mbali ya umri wake mdogo hivyo kuwa nyota wa soka barani Afrika na dunia
kuanzia mwaka huo.
1984: Kwa mara ya kwanza Cameroon walichukua kikombe hicho katika fainali
iliyowakutanisha na Nigeria
ambapo walishinda 3-1.
1986: Cameroon walifanikiwa kuingia fainali
kwa mara ya pili lakini wakafungwa na Misri kwa mikwaju ya penalt mbele ya
mashabiki 100,000 nchini Misri kwenye uwanja wa Cairo Stadium.
1988: Kwa mara ya tatu mfululizo Cameroon waliingia fainali lakini walionyeshwa
upinzani mkubwa na Nigeria
kabla ya mchezaji wa Cameroon
Emmanuel Kunde kuifungia timu yake kwa penalt pekee hivyo Nigeria kulala 1-0 mjini Casablanca.
1990: Algeria
iliifunga Nigeria
5-1 hivyo kutawazwa mabingwa wa soka barani Afrika kwa mwaka huo wa 1990.
1992: Kombe la Afrika liliongeza
mwamko na kufikia timu 12, kichekesho kilikuwa siku ya fainali ambapo Ivory
Coast iliilaza Ghana kwa
penalt 11-10 baada ya muda wa kawaida na muda wa nyongeza kuisha kwa suluhu
nchini Senegal.
1994: Zambia
walifika fainali ingawa walipoteza karibu kikosi chote katika ajali ya ndege
miezi kadhaa nyuma nchini Gabon,
lakini Nigeria haikuwaonea
huruma baada ya kuwatundika goli 2-1 katika fainali hiyo ambapo goli zote mbili
za Nigeria ziliingizwa
kimiani na Emmanuel Amunike aliekuwa akiwika sana kwa miaka hiyo.
1996: Kwa mara ya kwanza fainali za kombe la
Afrika lilishirikisha timu 16 cha kutia matumaini nchi ya Afrika Kusini
ilirudi katika michuano baada ya matatizo ya ubaguzi wa rangi nchini mwao
kuwatoa katika fainali za kwanza kabisa mwaka 1957.
Mark William wa afrika Kusini aliwakatili Tunisia kwa kutumbukiza goli mbili peke yake
hivyo Tunisia
kulala 2-0 na afrika kusini kuchukua kikombe kwa mara ya kwanza.
1998: Kuonyesha wana kiu ya michuano hiyo Afrika
Kusini waliingia fainali kwa mara ya pili mfululizo lakini Misri waliwatuliza
na kuwachapa 2-0 mjini Ouagadougou.
2000: Nigeria
kwa mara ya kwanza waliondoa kasumba ya wenyeji kufungwa katika fainali baada
ya kuichapa Cameroon
kwa mikwaju ya penalt 4-3 baada ya suluhu ya 2-2 katika dakika za kawaida na
nyongeza.
2002: ilikuwa ni nchini Mali ambapo Cameroon
walitawazwa mabingwa wa Afrika kwa mikwaju ya penalt dhidi ya Senegal iliyokuwa na vinara wa soka kama El-Hadji Diouf.
2004: Wenyeji Tunisia walibeba kikombe cha Afrika
baada ya kuwachapa Morroco 2-1.
2006: Misri walitawazwa mabingwa kwa mara
nyingine baada ya kuwachapa Ivory
coast waliokuwa na kikosi imara
kilichoongozwa na Didier Drogba.
2008: Misri waliendeleza ubabe na
kunyakua ushindi wa Afrika tena baada ya mshambuliaji wao hatari Mohammed
Aboutrika kuwainua mafarao hao dakika 13 kabla ya mchezo kuisha hivyo Ivory
Coast kulala 4-1 dhidi ya Misri kwa mara ya pili mfululizo.
2010: Ilikuwa ni mwaka wa maajabu katika
michuano hii baada ya Misri kuwa taifa la kwanza kushinda kombe hilo kwa mara
tatu mfululizo ilikuwa ni mjini Luanda
dhidi ya Ghana na kuifanya Misri mababa wa soka la Afrika kwa kuchukua kikombe
hicho kwa mara ya saba.
2012: Zambia walinyakua kikombe
hicho kwa mara ya kwanza baada ya tambiko lao mjini Gabon katika eneo walilopoteza
wachezaji wako kwa ajali ya ndege. Mikwaju ya penalt 8-7 dhidi ya Ivory Coast
iliamsha furaha ya wapenzi wa soka barani Afrika kwani watu wengi walikuwa
wakiwaonea huruma Wazambia kutokana na dua walizokuwa wakiomba ili kuweka
historia ya michuano hiyo.
Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania
29/01/2013