Saturday, January 12, 2013

MTU aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela.





Abubakari Kikulu (29), alipiga picha na mbunge huyo Desemba 23 mwaka jana, baada ya Lema kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara eneo la Mererani, ikiwa ni sehemu ya mikutano aliyoifanya kutokana na Mahakama ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake.

Mbali na kupiga picha hiyo na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari, kijana huyo alionekana katika picha hiyo akionyesha vidole viwili, ambayo ni alama ya Chadema.

Hata hivyo, baada ya picha hiyo, JWTZ lilimtilia shaka kijana huyo na kutangaza rasmi kumsaka, ili lijiridhishe kama ni mmoja wa wanajeshi wake.
Baada ya kumsaka kwa takriban siku 12, kijana huyo alikamatwa Januari 13, katika Mji wa Bomang’ombe wilayani Hai na baada ya kupekuliwa alikutwa na sare hizo.

Jana, Kikulu alifikishwa mahakamani mjini Moshi, akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kusomewa mashtaka mawili, ambayo yote alikiri kuyafanya kama ilivyodaiwa mahakamani.
Baada ya kukiri kosa hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Kilimanjaro, alimhukumu kifungo cha miaka minne jela, ili iwe fundisho wa wakosaji wengine wa aina hiyo.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka alimsomea mshtakiwa huyo mashitaka yake mawili, likiwamo la kujifanya Ofisa wa Jeshi, wakati akijua ni uongo.
Wakili huyo alidai mahakamani kuwa Januari 3, mwaka huu katika eneo la Bomang’ombe wilayani Hai, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kama mtumishi wa umma.

Katika shtaka la pili, wakili huyo alidai siku hiyo hiyo katika Mtaa wa Msikitini, eneo hilo la Bomang’ombe, mtuhumiwa alipatikana na sare za JWTZ kinyume cha sheria.

Sare hizo ni pamoja na suruali moja, mashati mawili na kofia mbili, vyote vikiwa na alama za Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya Hakimu Kobelo kumuuliza mshtakiwa kama ni kweli alitenda makosa anayoshitakiwa, mshtakiwa huyo alikiri makosa yake katika hali ambayo haikutarajiwa.

Kutokana na kukiri kwake makosa hayo, Hakimu Kobelo alimhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kwanza la kujifanya Ofisa wa JWTZ na miaka mingine miwili kwa kosa la pili.
Hata hivyo, Hakimu Kobelo alisema kuwa kwa kuwa adhabu hizo zinakwenda kwa pamoja (concurrent), mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, kosa alilolifanya mtuhumiwa huyo ni baya na linastahili adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotumia vibaya sare za majeshi nchini.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment