Tuesday, January 22, 2013

Unawafahamu waafrika waliodhulumiwa kwa kuipenda Afrika yao?


 
Patrice Lumumba akiwa amshikiliwa na waafrika wenzie baada ya Marekani na Ubelgiji kumtuhumu kuvuruga amani nchini Zaire. inasadikiwa mwili wake ulitumbukizw kenye pipa la asidi mpaka sasa kaburi lake halijaonekana.


Lumumba wakati wa harakati zake alipokuwa waziri mkuu nchini Zaire sasa inajulikana Congo DRC.

Patrice Emery Lumumba (2 Julai, 1925 – 17 Januari, 1961), alikuwa mpigania Uhuru wa Taifa la Zaire (Sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na Waziri Mkuu wa Kwanza halali aliyechaguliwa na Wananchi wa Taifa hilo. Aliuawa kwa Ushirikiano Mkubwa wa Mataifa ya Ubelgiji, Marekani na Vibaraka wao waliokuwapo huko Zaire Wiki kumi tu mara baada ya Uhuru wa Nchi yake, Januari 17, 1961, miaka 51 na siku 3 iliyopita.

Lumumba alikuwa Mwanaharakati wa kweli aliyeondoshwa katika uso wa dunia hii kwa hila wakati akipambana kuupinga utumwa wa kifikra na kiutendaji, ni mfano wa kuigwa kwa vijana wa leo walioamua kuyageuza maisha yao kama "Mipira ya Kiume" Kutumika na kisha kutupwa kando madhalili. Vijana wa leo ambao wameamua kuyakabidhi maisha yao kwa wapenda mamlaka huku wakikisaliti kizazi chao cha kishenzi.

Wakati huu tukidurusu Maisha ya Simba huyu wa Afrika ya zamani, ni muhimu sana kutambua kuwa Afrika ya sasa ni dhalili zaidi ya kipindi cha ukoloni mkongwe, Afrika ya sasa haina tumaini kwani vijana na watoto kama vizazi vya leo na kesho kwa dhahiri hawajitambui, hawana walijualo, ujinga wanaita maarifa, wanajiita "wasomi" ambao hawana uhusiano na wala hawana majibu ya matatizo ya jamii zao, wamekuwa makasuku wakutumainiwa na mabwana zao (ubeberu), Afrika inayokwenda mrama ambayo tumaini la kurejea kwenye hadhi na Utu wake Limepotea.

Aliyofanyiwa Patrice Lumumba unaweza ukadhani ni yeye peke yake, Utakuwa unajidanganya ndani ya nafsi yako. Joseph Mobutu hakuwa peke yake barani Afrika, walikuwepo wengi na bado wanagalipo na wengine zaidi wanazidi kujitokeza, thamani ya damu ya wanaadamu haitambuliki kabisa ndani ya bara la Afrika.

Wale waliodharau athari za mwanzo za akina Mobutu na wenzake, na wao yaliwafika yaliyowafika kutokana na kudharau dhambi zilizofanywa na dhalimu Mobutu kwa kugeuzwa kibaraka walio mtuilia. Leo Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imerithishwa maradhi yale yale ya kutokujali uhai wa mwanadamu.

Maradhi kama hayo, tukambukizwa na sisi Tanzania kwa mambo mengine makubwa na madogo na mengine mithili ya hayo yaliyo fanywa huko Congo. Wengine wakajifanya vipofu ati hawayaoni, yakiwemo ya mauwaji ya wanasiasa, uwekwajwi ndani bila makosa, wizi na Ufisadi wa Mali za Umma, Ubinafsi, Udini na Ukabili, Ukibaraka na kushadadia Ukoloni Mamboleo.

KINA LUMUMBA WETU: HUZUNI NA MAJONZI YA KUWAPOTEZA HANGA, SHARIFF, SADALLAH NA ABDULAZIZ K. TWALA.

"Karume hakuwapenda Wasomi, na hakuwa akiwaamini kabisa, hata ukiangalia wengi wa Viongozi wa ASP waliofungwa na Karume walikuwa ni wale Wasomi, Kama Othman Shariff.

Othman Shariff na Karume walikuwa ni Mahasimu ndani ya siasa za ndani za ASP hata kabla ya Uhuru wa Zanzibar, baada ya Mapinduzi Shariff aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu kisha mara tu baada ya Muungano na Tanganyika akateuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Marekani.

Inasemwa kuwa wakati flani Shariff aliporudi nyumbani Tanzania kwa mapumziko aliwahi kuonekana akipiga picha katika maeneo ya Ikulu, hilo tu la kuonekana akipiga picha Ikulu lilitosha kulifanya 'Baraza la Mapinduzi' kumtuhumu Balozi Shariff kuwa ni 'shushushu' wa CIA aliyekuwa akipeleleza kwa ajili ya Manufaa ya Serikali ya Marekani.

Mamlaka za Usalama zilimkamata kwa tuhuma za 'Ushushushu na Ukibaraka' lakini zilimuachia mara baada ya Rais Nyerere kuingilia hilo. Alishushwa Madaraka yake kutoka Balozi mpaka kuwa Afisa wa Mifugo katika Mkoa wa Iringa, Tanzania Bara.

Baadaye Usalama wa Taifa wa Zanzibar kwa amri Maalum ya Baraza la Mapinduzi ulitumwa kwenda kumkamata Balozi Othman Shariff Mussa huko Iringa na kumrejesha Zanzibar, Mwalimu Nyerere alijaribu tena kuingilia kwenye hilo baada ya kuombwa kufanya hivyo na Wazee wa Iringa.

Baadaye Nyerere alikubali kumkabidhi Shariff kwa Mamlaka za Usalama wa Taifa wa Zanzibar baada ya kushawishiwa na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, mara baada ya kufikishwa Zanzibar huo ndio ulikuwa mwisho wa Shariff.

Abdallah Kassim Hanga alikuwa Msomi kutoka Urusi na mtu Mashuhuri sana Miongoni mwa Wanachama Vijana wa Chama cha Afro-Shiraz (ASP). Mara baada ya Mapinduzi alitangazwa kuwa Makamo wa Rais wa Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar chini ya Karume kabla ya kuhamishiwa Jijini Dar es salaam kwenye Serikali ya Muungano mara baada ya Muungano. 

Punde tu Hanga alimtumbukia nyongo Nyerere kwa sababu ya Ukaribu wake na Kambona, aliyekuwa Waziri wa Nyerere wa Mambo ya Nje na Ulinzi. Wakati wa Uasi wa Jeshi la Tanganyika (King's African Riffles) mwaka 1964, alikuwa ni Kambona aliyekwenda kuzungumza na Wanajeshi wale akijaribu kuwatuliza wakati Nyerere akiwa Mafichoni.

Mara baada ya Kambona kukosana na Nyerere na kwenda Uhamishoni, Hanga naye alitazamwa kwa Jicho baya kwa kuwa alikuwa karibu mno na Kambona. Punde aliondolewa kwenye Baraza la Mawaziri na akaamua kuhamia Conakry, Nchini Guinea kwa kuwa alikuwa ameoa Mwanamke wa Kiguinea.

Baada ya muda, Rais Nyerere alipeleka Ujumbe kwa Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea, ambaye ndiye aliyekuwa amempa hifadhi Hanga Nchini mwake, akimuomba akubali kumrudisha Hanga Nchini Tanzania na akimuahidi kuwa Hanga asingedhuriwa na angebaki salama.

Kwa bahati mbaya, Mara baada ya Hanga kurejea Tanzania alikamatwa na akadhalilishwa hadharani wananchi wote wakishuhudia. Katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Nyerere alimleta Hanga Uwanjani hapo akiwa na Pingu mikononi.

Katika Hotuba yake aliyoitoa viwanjani hapo, Rais Nyerere alimdhalilisha na kumsema vibaya Hanga na kama haitoshi akakubali kumrudisha Zanzibar ambako aliteswa na kisha kuuawa kinyume kabisa na ahadi aliyoitoa kwa Rais Sekou Toure".

TUJIFUNZE KWA MAKOSA: FURAHA YA KUOKOLEWA KWA ALI SULTAN ISSA, PROFESA ABDULRAHMAN MOHAMMED BABU NA BAKAA YA MAKOMREDI WENGINE.

"Kesi ya kwanza ilikuwa ni kama Kuondoa Wapinzani, Ilionekana ni Kesi ya Kisiasa tu. Mamlaka za Utawala ziltaka tu kutuangamiza na kutupoteza Vigogo wote wa kilichokuwa Chama cha Siasa cha Umma Party.

Lakini Utawala wa Zanzibar ulikuwa na kikwazo kimoja katika nia na lengo lao hilo la kutuangamiza, Jijini Dar es salaam Nyerere alikuwa ameshamkamata Profesa Abdulrahman Mohammed Babu na akiwa amekataa 'kata kata' kuwarejesha Zanzibar akikhofia kuwa wangeangamizwa tu.

Wakati tulipogundua tukiwa Gerezani kuwa Babu naye alikuwa Gerezani huko Bara na kuwa tungefikishwa Mahakamani na sio kudhalilishwa tu hadharani na kuuawa kama walivyofanyiwa kina Hanga, tuliamini kwa dhati katika Nyoyo zetu kuwa hatutauliwa.

Aboud Jumbe, Mtu Msomi na Muelewa ndiye aliyekuwa Madarakani wakati huo, tofauti na Karume au Seif Bakari, na Babu akiwa hai. Kwa hili 'NAMSHKURU SANA' Nyerere.

Labda alijifunza kutokana na funzo la yaliyojitokeza alipoamua kuwakabidhi Hanga na Shariff kwa Serikali ya Zanzibar. kwa kukataa kwake kumkabidhi Babu na wafungwa wenzie waliokamatwa huko Bara kwa Baraza la Mapinduzi, Nyerere alituokoa sote tusiuawe. Kama angewakabidhi kina Babu, sote tungeangamizwa, sote tungeteketea.

Lakini Jumbe na Serikali yake walikaa chini na kufikiri kuwa 'Tunawezaje kuwaangamiza wote, ikiwa Kiongozi wa Mkasa huu yu salama huko Tanzania Bara'."

"HAKUNA ALIYE MBORA KWA WATU WOTE, NA WALA HAKUNA ALIYE MBAYA KWA WATU WOTE", FUNZO LA FUNGATE YA UHURU.

Maandishi haya (KINA LUMUMBA WETU na TUJIFUNZE KWA MAKOSA) ni sehemu tu ya Masimulizi ya Komredi Ali Sultan Issa wa Chama cha Umma Party, aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais Karume, Katika Ukurasa wa 206 wa Kitabu cha Mwandishi G. Thomas Burgess, kiitwacho "Race, Revolution and The Struggle for Human Rights in Zanzibar: The Memoirs of Ali Sultan Issa and Seif Sharif Hamad".

Kwa dhahiri maandishi yanaainisha mikasa, visa na masimango yafananayo na yaliyomkuta Komredi Patrice Lumumba yaliyowapata watu mbalimbali Nchini petu tofauti ikiwa kwa hapa yote hayo yalitendwa na Serikali yetu ya Kizalendo tofauti na aliyofanyiwa Lumumba ambayo yalikuwa na Nguvu na mkono mzito wa Mataifa ya Nje.

Maandishi haya ni funzo zito kwa Viongozi wetu walioamua kulala Usingizi Mzito wa Pono katika zama zao hizi za Fungate ya Uhuru wetu, wakiyatumia vibaya mamlaka na madaraka yao dhidi yetu, wakifanya ghiliba na hujuma za dhahiri juu ya rasilimali zetu na wakitumia kila nyenzo na silaha waliyonayo kwa kila aliyepaza sauti dhidi yao au kuwa tishio la Nafasi zao za kiutawala.

Maandishi haya ni wokovu na fursa ya mafunzo kwetu na kwa viongozi wetu kujifunza kutoka katika makosa ya mababa na mababu zetu kwa kuiga tu yale yaliyo mema na yenye tija kwa mustakabali wetu na kuacha yale Maovu yaliyofanywa na watangulizi wetu.

Ni maandishi yanayoonyesha Machungu, furaha, huzuni na shukrani, yakiainisha mikingamo, migongano, misuguano na makubaliano kati yetu na yakitupa wasaa wa kudurusu na kujenga namna bora ya miingiliano yetu. Zaidi ni maandishi yanayotuonyesha namna Wazee wetu walivyofanya Makosa na pia kujisahihisha, Kwa hakika ni funzo zito kwetu.

"KILA KIZAZI, KUTOKANA NA UTATA WA WAKATI WAKE, KINA WAJIBU. KIUTEKELEZE AMA KIUKATAE", FRANTZ FANON.

Hakuna jamii yoyote duniani ambayo ilishawahi kuendelea bila Uzalendo na Mapenzi ya dhati kwa Jamii (Watu) na Ardhi (Nchi) yao. Muhimu zaidi kutambua ni kuwa Uzalendo sio zao la Kinasaba bali ni zao la Utamaduni, Ustaarabu na Historia inayoishi na kufanya kazi. 

Kimsingi UZALENDO mtu hufunzwa, kizazi kilichopigania "Uhuru wa Bendera" wa bara hili kilirithi, kupata na kufungamana na Somo la Uzalendo kupitia madhila yaliombatana na Ukoloni Mkongwe, Mimi nauita Uzalendo wa Asili au utokanao na Mazingira.

Sisi kizazi cha sasa, ikiwa ni miongo kadhaa baada ya "Uhuru" hatukuweza kuwa na Fursa hizo za kupata nafasi ya kuwa na "Uzalendo wa Asili", na bahati mbaya ni kuwa hatuna pa kuupata na kujifunza uzalendo huo kwa kuwa tumeamua kuutupa Utamaduni, Ustaarabu pamoja na Historia inayoishi.

Muhimu kutambua ni kuwa Wajibu wa Kutekelezwa na Kizazi chetu hautuepuki kwa kuwa tu tumeamua kujikana, Kuepuka Maangamizi ni kuutekeleza wajibu wetu. Mpaka pale tutakapo rejea katika misingi ya uasili wetu, tukawa na "Cha kwetu" cha kuweza kukilinda na kukifia, kila nyanja ya maisha ikawa inasadifu Uafrika, hapo ndipo Uzalendo utakapomea na mapenzi ya Jamii na Ardhi yetu yatakapodhihiri kvitendo na hatimaye uhuru wa kweli kupatikana.

Mungu Ibariki Afrika Moja, Mlaze Pema Baba Lumumba na Mashujaa wetu wengine.

Makala haya kutoka ukurasa wa facebook : Watanzania mashuhuri

No comments:

Post a Comment