Na Hafidh Kido
Kuna siku nilikuwa
nikitembelea mijadala katika mitandao ya kijamii, nikakuta mada kuhusu
ujasiriamali. Mchangiaji mmoja aliuliza swali juu ya ujasiriamali unataka
vigezo gani. Alitaka kujua ujasiriamali ni pesa au nia ya dhati ndipo mtu apate
mafanikio.
Baada ya kutafakari kwa muda
mrefu nimeona ujasiriamali unahitaji mambo manne katika mengi ambayo watu wengi
wanayatumia kupata mafanikio. Mtaji, ubunifu, fursa na mawasiliano.
Kwa nchi zinazoendelea tatizo
kubwa ni ukosefu wa rasilimali za kutosha, kwa Tanzania si rasilimazi za kutosha tu
bali ni matumizi mabaya ya rasilimali tulizonazo ima kwa kuwapa wageni ama
kushindwa kuzizalisha kwa faida ya wote.
Hili hushusha pato la taifa
na kufanya ajira kuwa chache kwani mashirika ya umma na binafsi yanashindwa
kuajiri kwa kasi kinachotakiwa kutokana na pato dogo wanalopata katika huduma
wanazotoa ama bidhaa wanazouza.
Baada ya kuona hilo Serikali iliamua
kuanzisha mpango wa kupunguza na kuondoa umsikini Tanzania (MKUKUTA) na
Visiwani wakaanzisha (MKUZA).
Lakini mpaka sasa imepita
miaka mingi bado mipango hiyo haijazaa matunda wala kuonyesha mafanikio yoyote
zaidi ya uongeza vitambi kwa wakuu wa miradi.
Miaka ya hivi karibuni kumeingia
dhana mpya ya maendeleo katika jamii kwa kuzuka neno ‘ujasiriamali’ lakini watu
wengi ima hawaifahamu dhana hii ama wanaielewa vibaya.
Kwa mtu anaetaka kuwa
mjasiriamali kitu pekee anachotakiwa kuwa nacho ni maarifa ya biashara; baada
ya hapo ndipo yanapokuja masuala ya mazingira ya biashara, mwelekeo wa uchumi
katika nchi, sheria na masuala ya fedha za kigeni.
Aidha katika mambo manne
niliyoyataja hapo juu yaani Mtaji, Ubunifu, Fursa na Mawasiliano kuwa ndiyo
uhai wa mjasiriamali katika shuguli za kila siku, ufafanuzi wake ni huu.
Mtaji
Tukianza na mtaji katika
ujasiriamali hiki ndicho kitu cha kwanza mtu anaetaka kuwa mjasiriamali kupasa
kuwa nacho. Unaweza kuwa mtaji wa fedha, fikra ama matarajio makubwa katika
shughuli zako.
Maana bila mtaji huwezi
kuanza kitu chochote, lazima uwe na kitu kitakachoweka uhai. Fedha ni kitu cha
pili baada ya nia na umadhubuti wa kusimamia kile utakachokianzisha.
Watu wengi wanashindwa
kuendeleza shughuli za kijasiriamali kwa kuamini fedha ndiyo mtaji pekee kwa
biashara ama huduma ya kijasiriamali.
Mawasiliano
Hapa mjasiriamali anapasa
kuwa na mawasiliano mengi kadiri awezavyo, na mawasiliano yenyewe ni kwa wateja
wapya na wa zamani, wapinzani na washirika katika biashara na serikali.
Mjasiriamali ambae anatumia
muda mwingi kuwasiliana na watu anakuwa na nafasi kubwa ya kujiweka sawa ama
kukabiliana na changamoto anazokutana nazo katika shughuli zake.
Lazima ujue kuhusu mabadiliko
ya bei za bidhaa katika mataifa makubwa, ujue kuhusu sera za Serikali kuhusiana
na biashara unazofanya ama mawasiliano na wateja wako wa kila siku na wale
wapya kujua wanataka nini na hawataki nini katika biashara mnayofanya, maana
biashara ni maelewano.
Ubunifu
Katika vitu vinavyowashinda
watu wengi katika biashara ni kuwa wabunifu, wajasiriamali huamini baada ya
biashara kusimama basi kila kitu kinakwenda sawa.
Lakini hakuna kitu hatari kama kumchosha mteja wako kwa kuona kitu kilekile kwako.
Ni vema kubadilikabadilika ili kuendelea kumpa hamu mteja wako na hata kumvutia
mteja ambae alikuwa hapendezwi na mfumo ama mwonekano wa zamani katika eneo
lako la bishara.
Unaweza kushusha bei katika
msimu wa sikukuu, ama kubadili nembo ya biashara yako kila baada ya mwaka mmoja
ama wakati maalum hasa nyakati ambazo zinawagusa wateja wako wa imani fulani
ama kundi maalum la watu.
Fursa
Hiki ni kitu ambacho watu
wengi wanakikosa katika harakati za ujasiriamali, na sababu kubwa ni rushwa na
kujuana.
Wapo watu ambao wanapewa
kandarasi ambazo hawaziwezi ama wanashinda zabuni ambazo hawana uwezo nazo.
Lakini zote hizi ni fursa ambazo mjasiriamali anahitaji kuwa nazo ili aweze
kufika mbali katika shuguli zake.
Lakini hakuna kilichoharibika
ikiwa utakosa fursa kwasababu hutoi rushwa ama hujulikani. Maana waswahili
husema chema kinajiuza na kibaya kinajitembeza, onyesha juhudi katika kazi zako
watu watakufuata ili kutaka huduma zako, maana mbali ya mambo kuendeshwa kwa
kujuana lakini watu wanapenda ufanisi katika kazi na si kubebana.
Hivyo ni vema mtu anapopata
nafasi ya kufanya kazi basi afanye hivyo kwa kiwango cha juu ili walio pembeni
yake ama washindani wake waone tofauti kati yao na yako.
Faida na hasara za kuajiriwa
Kwa sasa watu wengi
wanafikiria kuacha kazi ili kujiajiri, ama utakuta asilimia kubwa ya watu
walioajiriwa serikalini na sekta binafsi pembeni utakuta wana biashara
ndogondogo wanazofanya ili kuwakimu. Kwa maana mishahara haitoshi kwa kila mtu.
Wataalam wa uchumi duniani
walipiga hesabu ndogo inayoonyesha ni namna gani mwajiriwa hawezi kutimiza
malengo yake ikiwa hatakuwa na biashara pembeni.
Taarifa zinasema zaidi ya
asilimia 90 ya wafanyakazi duniani hawajui njia nzuri ya kutafuta pesa, watu
wengi wanatumia kiasi kikubwa cha pesa kutafuta faida tofauti na kiasi
wanachorudisha.
Tuanatumia nguvu nyingi sana kubuni miradi lakini hatufanyi utafiti ni namna gani miradi hiyo itaweza kudumu.
Wajasiriamali wengi hufanya biashara za kupata kula ya siku moja tu. Elimu inahitajika sana.
Matokeo yake wanatumia maisha yao yote kutafuta pesa ambazo hawafanikiwi kuzipata ila wanawazalishia waajiri wao bila kujijua. Mbaya zaidi waajiri hao hawajali masilahi ya wafanyakazi waliowazalishia zaidi ya kuwalipa mishahara ambayo kimsingi haiwafai chochote.
Kwa mfano, ikiwa umeajiriwa na unafanya kazi kwa saa nane kwa siku, siku tano katika wiki na wiki 50 katika mwaka; maana yake utakuwa unafanya kazi saa 2,000 kwa mwaka.
Kwa mshahara wa kitanzania mtu anaelipwa mshahara wa juu ni milioni moja, maana yake kwa mwaka atakuwa anaingiza milioni 12, ambayo ameisotea kwa saa 2,000.
Sasa tujiulize kwa pamoja, ikiwa utaamua kuwa mjasiriamali unafanya shughuli zako mwenyewe kwa mikono yako kwa saa hizo 2,000 kwa mwaka ambazo ni sehemu ya saa 9125 kwa mwaka. Tumepiga hesabu ndogo ya saa 24 kwa siku zidisha siku 365 za mwaka.
Utakuwa unaingiza kiasi gani kwa jasho lako mwenyewe kwa saa zote hizo, na utakuwa na uhakika wa kupumzika muda unaotaka na kufanya kazi kwa muda unaotaka kikubwa ni nidhamu ya kazi. Tofauti na waajiri ambao hawajali umefiwa, unaumwa ama umechoka.
Hivyo tunakubaliana kwa pamoja kuwa suluhisho la umaskini katika nchi zinazoendelea ni ujasiriamali uliotukuka.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
0713 593894
10/1/2013
Dar es Salaam, Tanzania
No comments:
Post a Comment