Sunday, January 6, 2013

Coastal Union kusuka au kunyoa kesho....


Kocha msaidizi wa Simba SC ya Dar es Salaam Jamhuri Kihwelu ‘Julio Pereira’ amesema atajiuzulu ikiwa timu yake itafungwa na Bandari katika mechi yao ya mwisho katika kundi A kombe la Mapinduzi usiku wa leo uwanja wa Amaan Unguja.

Kwa mujibu wa Farouk Kareem ambae ni miongoni mwa waandaaji wa kombe hilo alitangaza jana uwanjani wakati wa mechi ya Azam na Miembeni iliyoisha kwa Miembeni kubugizwa magoli 3-1 na Azam, alieleza kuwa Julio amesema atajiuzulu nafasi yake kama kocha msaidizi wa Simba kwani Bandari si timu ya maana kuweza kuwafunga.

Michuano hiyo inayofanyika kila mwaka wiki mbili kabla ya tarehe 12 Januari kuadhimisha mapinduzi matakatifu ya mwaka 1964 Januari 12, lengo ni kusherehekea pamoja kwa kumuondoa Muarabu katika visiwa vya Unguja na Pemba ambae aliwatawala kwa karne nyingi.

Timu za Tanzania bara zinazoshiriki michuano hiyo ni Simba SC, Coastal Union, Azam FC na Mtibwa Sugar, timu moja ya Tusker kutoka nchi jirani ya Kenya ambao ni mabingwa wa soka mwaka jana nchini humo nayo inashiriki kama mgeni mualikwa.

Timu za Zanzibar ni Miembeni, Bandari na Jamhuri ya Pemba. Michuano ina makundi mawili ambayo ni kundi A yenye timu za Simba SC, Tusker, Jamhuri ya Pemba na Bandari, wakati Kundi B zipo timu za Coastal Union, Azam FC, Miembeni na Mtibwa Sugar.

Mpaka sasa kundi la kifo limekuwa ni kundi B tofauti na watu walivyofikiria awali kuwa kundi la kifo lingekuwa ni kundi A ambalo lina timu nzuri tupu hasa baada ya kukusanya mabingwa watatu Tusker, Simba na Jamhuri ya pemba.

Aidha tofauti na matarajio katika kundi hilo timu mbili za Simba na Tusker zina nafasi kubwa ya kuingia hatua ya nusu fainali kwani timu hizo katika mechi zao mbili walishinda moja na kupata suluhu moja. Simba walicheza na Jamhuri nakuwafunga magoli 4-2, halafu mechi ya pili walicheza na  Tusker na kutoka suluhu ya bao moja kwa moja mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu hasa baada ya Simba kufungwa na Tusker katika mechi ya kirafiki jijini Dar es Salaam wiki moja tu kabla ya mchezo huo.

Tusker nao katika mchezo wao wa kwanza waliwafunga Bandari mabao 5, na suluhu moja dhidi ya Simba. Wakati Bandari wao wamekuwa kama watoto yatima katika kundi hilo kwani wamepoteza michezo yote miwili dhidi ya Tusker na dhidi ya Jamhuri, wamebaki na mchezo mmoja kibindoni dhidi ya Simba ambao hata wakishinda magoli 100 hawawezi kupita maana tayari Simba na Tusker wana point nne wakati wao hawana point hata moja.

Jamhuri kidogo wana matumaini kwani walipoteza mchezo na Simba na wakashinda mchezo wao dhidi ya Bandari, hivyo wana point tatu na wakishinda mechi yao dhidi ya  Tusker leo jioni wanaweza kuendelea na michuano hiyo, lakini tu wanatakiwa waombe ndugu zao Bandari wawafunge Simba ambacho ni kitu kisichotegemewa. Kwani wakishinda wao watakuwa na point sita magoli manne, wakati Simba wakishinda watakuwa na point saba. Mmenifaaahaaaamm…?

Sasa tuje kundi B ambalo ni la kifo, Coastal Union wanatakiwa kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Miembeni japo kwa goli moja ili wapate point tano, matokeo yoyote mbali ya hayo yanamaanisha Coastal Union wapo nje ya michuano. Kwani mchezo wao wa kwanza dhidi ya Azam walitoka suluhu ya bila kufungana, mchezo wa pili dhidi ya Mtibwa walitoka suluhu ya goli moja kwa moja. Maana yake Coastal Union wana point mbili na goli moja.

Wakati Mtibwa wao walifungwa magoli manne na Miembeni katika mchezo wao wa kwanza na kutoa suluhu ya goli moja na Coastal Union, hivyo wana point moja na magoli mawili. Wakishinda mechi yao dhidi ya Azam watakuwa na point nne.

Azama nao wana point nne na magoli matatu baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Coastal Union halafu wakashinda mchezo wao dhidi ya Miembeni kwa magoli 3-1. hivyo bado hawana uhakika wa kupita ingawa wanaongoza kundi, ila tu nao wanatakiwa kwa hali na mali washinde mechi yao dhidi ya Mtibwa ambapo watakuwa na point saba.

Hata hivyo, Mtibwa wakiwafunga Azam magoli zaidi ya moja na Azam wakashindwa kufunga goli hata moja katika mchezo wao maana yake Azam watatoka, kwani Azam wana magoli matatu tu na point nne, wakifungwa goli 2-0  na Mtibwa maana yake Mtibwa watakuwa na magoli manne na point nne.

Miembeni wao wana point tatu na magoli matano, wakifungwa na Coastal Union wametoka, ila wakishinda watakuwa na point sita maana yake hakuna ubishi wamepita tena kwa kishindo.

Hiyo ni tathmini yangu ndogo tu kwa namna michuano nilivyoiona, kundi B bado ni gumu halitabiriki. Lakini nimefurahi sana michuano imeleta changamoto ingawa yapo baadhi ya mapungufu nitakuja kuandika mapungufu hayo michuano ikiisha.

Chanzo… www.coastalunionsc.blogspot.com
COASTAL UNION OFFICIAL BLOG
unguja, Zanzibar
0713 593894
6/1/2013


No comments:

Post a Comment