Monday, January 21, 2013

Soma maneno ya Kaka yangu Maggid Mjengwa namna Hospitali ya Taifa Muhimbili inavyotutia kilizi.


Ndugu zangu,
Usiku huu nilifika Wodi ya Sewa Haji pale Muhimbili kumwona ndugu yangu aliyepata ajali.

Hakukuwa na ruhusa ya kuingia wodini kwa vile ni usiku. Baada ya kujieleza kwa mlinzi akanielewa. Nikaruhusiwa kuingia, maana, mgonjwa alinihusu sana na kesho nisingeweza kumwona.

Nilipoingia kwenye corridor za wodi niliingiwa na simanzi kuwaona wagonjwa waliolala pembezoni mwa korido, wengine wakiugulia maumivu.

Picha iliyonijia haraka ni kama vile nchi yetu imeingia kwenye vita ambavyo hatukujiandaa, na kwamba ninaowaona ni majeruhi wa vita waliokosa vitanda.

Kuna tatizo kubwa, maana Muhimbili ndio ilipaswa kuwa Hospitali kubwa ya Rufaa hapa nchini. Unajiuliza, kama Muhimbili hali ni kama hii, je hali ikoje kwenye hospitali za wilaya?

Nimerudi nilikofikia nikiwa hata hamu ya chakula imeniishia. Nawafirikiria wagonjwa wale wa kando kando ya korido za wodi watakavyopitisha usiku huu wakiwa wamelala chini, wenye maumivu na hata vyandarua hawana.

Na kuna wenye kufikiri , eti , wawekezaji wavune gesi yetu, na kama shukrani, watujengee kule Kilwa hospitali ya hadhi ya Appolo kule India. Kwamba ije iwahudumie Marais na waheshimiwa wengine! 

Wenye kufikiri hivyo wanasahau kuwa tuna Muhimbili yenye kuhitaji kurejeshewa hadhi yake ya Muhimbili ya enzi hizo. Inawezekana.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment