Friday, January 11, 2013

Unajua nini kuhusu Malcolm X ama Malik El-Shaabaz

 Malcolm X akiwa na rafiki yake kipenzi Abdulrahman Babu aliekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania

                                            Malcolm X akiwa na Rais wa Cuba Fidel Castro..



Malcolm X ambae alipobadili dini kuwa Muslam alijiita Malik El-Shaabaz, ni mpigania haki za Marekani weusi aliezaliwa tarehe 19 May, 1925 katika jimbo la Omaha, Nebraska nchini Marekani.

Kutokana na msimamo wake wa kupinga ubaguzi wa rangi uliokithiri nchini humo kwa wazungu kuwaona watu weusi hawastahili heshima ya ubinaadam Malcolm X alipata maadui wengi kiasi alipewa majina kama mchochezi na mpenda ghasia.

Lakini ukweli ukabaki kuwa yeye ndie mmarekani mweusi aliekuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi na fasaha ya kuzungumza katika historia ya nchi hiyo.

Mwaka 1946 akiwa na miaka 20 Malcolm x alipelekwa gerezani kwa kosa la wizi, akiwa gerezani alibadili dini na kuwa Muislam ambapo kidogokidogo alianza kupanda daraja na kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa dini ya kiislam nchini humo.

Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushawishi watu alijikita zaidi katika kupigania waafrika wenzie ambao walikuwa wakinyanyasika kutokana na sera mbovu ya nchi hiyo inayobagua watu weusi.

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, alitembelea bara la Asia, Mashariki ya kati na Afrika ambapo alipata mwanga mpya wa mabadiliko; aliporudi Marekani alianzisha Muslim Mosque, Inc na Organization of Afro- American Unity.

Lengo la kuanzisha taasisi hizo ni kuhakikisha wamarekani weusi wanapata jukwaa la kuzungumza matatizo yao na kuangalia mustakabali wa maisha ya kibaguzi nchini humo.

Kwa maelezo yake Malcolm X anaeleza kuwa sababu ya yeye kuingia katika harakati za kutetea watu weusi ni kutokana na ndugu zake watatu kuuliwa kinyama na wazungu kutokana na manyanyaso ya ubaguzi wa rangi.

Malcolm X alifanikiwa kupata watoto sita kutoka kwa mkewe Betty Sanders ambae baadae alibadili jina na kujiita Betty X baada ya kujiunga na kikundi cha black Muslims.

Katika harakati zake za kupigania haki za weusi nchini Marekani, Malcolm alifanikiwa kukutana na baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kama Keneth Kaunda wa Zambia, Gamal abdu Naser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanzania, Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa Congo, Ben Bella wa Algeria na Rais wa Cuba Fidel Castro ambae alihudhuria katika moja ya mikutano yake ya harakati za haki za binaadam.  Hata Abdulrahman Babu aliwahi kuwa mgeni mualikwa katika moja ya mikutano ya Malcolm X alipotembelea nchini Marekani kama rafiki wa mapinduzi ya watu weusi duniani. Wakati huo Babu alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, na Babu ndie aliemuunganisha Malcolm X na Mwalimu Nyerere.

Siku ya tarehe 21 February, 1965 wakati akihutubia katika mkutano wa Afro-American Unity katika mji wa Manhattan Marekani mbele ya umati wa watu 400 alipigwa risasi kadhaa mwilini na kukimbizwa hospitali ya Columbia Presbyterian na kutangazwa amefariki saa 3:30 usiku muda mchache baada ya kukimbizwa hospitalini hapo.

HAFIDH KIDO

kidojembe@gmail.com

0713 593894/ 0752 593894

11/1/2013

Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment