Na Hafidh Kido
Michuano ya kombe la
mapinduzi inayofanyika kila mwaka kuadhimisha sherehe za mapinduzi matakatifu
yaliyomng’oa mkoloni wa kiarabu katika visiwa hivyo mwaka 1964 inakwenda
mwishoni baada ya kubakia timu nne katika nane zilizoshiriki michuano hiyo.
Timu zilizoshiriki michuano
hii ni nane ambazo kundi A lilikuwa na Simba, Tusker (Kenya ), Jamhuri ya Pemba
na Bandari. Kundi B lilikuwa na timu za Coastal Union, Mtibwa Sugar, Azam FC na
Miembeni.
Timu zilizoingia hatua ya
nusu fainali ni Tusker na Simba kwa kundi A, wakati kundi B ni Azam FC na
Miembeni.
Nusu fainali ya kwanza
itachezwa jumatano (leo) saa mbili na nusu usiku katika uwanja wa Amaan kati ya
Simba na Azam FC, wakati nusu fainali ya pili itachezwa kesho alhamisi usiku
katika uwanja huohuo kati ya Tusker na Miembeni. Wakati fainali iategemewa
kuchezwa siku ya kilele cha sherehe za mapinduzi tarehe 12 January mwaka huu.
Simba kuondoa kikosi cha
kwanza katika michuano
Timu ya Simba kutoka Tanzania bara ambayo imefuzu kuingia hatua ya
nusu fainali katika michuano hii imeduwaza mashabiki wake wa Zanzibar
baada ya kutangaza kuondoa kikosi cha kwanza cha timu hiyo ili kuweka kambi
nchini Oman
kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu bara.
Wekundu wa mtaa wa msimbazi
kariakoo Dar es Salaam wanafanya hivyo ili kujibu mapigo ya watani wao Young
Africans nayo ya Kariakoo mtaa wa twiga baada ya timu hiyo kuwek kambi nchini
Uturuki kwa wiki mbili sasa.
Kocha mkuu wa Simba Mfaransa
Patrick Liewing aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kuwa ameamua kufanya
hivyo kwani anahitaji kukaa na kikosi cha kwanza cha timu hiyo ili kuweza
kuwajua vema hasa ikizingatiwa mzungu huyo bado hajawaona Simba wakiwa
uwanjani, kwani ameshuhudia mechi tatu za kombe la mapinduzi lakini asilimia
kubwa ilikuwa ni vijana wa timu B.
Kwa uamuzi huo maana yake
Simba watalazimika kuwaachia wachezaji wa timu B kuendelea na hatua ya nusu
fainali ambapo mechi ya kwanza watakutana na Coastal Union
kutoka mjini Tanga.
Mtibwa Sugar kuwekwa kambi
moja na Coastal Union
Waswahili wanasema akumulikae
mchana usiku atakuunguza, waandaaji wa michuano hii wamefanya kitendo cha ajabu
sana katika
taratibu za soka kwa kuwaweka wapinzani wawili kwenye hoteli moja.
Coastal Union na Mtibwa Sugar
ni timu zilizo katika kundi moja yaani kundi B, lakini cha ajabu wote wamewekwa
katika hoteli moja. Ni ajabu sana
kwa waandaaji kufanya kitendo hicho kwani wanajua wazi katika michuano yoyote
timu zinakuwa na usiri mkubwa hasa katika mbinu za kukabiliana na mpinzani
wawapo uwanjani.
Wachezaji kukaa eneo moja
kunaweza kuibua vitendo vya hujuma ama kuleta urafiki usio na msingi kwa timu
zao.
Sasa sijui ulikuwa ni uhaba
wa hoteli, kukosa fedha ama dharau tu kwa timu hizi kutoka Morogoro na Tanga.
Raia Mwema ilijaribu kuzungumza na waandaaji juu ya suala hili lakini majibu yao ilikuwa ni ya mkato.
Hakuna alietoa jibu la uhakika kuwa kwanini timu za kundi moja ziwekwe kwenye
kambi moja, mpira ni vita, kuna mbinu nyingi za ndani ya uwanja na mbinu nyingi
zaidi za nje ya uwanja. Lazima ZFA waandaaji wa michuano hii wajirekebishe.
Uwanja wa Mao Tse Dong
Lakini cha kushangaza
wameamua kuutumia uwanja wa Mao Tse Dong ambao hadhi yake hauwezi hata
kuchezesha ligi kuu ya Tanzania Bara. Upo katika hali mbaya sana ,
hakuna majukwaa na hata eneo la uwanja ‘pitch’ imezuiwa kwa kiasi kidogo sana . Laiti mashabiki
watakuwa na hasira ni rahisi kuweza kuwavamia na kuwadhuru.
Aidha hakuna vyumba vya
kubadilishia nguo wala vifaa vya usalama kama
mitungi ya kuzimia moto na milango ya dharura ikiwa kutatokea vurugu. Ni uwanja
ambao hauwezi kuuelezea kwa maneno matupu kuwa haufai hata kidogo kwa michuano
hii ambayo inashirikisha mpaka timu kutoka nchi jirani kama Kenya ama Uganda .
Uwanja hauna vyoo kiasi
wachezaji wakitaka kujisaidia ni tatizo kubwa kwani Raia Mwema ilishuhudia
wachezaji wa timu ya Miembeni wakijisaidia haja ndogo pembeni ya kuta za uwanja
huo bila aibu. Hata mashabiki wa kike wanaokuja kuangalia mpira wanakuwa na
wakati mgumu kupata huduma ya vyoo.
Hii ni changamoto kwa chama
cha soka cha Zanzibar ZFA kujipanga na kuomba msaada wa kujengewa viwanja vya
soka. Maana Zanzibar ina wachezaji wenye vipaji vikubwa vya soka.
Na hata timu ya Zanzibar
Heroes ilijizolea mashabiki wengi katika michuano ya Challenge mwaka jana.
Hivyo ni vema kuwapa mashabiki wa soka Zanzibar
kile wanachostahili. Hakuna anaejua lakini Zanzibar ni mji wa kitalii wanaweza kupata
bahati ya kupendekezwa kusimamia michuano ya Afrika ama Challenge kwa Afrika
Mashariki na kati.
Uwanja hauna majukwaa.... Mao Tse Dong Zanzibar.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
0713 593894/ 0752 593894
9/1/2013
Unguja, Zanzibar
No comments:
Post a Comment