Thursday, January 17, 2013

Vuguvugu la uchaguzi nchini Kenya...


Vituo vya kupiga kura vimefunga nchini Kenya katika mchakato mzima wa upigaji kura ya mchujo kote nchini.
Katika baadhi ya maeneo ya Nairobi na viunga vyake uchaguzi ulikabiliwa na changamoto nyingi za maandalizi huku baadhi ya vyama vikilazimika kuakhirisha shughuli hiyo hadi kesho.
Vyama vya siasa vinavyohusika hussusan muungano wa Cord unaoongozwa na waziri mkuu Raila Odinga havikuwa na mpangilio maalum na kuwaacha wapiga kura kusubiri kwa muda mrefu.
Wakati huo huo muungano wa Jubilee wake naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta na mwenzake William Ruto, ulikuwa na matatizo kama hayo na umelazimika kuakhirisha kura hizo za mchujo hadi kesho.
Hayo yanajiri huku baadhi ya vyama vikiwazuia wanasiasa kadhaa kugombea nyadhifa kwa ukosefu wa stakabadhi za elimu.
Wapiga kura wameelezea malalamishi yao katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi, kuu zaidi wakitaka kujua sababu ya maafisa wa chama cha ODM kilicho chini ya muungano wa CORD kukosa kutimiza ahadi yao kuhusiana na maandalizi ya uchaguzi.
Na kwa sababu hiyo baadhi yao hawakutaka kuvumilia zaidi na wakalalamika hata zaidi wakisema kuwa walikuwa wakinyimwa haki yao ya demokrasia. Picha ilikuwa ni ilele katika shule ya msingi ya St. Georges jijini Nairobi.
Licha ya wapiga kura kujitolea asubuhi na mapema kufikia saa sita hivi mchana hamna cha mno kilichokuwa kikiendelea. Na kama wenzao wa Kibera wakawalaumu viongozi wa chama kwa kubabaisha katika maandalizi ya shughuli hiyo muhimu. Na katika mkoa wa kati sehemu ya kiambu hali ilikuwa tofauti hata zaidi.
Wapiga kura walijipata katika hali hiyo na wakaambiwa na wanaohusika kuwa warejee kesho kuwachagua wawakilishi wao....Hata hivyo kinachojitokeza kwa sasa katika uchaguzi huo ni kuwa vyama vya siasa havikuwa vimejiandaa kikamilifu katika shughuli hii.
Kadhalika baadhi ya vyama vilionekana kutokuwa na orodha zinazohitajika za vyama vyenyewe na sajili ya wapiga kura kutoka kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka.
Vivyo hivyo ni muhimu kutaja kuwa sheria ya uchaguzi nchini Kenya inaonekana haijaeleweka vizuri na wanasiasa kwani kwa mujibu wa sheria inatakiwa shughuli hiyo kukamilika hii leo lakini dalili ni wazi kuwa matokeo ya kura hizo hayatapatikana yote leo kutokana na ucheleweshwaji ulioshuhudiwa.
Hii si mara ya kwanza uchaguzi wa mchujo kukabiliwa na utata nchini Kenya kwani ilifanyika hivyo vile vile katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 na ule uliopita wa 2007.
Na kwa sababu hiyo baadhi ya wansiasa wamehamia katika vyma vingine wakihofiwa kutotendewa haki katika uchaguzi huu wa mchujo.
Hata hivyo baadhi ya wagombea watakaoshinda katika kura hizi za mchujo watakuwa wamepata tiketi ya moja kwa moja ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Machi tarehe nne.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment