Monday, January 21, 2013

JINA la Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa majina yatakayotumika kuitambulisha mitaa ya Makao Makuu ya Mamlaka ya Palestina, Ramallah.Hayo yalithibitishwa na Balozi wa Palestina hapa nchini, Nasri Abujaish wakati wa hafla ya kuzindua jina la Barabara ya Yasser Arafat, iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam jana.
Abujaish alisema Mwalimu alikuwa na uhusiano mzuri na kiongozi huyo wa zamani wa Mamlaka ya Palestina ambaye pia alikuwa Rais wa kwanza wa Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO).

“Sababu kubwa za kuipa barabara hii jina hili ni kuwa Rais Arafat alizuru mara kadhaa hapa Tanzania akialikwa na Mwasisi wa Taifa lenu Mwalimu Nyerere. Uhusiano huu uliendelea baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuchukua madaraka na baadaye Rais Mkapa” alisema Balozi Abujaish.

Balozi wa Taifa hilo linalopigana vita visivyoisha kati yake na Israel aliwaambia waandishi wa habari waliohudhuria hafla hiyo kuwa, Arafat ndiye aliyeanzisha upinzani dhidi ya Taifa hilo dogo la Mashariki ya Kati kudai ardhi yao wanayoikalia kimabavu kwa zaidi ya miongo mitano sasa.

“Ni matumaini yangu kuwa kwa kufanya hivi tutaweka kumbukumbu zetu na vizazi vijavyo kuwa hai kwa waasisi wa mataifa yetu”
Abujaish aliongeza kuwa kiongozi huyo aliyefariki Novemba 2004 wakati akitibiwa katika hospitali moja ya kijeshi nchini Ufaransa, ndiye chimbuko la maono ya kutaka Palestina itambuliwe kama Taifa huru.

Alisema kuwa ingawa Arafat hayupo, lakini msingi aliouweka umezaa matunda kwa Palestina kutambuliwa kama Taifa ingawa siyo mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), lakini mapambano yataendelea hadi ardhi yao ipatikane na Palestina kuwa mwanachama kamili wa UN.

Balozi huyo alisema uhusiano wa Tanznaia kwa Palestina upo kwa jinsi wanavyoshikamana na kuwaunga mkono katika mapambano yao dhidi wakoloni wa ardhi yao kama ambavyo walifanya wakati wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini.

Katika hafla hiyo Diwani wa Kata ya Kigogo, Richard Chengula aliyemwakilisha Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda, alisema kuwa wananchi wa Oysterbay ndiyo waliamua barabara hiyo iliyokuwa ikiitwa Hill Road kupewa jina hilo kutokana na kuwa karibu na makazi ya Balozi wa Palestina.
 Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment