Friday, January 11, 2013

Abdulrahman Babu.... mchango wake unathaminiwa vipi?


abdulrahman Babu akiwa na mpigania haki za weusi nchini marekani malcolm X. Babu alipata mualiko maalum na Malcolm X kumtembelea na kutoa hotuba katika mkusanyiko wa wamarekani weusi nchini humo.


Mmoja kati ya marafiki zake wakubwa marehemu Abdulrahman Mohamed Babu,Profesa wa sheria kwenye chuo kikuu cha North Carolina, Bereket Habte Selassie (pichani) akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Abdulrahman Mohamed Babu alipofika Zanzibar akiwa njiani kwenda Dar Es Salaam kuhudhuria mkutano wa Nyerere Foundation hivi majuzi.Picha na Martin Kabemba

Abdulrahman Babu ni msomi na mwanamapinduzi wa kiafrika ambae alishiriki kikamilifu mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 januari, 1964. mapinduzi hayo yaliondoa utawala dhalimu wa kisultan visiwani humo ambao ulidumu kwa karne nyingi waafrika wakikandamizwa huku maslahi yao yakipuuzwa.

Babu alizaliwa mwaka 1924 mjini Unguja Zanzibar, wakati huo ikiwa chini ya utawala wa Waingereza.

Aidha kutokana na ufahamu wake katika masuala ya kimataifa Babu alifanywa mmoja wa wataalam wa mipango katika kamati ya mapinduzi iliyokuwa ikiongozwa na Abeid Karume ambae baada ya mapinduzi alikuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar.

Akiwa katibu mkuu wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Babu alitengeneza mahusiano mazuri na nchi za kijamaa hasa China. Hivyo kuwa mpigania uhuru wa kwanza Afrika mashariki na kati kutembelea nchi ya China mwaka 1959.

Hata hivyo baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar miezi michache baada ya mapinduzi tarehe 24 April, 1964 Babu aliteuliwa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali ya muungano wa Tanzania chini ya Julius Nyerere.

Kutokana na mahusiano mazuri na China, inasadikiwa Babu ndie kiungo kikuu kilichowashawishi wachina kujenga reli ya TAZARA. July 1965 nchi ya China ilitoa msaada wa Pauni 225 milioni kwa nchi mbili za Tanzania na Zambia ili kugharamia ujenzi wa reli ya Tazara kwa ushawishi wa Babu.

Lakini miaka michache baadae mnamo mwaka 1972 baada ya kifo cha  makamu wa kwanza wa Rais Abeid Amani Karume, Babu alikuwa miongoni mwa watuhumiwa 34 ambao walihukumiwa kifo kwa kuhusishwa na kifo cha Karume.

Kwa msaada wa Rais Nyerere, Abdulrahman Babu alikimbilia uhamishoni nchini Uingereza ambapo mauti yalimkuta tarehe 5 August, 1996 akiwa na umri wa miaka 72.

Kabla ya mauti kumfika mwaka mmoja nyuma yaani mwaka 1995 Babu alikuja nchini Tanzania kugombea nafasi ya umakamu wa Rais kupitia chama cha NCCR Mageuzi kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Augustino Lyatonga Mrema mgombea kiti cha urais.

Tume ya uchaguzi iliengua jina lake kama mgombea mwenza kutoka visiwani kutokana na hatia ya kifo cha Rais Karume mwaka 1972, hivyo alirudi nchini Uingereza ambapo alikuwa akiishi kama msomi na mhadhiri katika vyuo vikuu vya nchi hiyo kabla mauti hayajamkuta katika hospitali ya London Chest Hospital.

Babu katika maisha yake aliandika insha na makala kadhaa katika magazeti na majarida kuonyesha msimamo wake hasa wa usoshalisti akiunga mkono kambi ya Urusi na China katika vita baridi ya magharibi na mashariki.

Mpaka anafariki mwaka 1996 Babu alichapisha vitabu kadhaa mojawapo kikiwa ni ‘African Socialism or Socialist Africa’? Alichokitoa mwaka 1981.

 HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
0713 593894/ 0752 593894
11/1/2013
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment