elimu ya ujasiriamali haitolewi kwa wakati muafaka.
Na Hafidh Kido
Kila mwaka Tanzania inazalisha wahitimu wa
shahada ya kwanza wasiopungua 5000, wale wanaosoma vyuo vya ndani na vyuo vya
nje.
Maana ya idadi hiyo kubwa ya
wahitimu ni vita ya kutafuta ajira ambayo inaishia wahitimu kutembea na bahasha
za vyeti kila ofisi bila matumaini ya kuajiriwa.
Kama hiyo haitoshi hata wale
ambao wanapata bahati ya kuajiriwa wanakuwa na wakati mgumu sana
kutoa ushirikiano kazini kwani inawapasa kufundishwa upya namna ya kufanya kazi
kwani vyuo vingi barani Afrika vinafundisha nadharia na si vitendo kitu
kinachowagharimu sana
wasomi wapya.
Nchi zilizoendelea ziligundua
changamoto hii karne nyingi sana
tangu miaka ya 1700, ndipo wakaja na wazo la ujasiriamali. Lengo likiwa ni
kumfanya mhitimu kujiajiri mwenyewe bila kufikiria kuajiriwa.
Wachumi barani Afrika mbali
ya kuipokea dhana ya ujasiriamali bado wanaumiza vichwa kuhusiana na dhana hii
ili kuweza kuipatia tafsiri ya moja kwa moja.
Hata sasa ukienda mitaani
kuuliza watu maana ya ujasiriamali utapata tafsiri zaidi ya elf moja. Hakuna
mtu ambae atakueleza kitu cha kunyooka. Maana yake bado elimu ya ujasiriamali
haijasambaa katika vichwa vya watanzania.
Wachumi wanasema ujasiriamali
ni hali ya mtu kuthubutu kuanzisha kitu kipya katika biashara ili aweze kupata
faida baadae.
Kwa lugha ya kibiashara
mjasiriamali ni mbunifu ambae hunadi ubunifu wake kwa vitendo kupitia bidhaa
anazouza ama huduma anazotoa kwa njia mpya ya uzalishaji pesa sokoni.
Hapa ndipo panapochanganya
watu wengi, utaweza vipi kubuni kitu kipya ambacho hakipo katika jamii. Watanzania
wengi wanaonekana wavivu kwa kushindwa kuzitumia elimu zao vyema. Maana
ukimwambia mwanafunzi aliehitimu shahada ya biashara aanzishe biashara
atakwambia nianzishe biashara gani wakati kila biashara ninayoifikiria tayari
imeshashamiri katika soko.
Nilipokuwa masomoni nchini Kampala mwalimu wangu wa
somo la ‘micro economics’ anaitwa Ssekajubo Gideon, alipata kusema akiwa
darasani kuhusu ujasiriamali;
Alisema “Mjasiriamali ni yule
anaeleta mageuzi au mabadiliko katika soko na kuwajibika katika bidhaa au
huduma anayofanya kwa kutafiti mazingira ya biashara au huduma kabla hajaamua
kutoa pesa zake mfukoni kuwekeza katika shughuli hiyo ya kijasiriamali.”
Kitu nilichojifunza kutoka
kwa mwalimu huyu wa uchumi ni kuwa watu wengi wanakosa nafasi ya kutafiti
mazingira ya biashara kabla hawajaamua kutoa akiba yao ama mtaji.
Utaona watu wengi wanapata
pesa nyingi lakini ukiwaambia waanzishe biashara haichukui muda atakwambia
biashara ni mbaya na pesa zote zimeisha, kibaya zaidi atakwambia mbali ya pesa
kuisha lakini bado anadaiwa.
Kwa sasa ujasiriamali
unafundishwa katika ngazi nyingi za elimu kuanzia sekondari mpaka vyuo, lakini
hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika katika sekta ya ajira. Unaweza kujua
sababu?
Hao waalimu walioteuliwa
kufundisha somo la ujasiriamali wenyewe hawaamini katika ujasiriamali. Hapo
ndipo tatizo lilipo, hakuna siri.
Mwalimu wa somo la
ujasiriamali hana biashara hata ya kuuza mkaa, hajaonyesha mafanikio yoyote
katika kitu anachokifundisha. Maana yake hawezi kutoa mifano hai kwa wanafunzi
wake na hicho kinawafanya wanafunzi waamini wanachofunzwa ni somo tu kama yalivyo masomo mengine.
Hakuna uzito wowote
unaochukuliwa na wanafunzi wa somo la ujasiriamali, hiki ni kikwazo na
kunahitaji kufanywa utafiti kuona ni namna gani masomo ya ujasiriamali kwa
baadhi ya vyuo na shule za sekondari yameleta mafanikio kwa wanafunzi tangu
kuanzishwa utaratibu huo.
Mwalimu Ssekajubo aliendelea
kutueleza dhana ya ujasiriamali kuwa ni “Kwa yeyote anaetaka kuwa mjasiriamali
ni lazima awe na mapenzi ya biashara ama huduma anayotoa, asifuate mkumbo kwa sababu
tu biashara anayotaka kuifanya ni maarufu katika eneo analoishi.
“Bali mtu ajikite kwa dhati
na tija ili kupata kipato katika maisha yake la muhimu ni nia ya dhati na
kujitoa akubaliane na changamoto zozote atakazokutana nazo maana biashara
unapoanza ni ngumu na hakuna faida ya haraka labda iwe ni biashara ama huduma
ya haramu.”
Watu wengi wanashindwa katika
ubunifu, utakuta biashara imeanza vizuri na maendeleo ni mazuri, lakini
haonyeshi mabadiliko ama ubunifu ili kuweza kuwavutia wateja wake.
Usafi katika eneo la kazi,
mavazi ama sare za watoa huduma, zawadi na ahadi ndogondogo kwa wateja wa kila siku
ama kauli nzuri pia ni kitu muhimu sana
kwa mjasiriamali. Hakuna kitu kibaya kama kuwa na kauli mbaya kwa wateja hasa
wateja wa zamani, mtu asiridhike kwa kusema hawa ni wateja wangu hakuna sehemu
nyingine watakayopata huduma nzuri kama hapa, waonyeshe kwa vitendo kuwa wewe ndie
kimbilio lao na si kujisifu tu.
Katika suala la mtaji mwalimu
Ssekajubo alieleza kuwa “Kuanzisha biashara ni suala la maamuzi, ni lazima
uhakikishe unakipenda kile unachokifanya na uwe na njaa ya mafanikio.
“Watu wengi pesa ndiyo
wanaita mtaji, lakini kwangu mtaji ni shauku ya kufanikiwa na ndicho kitu
kitakachofanya biashara yako ikaendelea na kuleta mafanikio makubwa. Mathalani
umepanga kupata 1,000,000/= kwa mwaka usipate 500,000/= halafu ukasema
inatosha. Ni lazima ujiulize umeshindwa vipi kutimiza malengo yako,” anahoji.
Mafanikio yana njia nyingi,
usiridhike na hatua uliyofikia, elimu ni kila kitu. Usisite kujiendeleza
kielimu na kujua zaidi kuhusu biashara ama huduma unayotoa.
Mjasiriamali hana wivu mbaya
bali ana wivu wa kimaendeleo kwa kutembelea ofisi za washindani wake kibiashara
na kujua siri za mafanikio yao
badala ya kukaa na kunung’unika tu kuwa mambo hayamuendei vizuri.
Wapo watu wanaamini tofauti
kubwa ya pengo kati ya maskini na tajiri ni elimu ya ujasiriamali. Maana ya
imani hii ni kuwa maskini wengi wanashindwa kuendesha biashara kwakuwa hawana
elimu ya ujasiriamali ima kwa kuipata darasani ama kwa kuona.
Matajiri wengi duniani hawana
elimu kubwa, ima waliacha shule wakiwa wadogo ama walishindwa kumaliza elimu ya
chuo kwa kuelekeza nguvu zao katika kutafuta pesa.
Hii maana yake ni kuwa
haihitaji kukaa darasani kujifunza ujasiriamali, bali hata kwa kukaa na watu
wanaojua elimu hii unaweza kujifunza kwa vitendo. Lakini tatizo kubwa
tulilonalo kwa sasa nchini mwetu ni namna gani tutawasaidia wahitimu
wanaotangatanga mitaani bila kazi.
Dhana ya ujasiriamali katika
akili za watu inabaki kuwa ni biashara. Lakini hata huduma inaweza kuwa ni
ujasiriamali. Maana si wanafunzi wote wanaomaliza vyuo ni wahitimu wa shahada
ama stashahada za elimu ya biashara. Bali kuna
wanafunzi ambao wamesoma computer, maendeleo ya jamii, utawala na mawasiliano
ya umma ama uhandisi.
Hivyo kinachopasa kufanywa na
serikali kwa sasa ni kuhakikisha wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi
waliohitimu na si wanafunzi ambao bado wapo vyuoni. Maana wengi hugundua
umuhimu wa masomo kama hayo mara wamalizapo
shahada zao.
Masomo ya ujasiriamali
huonekana kama masomo ya kujazia vyeti hayachukuliwi
kwa uzito wake. Mwanafunzi aliehitimu shahada ya uongozi atakwambia mimi ujasiriamali
utanisaidia nini, lakini hajui kama anaweza
kufungua ofisi na kutoa huduma zinazotokana na masuala ya uongozi wa umma na
kupata ajira bila kutegemea Serikali kumpa ajira.
Yote haya hayafunzwi ama
yanafunzwa lakini wanafunzi hawayachukulii kwa uzito wake. Kimsingi elimu ya
ujasiriamali ndiyo mkombozi wa tatizo la ajira kwa nchi zinazoendelea.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
0713 593894
10/1/2013
Dar es Salaam, Tanzania
No comments:
Post a Comment