Tuesday, January 22, 2013

Kiongozi wa msafara wa Yanga Uturuki, adhalilisha mwandishi wa habari Michael Momburi.


Na MICHAEL MOMBURI 
ACHANA na safari za ndani ya mipaka ya Tanzania. Nimesafiri na Yanga kwa miaka tofauti kwenye ziara za kikazi katika nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia na Misri. Zote hizo nilisafiri na Yanga kwa mafanikio na kupewa ushirikiano wa kiwango cha juu kutoka kwa viongozi. 

Lakini hakuna safari ya kipuuzi niliyowahi kusafiri nje ya nchi na timu ya Tanzania kama hii nilipokuwa na Yanga mjini Antalya, Uturuki. 

Nimetumia neno upuuzi kwa kuwa hakuna msamiati mbadala wa kuelezea majanga niliyokutana nayo Antalya ambayo yamesababishwa na mtu mmoja ambaye alikuwa na masilahi binafsi ikiwemo kujitafutia umaarufu kwa njia ya kugombana na watu, ingawa baadaye niligundua nikutojiamini kwake. 

Kama kawaida ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kupeleka waandishi wake kwenye safari mbalimbali katika kila kona ya Dunia ili kuwapa Watanzania wanachostahili. 

Kampuni yangu ya MCL ilinigharamia kila kitu na nikakwea ndege na Yanga kwenda Uturuki kufuatilia matukio mbalimbali. Lakini baada ya siku tatu nikaingia matatani na mtu anayeitwa Mohammed Nyenje, ambaye alijitambulisha kama kiongozi wa msafara wa Yanga. 

Sitaki kuingia kiundani historia yake kisoka kwa kuwa hata miaka yangu yote ya kufanya kazi jijini Dar es Salaam sikuwahi kumsikia zaidi ya kumkuta Uturuki. 

Ila nina uhakika ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuwa Mkuu wa Msafara wa timu kubwa kama Yanga. 

Pia ilikuwa mara yake ya kwanza kuongoza msafara wa timu kwenda barani Ulaya. 

Nyanje pia ni uhakika ni mchanga sana katika uongozi wa soka kwani ndio mara ya kwanza amejipenyeza kwenye duru hizi. 

Nilitua Uturuki, Desemba 31 siku moja baada ya Yanga kufika huko. Nikalazimika kufikia Elegance Palace karibu na Uwanja wa ndege wa Antalya kwa kuwa hoteli niliyokuwa nimepanga kufikia ya Asteria Sorgun haikuwa na nafasi siku husika. 

Kesho yake asubuhi nikachukua Taxi umbali wa dakika 30 kuifuata Yanga na hapo tayari nilishapata ripoti kwamba hawajafikia tena kule walikopanga kufikia awali hoteli ya Seonu ambako ni karibu na Asteria. Walikwenda Fame Residence ambako ni Kilomita tisa mbele. 

Ikabidi nihudhurie mazoezi nitume ripoti Dar es Salaam kisha nichukue Taxi kwenda Asteria kufuta mpango wangu wa kufikia hotelini hapo kwa kuwa waligoma kushughulikia suala langu kwa mawasiliano ya simu kwa madai kwamba nilikuwa nimechelewa vinginevyo nisingekwenda basi wangekata fedha kwenye kadi yangu ya benki. 

Nilipofika kutokana na umbali ikanilazimu kulala usiku mmoja kwa kuwa ni mbali na ilikuwa gharama kubwa kurudi mjini. Hoteli hiyo iko mkabala na Seonu ambako Yanga ilikuwa ifikie, hoteli hizo mbili zote ni maarufu kwa kupokea watu wa Ujerumani na Ufaransa. 

Usiku huo nikiwa mweusi pekee kwenye mgahawa na ufukwe uliokuwa umejaa Wajerumani zaidi ya 250 nikakumbana na manyanyaso na vituko vya ubaguzi wa rangi kutoka kwa Wajerumani hao, muongoza watalii wa Kituruki aliyeshuhudia ikamuuma akanipeleka kwa uongozi wa hoteli ambao ulionekana kunituliza na kuniomba yaishe kutokana na idadi ya Wajerumani hao kuwa wengi mno hotelini hapo na ndio wanamuingizia fedha asingeweza kufanya chochote. 

Nilipogundua kwamba hata Tanzania haina ubalozi Uturuki nikaripoti kwenye gazeti la Mwananchi kesho yake kwamba nimekumbana na vitendo vya kibaguzi kwenye eneo ambalo Yanga ilipanga kufikia. 

Nyanje alipoona habari hizo gazetini akakasirika akaanza kunifokea mbele ya kadamnasi ya wachezaji bila kuelewa chanzo. Akanishusha kidhalilishaji kwenye gari asubuhi nikielekea mazoezini mpaka wachezaji wakashangaa na wengine wakanitumia ujumbe baadae kunituliza na kuniambia hawajafurahishwa na unyama huo. 

Hapo tayari ameshakwenda kwa kocha na kumjaza maneno kwamba nimeripoti Yanga imefanyiwa vitendo vya ubaguzi wa rangi kitu ambacho hakikuwa kilichoripotiwa. Kocha Ernest Brandts alikasirika baada ya kupotoshwa na Nyanje ambae alionekana kuwa na malengo yake binafsi kwani tangu mwanzo hakuonyesha ushirikiano alipokuwa akiulizwa mambo mbalimbali. 

Pengine alidanganywa kwa kuzozana na Mwanaspoti na Mwananchi yatampandisha chati kwa Wanayanga kitu ambacho hakikufanikiwa, ingawa baadae wachezaji watano wakubwa na baadhi ya wanachama maarufu wa Yanga walinipigia simu na kunitumia ujumbe wakinisisitizia kwamba hata Ofisa Habari, Baraka Kizuguto ambaye alijifanya rafiki yangu wa karibu sana aliongeza chumvi kwenye malumbano hayo ili awe chanzo pekee cha habari za Yanga na kuupa chati mtandao wa klabu. 

Jambo hilo halikumsaidia pia. 
Huo ulikuwa mgogoro wa kwanza wa kipuuzi na safari ikaonekana ya kipuuzi vilevile ingawa sikukata tamaa kutokana na uzoefu na upeo wangu kwenye kufanya kazi na watu aina ya Nyanje. 

Siku hiyo ambayo ilikuwa ni kama siku ya nne tangu Yanga ianze kambi akatangaza hataki kuniona kambini wala mazoezini na akatangazia ni walinzi wa pande zote mbili huku akizidi kumjaza upuuzi kocha kwa kumuonyesha habari zinazoripotiwa na magazeti ya Tanzania kwa kumnukuu bila idhini yake. 

Watu wa karibu na kocha wakanieleza kuwa anaamini mimi ndiye natuma habari hizo wakati hata magazeti yenyewe siyajui na hayana hata jeuri ya kunitoa Mwanaspoti. 

Bado upotoshaji wa bwana Nyanje unazidi kupata umaarufu na sipewi nafasi ya kukutana na kocha nimuelezee uhalisia na hata akikutana na mimi kwenye mechi hataki hata tuonane uso kwa uso. 

Wachezaji walichukizwa na Mwanaspoti kuzuiwa kuingia kambini huku wengine wakijaribu kuchokonoa uhasama huo ufutike kwa kusaidiana na wazalendo wengine lakini bado kocha akawa ameshiba propaganda za bwana Nyanje ambaye alizidi kujisikia aibu zaidi siku ya mwisho kwa jinsi wachezaji wote walivyonikuta uwanja wa ndege wa Antalya wakati timu inaondoka wakaja kunisalimia na kunitaka kupuuzia yaliyonikuta. 

Kituko cha Pili. Baridi. Siku mbili za awali Antalya ilikuwa na baridi kali na mvua ambayo ililazimisha wachezaji kufanya mazoezi na makoti asubuhi na jioni. 

Nikaripoti uhalisia, Nyanje hataki anataka niseme kuna Jua na hali ya hewa safi kitu ambacho ni uongo siwezi kutumwa na kampuni nije kudanganya Watanzania kwa masilahi ya mtu mmoja au kikundi cha watu. 

Mimi sio Kanjanja elewa Nyanje. 
Mbona baadae hali ya hewa ilikuwa nzuri na tukaripoti kwamba hali imetangemaa kwa kiasi ingawa jua lilikuwa likiwaka kwa kuambatana na baridi ambayo wachezaji wote walikuwa wakishinda na makoti. 

Nyanje anataka Yanga isifiwe tu kitu ambacho kwa enzi hizi hakiwezekani ndio maana tunajifadhili wenyewe kila kitu tunapokuwa sehemu yoyote ile kuepuka utegemezi na tabia za Kikanjanja. 

Pengine kuna watu wamempotosha Nyanje na kumjaza upepo kwamba akisifiwa, basi akirudi Dar es Salaam atajipatia umaarufu. 

Upuuzi wa tatu. Mechi za kirafiki. Wakala wa Yanga aliwaahidi mechi tatu lakini siku za awali nilikaa na Ofisa wake akanieleza ugumu waliokuwa wakikumbana nao kupata mechi na Kocha wa Yanga pamoja na Nyanje walikuwa wanajua ukweli. 

Ukweli ni kwamba wakala aliwaambia timu zote kubwa za Ligi Kuu ya Uturuki zimewatolea nje hata baadhi za Ujerumani zilifanya hivyohivyo ndio maana wakaishia kucheza na timu za Daraja la Nne na zile za Daraja la Kwanza za Uturuki, Ujerumani na Uholanzi. 

Nyanje kusikia taarifa hizo zimefika Tanzania akazidi kuweka miiba mwandishi isivuke. 

Alitaka uminywe ukweli ukiwemo ule Arminia Bielefeld ya Daraja la Nne huko Ujerumani kudengua kucheza na Yanga ndio maana kipindi cha kwanza ikachezesha kikosi dhaifu cha watoto kabla ya kuingiza timu halisi kipindi cha pili ambao licha ya kucheza kwa kujifurahisha walisawazisha bao moja la Yanga kushambulia lango la Yanga kwa muda wote. Yanga wanataka Mwandishi atumike kuwajaza upuuzi na sifa za kijinga Watanzania. 

Baada ya kutokea kutoelewana kati yangu na Nyanje, uongozi wa Mwanaspoti ulijitahidi kuweka mambo sawa kwa kuanzia na viongozi wakuu wa Yanga walioko Tanzania ambao walichukulia kama changamoto za kawaida na kukubaliana na Mwandishi aendelee kuambatana na timu lakini Nyanje kwa chuki zake binafsi akazidi kuminya na kumzuia mwandishi kuingia kambini na mazoezini kwa kuweka ulinzi getini mpaka wachezaji wakawa wanashangaa. 

Mwandishi akataka kiwepo kikao cha kuelezana hali halisi ili tusigombane kwenye nchi ya watu kwa kuwa wote ni Watanzania lakini bado kiongozi huyo bila ya kujali gharama kampuni ilizoingia kusafirisha mtu mpaka Uturuki na ni chombo pekee cha Tanzania kilichopo Uturuki akazidi kugoma. 

Pengine alifanya hivyo akijua ndiyo njia pekee ya kutangazwa na kujulikana kwa kuwa pengine huenda asipate tena zali kama hilo la kusafiri na Yanga kama kiongozi. 
Nyanje umechemka. 

Unapaswa kujua kwamba huwezi kuwa maarufu au kupata cheo Yanga au kufanikisha mambo yako kwa kupambana na mwandishi wa habari. 

Tafuta njia nyingine kuuza jina lako kwa sera na kuifanyia Yanga mambo ya maendeleo, wenzako hawakutoka kwa njia za kibabaishaji. 

Ni upuuzi kulumbana na mwandishi kutoka chombo kimoja cha habari na kibaya zaidi mkiwa ugenini. 

Katika hali ya ubinadamu, wa kawaida hivi kweli watu wa taifa moja mnakorofishana. 

Hata Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema dhambi ya ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu. Ukila mara moja huwezi kuacha. 

Haikusaidii zaidi ya kufunua upeo wako mbele ya watu wenye fikra chanya ambao wanakutafsiri hasi. 

Popote pale unapokuwa ugenini na Watanzania wenzako unapaswa kuonyesha uzalendo na ushirikiano kwa kuwa siyo watu wote tuko kwa ajili ya Watanzania ambao ni mashabiki na haohao wasomaji wa gazeti wana haki ya kupata ripoti ziwe chanya au hasi ili waelewe hali halisi. Kuna matukio mengi ya aibu yalikuwa yanajiri Uturuki. 

Yanga kwenye mechi ilikuwa haina daktari wake binafsi, wachezaji waliokuwa hawachezi ndio walikuwa wakisaidiana na meneja Hafidh Saleh kusaidia wachezaji waliokuwa wanaumia uwanjani na hakuna huduma waliyokuwa wakipata zaidi ya kusuguliwa na barafu. Mfano mzuri ni kwenye mechi na Arminia yalitokea matukio kadhaa ikiwemo Mbuyu Twite kuumia lakini alisaidiwa hivyo hivyo kimagumashi. 

Gari la wagonjwa lilikuwepo lakini hakukuwepo daktari wa kutoa huduma ya kwanza. Je Nyanje haoni hii ni kuhatarisha maisha ya wachezaji. Hayo tuliyamezea lakini Nyanje anathubutu kukurupuka na kuifukuza Mwanaspoti kambini kwamba inairipoti vibaya Yanga. 

Ingawa habari za awali zinasema ilikuwa hakuna jinsi zaidi ya kuifukuza Mwanaspoti kambini kulinda masilahi ya wakubwa akiwemo Nyanje ambao walipendekeza Yanga ipige kambi Uturuki. Ingebaki ingetibua ukweli wa mambo mengi yaliyokuwa yamejificha. 

Narudia tena sikuwahi kukutana na vitimbi nilivyokutana navyo kwenye kambi ya Yanga katika safari zote nilizowahi kusafiri na klabu za Tanzania pamoja na timu za Taifa nje ya nchi kwa miaka kumi mfululizo. 

Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingilia uhuru wa chombo cha habari ndio maana kwa kutaka kuwa huru zaidi Kampuni ya Mwananchi imekuwa ikigharamia kila kitu cha waandishi wake wanaokwenda popote Duniani na ndicho kilichonifanya kuishi kwa amani baada ya udhalilishaji wa Nyanje. Nyanje ana roho ambayo nashindwa kuielekezea. 

Yanga inasafiri kwa basi kubwa tu na ambalo lilikuwa halijaa kwenda kucheza mechi kilomita 60 mpaka 300 nje ya mji kabisa lakini anazuia hata mwandishi kuambatana kwenye basi moja inabidi kuchukua Taxi kwa gharama kufuata msafara nyuma mpaka utakapofika ndio uanze kupatana na dereva ambayo kwa maisha ya Ulaya ilikuwa ikigharimu fedha nyingi kwa kuwa madereva walikuwa wanataja fedha nyingi wakitumia mwanya wa mimi kutofahamu mazingira. 

Hakukuwa na athari yoyote ya mwandishi kupanda basi la Yanga kwenda umbali wa kama Dar es Salaam na Mikumi Morogoro tena kushuhudia mechi ya kirafiki ujue Nyanje ana roho ya aina gani na anatoa picha gani kwa Yanga mbele ya jamii. Lakini Watanzania walipata matokeo bila matatizo kupitia Mwanaspoti yao. 

Pengine ningekuwa nimesafirishwa kwa gharama za Yanga ningefia Uturuki kutokana na Nyanje alivyoonyesha kutokuwa na thamani utu na uzalendo pengine angenitelekeza kabisa mitaani na mwili wangu usionekane kabisa hasa ukizingatia Tanzania haina hata ubalozi Antalya. Mungu saidia nimetua salama Dar es Salaam jana alfajiri ila sijawahi kuona upuuzi kama huu wa Nyanje alionifanyia Uturuki. 

Hata Waisraeli na Wapalestina wanachukiana lakini si kwa kiwango hicho. Nyanje jifunze utu umaarufu hauji kwa kugombana na Michael Momburi shawishi Wanayanga kwa njia nyingine.
Chanzo: gazeti mwanaspoti

No comments:

Post a Comment