Monday, January 28, 2013

CHADEMA wajigawa kimajimbo kuonyesha umuhimu wa kuwa na serikali ya majimbo.

 Mbunge wa jimbo la Ubungo John Mnyika ni miongoni mwa viongozi vijana wa chama hicho wenye mvuto kwa wananchama wengi wa chadema.

 Chadema NEC wakisema peeeoopleeee poweeerrr katika ukumbi wa Diamond Jubelee jana.

 Aliekuwa naibu katibu mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi na diwani wa Babati vijijini Lawrence Tara akikabidhiwa kadi ya CHADEMA kuashiria kujiunga na chama hicho jana.


Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA ambae pia ni naibu katibu mkuu wa chama hicho pia ni miongoni mwa viongozi wenye mvuto sana. Hapa akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho jana.


Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe amesema chama chake kinaunga mkono wananchi wa mikoa ya kusini kuhusu suala la gesi na kuweka wazi kuwa ifike wakati kila mkoa ujivunie rasilimali yake.

Akizungumza katika mkutano wa dharura wa baraza kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam jana Mbowe aliweka wazi msimamo wa chama chake na kusisitiza suluhisho la matatizo ya ugawanyaji finyu wa rasilimali za taifa ni kuleta serikali ya majimbo.

Kwa kudhihirisha hayo Mbowe amekigawa chama chake katika majimbo kumi ambayo yatakuwa yanafanya maamuzi kwa kujitegemea bila kuingiliwa na makao makuu.

Tumeamua kuwa mfano kwa serikali, tunagawa majimbo ili kuondoa dhana kuwa makao makuu yanaamualia mambo ya msingi mikoa. Kwa kufanya hivyo tutaondoa dhuluma inayofanywa na serikali kuu kwa kuwa watu wachache wa Dra es Salaam ndiwo wanaofaidi rasilimali nyingi zilizopo hapa nchini kwa kukaa tu Dar es Salaam wanavuna rasilimali mikoani na kuzuleta hapa halafu wanazichakachua.

“Angalia mkoa wa Geita, mgodi wa Geita unazalisha dhahabu nyingi kuliko migodi yote Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika, lakini Geita ndiyo mkoa maskini kuliko mikoa yote. Watu wa Mtwara na Lindi wana haki kufanya walichofanya kwani ni haki yao,” alisema Mbowe.

 Akifafanua mpango mkakati wa kuchukua nchi mwkaa 2015 mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Mbowe alisema chadema imelenga kufanya mabadiliko ya uongozi kuanzia ngazi ya taifa kwenda katika majimbo na kukipanga upya chama hicho kwa mustakabali wa taifa. “Mtakumbuka kwamba wakati tunakianzisha chama chetu, tulizungumzia sera ya majimbo na kuainisha kazi zake…sasa tumeanza kupanga kazi zenyewe kwa kugawa majukumu katika kanda kumi. “Tunataka tuishi vile tunavyosema kwa kuwa katika miaka mingi ya kuwa chini ya uongozi wa serikali ya CCM, wananchi wamekuwa wakiamriwa mambo yao na kundi dogo la watu wanaojikusanya sehemu moja ya nchi, hilo kwetu si mfano bora wa uongozi,” alisema.

Mbowe aliongeza kuwa katika miaka 20 ya kuhimili misukosuko ya kisiasa chama hicho kimejifunza mengi na sasa kiko tayari kushika dola ndio maana wameanza kugawa majukumu kwa wananchi kupitia uongozi wa kikanda. Alisema kuwa wamejiandaa kwa mashambulizi ya aina zote na sasa jukumu kubwa la kila kanda litakuwa ni kuhakikisha kila mwananchi anaiunga mkono CHADEMA katika eneo atakalokuwa.
Mwenyekiti huyo alitaja kanda hizo na mikoa husika kuwa ni
1.    Kanda ya Ziwa Magaharibi (Mwanza, Geita, Kagera),
2.    Ziwa Mashariki (Mara, Simiyu, Shinyanga),
3.    Ziwa Magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi)
4.    Kati (Singida, Dodoma, Morogoro).
5.    Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Ruvuma, Iringa),
6.    Kusini (Lindi na Mtwara),
7.    Mashariki (Pwani, Dar es Salaam na Tanga),
8.    Kaskazini (Kilimanjaro, Manyara, Arusha),
9.    Pemba na Kanda ya Unguja.

Mbowe alisema katika kuhakikisha vikosi hivyo vinafanya kazi zake vizuri, kila kanda itajengewa ofisi, kununuliwa magari, pikipiki na vifaa vyote vya ofisini na za mikutano. “Lengo la mkakati huo pia ni kuhakikisha CHADEMA inasimama katika chaguzi zote bila kupingwa…tunataka CCM ndiyo ipingwe katika chaguzi na hili tutalifanikisha,” aliongeza.

Katika suala zima la Muungano, Mbowe alisema uwepo wa serikali tatu hauepukiki kwa kuwa tayari Tanzania Visiwani wameshakuwa na serikali yao hivyo ni jukumu la Watanzania Bara kupata serikali ya Tanganyika na kisha kuwepo na serikali ndogo ya Muungano. Alisema serikali tatu inawezekana ikiwa viongozi wataacha unafiki wa kusema muungano utavunjika huku tayari wakitoa uhuru wa Zanzibar kuwa na Rais, bendera na wimbo wao ya taifa. Tunawaunga mkono wenzetu Wazanzibar katika kupigania uhuru kamili na kwa sasa sisi ndio tunaoonekana wa ajabu kushindwa kuuliza serikali ya Tanganyika,” alisema.

Mbowe pia aligusia tume huru ya uchaguzi akisema serikali ihakikishe Watanzania wanapata tume hiyo kwa kuwa tayari hata viongozi wa chombo hicho wameshatoa maoni na kutaka wapewe uhuru wa kufanya kazi.
Alisema serikali kama inafikiri kuwa CHADEMA itaingia katika uchaguzi wa 2015 ikiwa chini ya tume iliyopo sasa watakuwa wanajidanganya na badala yake watalazimisha upatikanaji wa tume hiyo.
Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania
kidojembe@gmail.com
29/01/2013



No comments:

Post a Comment