Monday, January 28, 2013

Kombe la mataifa Afrika lilianza na timu tatu mwaka 1957...

Kombe la Mataifa ya Afrika lililoanzishwa mwaka 1957 limeongezeka umaarufu katika macho ya wapenda soka si barani Afrika tu bali dunia nzima, kwani vilabu vya mpira wa miguu hasa barani Ulaya hutumia michuano hii kuchukua wacheaji wa kuwasaidia kwenye timu zao.

Kombe hili lilianza kwa kushirikisha timu tatu tu nchini Sudan lakini sasa kuna timu 16 zinazowania kombe hilo linaloshikiliwa na timu ya Zambia lililobeba kwa mara ya kwanza mwaka 2012.

Nchi ya Misri ndiyo ya kwanza kunyanyua kombe hilo nchini Suda baada ya kuwafunga Ethiopia magoli 4-0 katika fainali, na hiyo imekuwa kama nyota njema kwa nchi ya Misri kuendeleza ubabe wa soka barani Afrika kwa kuchukua kombe hilo mara saba tangu kuanzishwa kwake mwaka huo wa 1957.

Orodha ya timu zilizochukua kombe la mataifa ya Afrika ni kama ifuatavyo:

1957: katika timu nne zilizothibitisha ushiriki Afrika Kusini ilijitoa katika mashindano na kuzibakisha timu tatu za Misri, Sudan na Ethiopia. Misri wakawa mabingwa wa kwanza wa kombe hilo kwa kuwachapa Ethiopia 4-0 katika fainali.

 1959 : Misri walichukua ushindi kwa mara ya pili mfululizo wakiwa nyumbani katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu tatu tu za Sudan, Ethiopia na wenyeji Misri. Katika fainali Ethiopia walikubali uteja kwa mara ya pili kwa kulazwa 4-0.

1962 : Ethiopia waligoma kugeuzwa kichwa cha mwendawazimu na Misri kwa kutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kuichapa Misri 4-1 katika muda wa nyongeza baada ya dakika tisini za kawaida kuisha kwa suluhu. Mchezaji wa Ethiopia Menguistu Worku, ndie alieiwezesha nchi yake ya Ethiopia kuwa wafalme wa soka barani Afrika kwa mara ya kwanza kwa kuingiza magoli mawili peke yake katika dakika za nyongeza. Tunisia na Uganda zilishiriki kwa mara ya kwanza na kufanya idadi kutoka tatu mpaka tano

1963 : Wenyeji Ghana waliutumia vema mji wa Accra kwa kunyakua kombe hilo mara ya kwanza kwa kuichapa 3-0 Sudan katika fainali. Mwaka huo timu ziliongezeka na kufikia sita,

Kadhalika fainali za mwaka hu rikodi ya mabao 6-3 iliyowekwa na Misri dhidi ya Nigeria ndiyo idadi kubwa ya magoli iliyowahi kufungwa katika mechi moja ya michuano hiyo ya kombe la Afrika mpaka sasa.

1965: Ghana waliendeleza ubabe kwa kuwaaibisha wenyeji Tunisia kwa mabao 3-2 kwenye fainali katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida kuisha kwa suluhu. Mwaka huu wa 1965 timu mbili za DRC Congo na Ivory Coast ziliongezeka.


1968 : Congo DRC walinyakua ubingwa wa Afrika kwa mara ya kwanza nchini Ethiopia kwa kuifunga Ghana walioingia kwenye hatua ya fainali kwa mara ya tatu mfululizo tangu kuanza kushiriki mwaka 1963, bao pekee la Pierra Kalala ndilo lililozamisha ndoto za Ghana kuchukua kombe hilo mara ya tatu mfululizo.

1970: Kwa mara nyingine tena Ghana walinyang’anywa tonge mdomoni na Hassabou el Saghir katika fainali iliyoisha kwa Ghana kulala bao 1-0. Hii ilidhihirisha kuwa kwa kipindi hicho Ghana ndiyo ilikuwa timu bora ya Afrika inayocheza soka la hali ya juu mpaka kufanikiwa kuingia fainali za Afrika mara nne mfululizo na kufanikiwa kushinda mara mbili mfululizo, yaani mara ya kwanza waliposhiriki na mara ya pili kushiriki


1972:  Kwa mara ya kwanza na mwisho nchi ya Congo Brazzaville kuchukua kombe la Afrika ni mwaka huo wa 1972 nchini Cameroon katika mji wa Yaounde ambapo mchezaji wa Congo Brazzaville Micahel M’Bono alitumbukiza wavuni mabao matatu peke yake na kuitoa kichwa chini Mali kwa mabao 3-2.

1974: Huu ndiyo mwaka pekee katika historia za michuano ya kombe la Afrika mchezo wa fainali kurudiwa, ambapo katika mchezo wa kwanza DRc Congo walifungana 2-2 na Zambia nchini Misri, kutokana na sababu zisizozuilika mchezo uliahirishwa na kuchezwa siku mbili baadae.

Katika mchezo wa pili Zambia walilala kwa mabao 2-0 hivyo DRC Congo kuwa mabingwa kwa mara ya pili tangu walipochukua kwa mara ya kwanza mwaka 1968 nchini Ethiopia. Mchezaji wa DRC Congo Mulamba Ndaye ndie alieibuka kidedea kwa kuweza kuifungia mabao yote ya usindi katika mechi zote mbili, yaani ile ya kwanza iliyoisha kwa 2-2 na ya pili iliyorudiwa ya mabao 2-0.

1976: Haya ndiyo mashindano ya pili na ya mwisho kuamuliwa kwa mfumo wa ligi na Morocco kushinda kwa point moja mbele ya Guinea baada ya timu hizo kutoka suluhu ya 1-1 katika mechi ya mwisho nchini Ethiopia. 

1978: Ghana walichukua kikombe kwa mara ya tatu nyumbani kwao Accra, baada ya mchezaji wao Opoku Afriyie kutumbukiza mabao mawili katika fainali dhidi ya Uganda walioingia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza hivyo kuoshia nafasi ya pili kwa kufungwa 2-0.

1980: Nigeria walitumia vema uwanja wa nyumbani kwa kuichapa Algeria mabao 3-0 katika fainali iliyotawaliwa na mchezaji wa Nigeri Segun Odegbami kufunga mabao yote matatu, na kuwa washindi wa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.

Itakumbukwa katika mwaka huu Rais wa TFF Leodger Tenga aliongoza kikosi cha Taifa Stars nchini Nigeria kushiriki kwa mara ya kwanza na mara ya mwisho michuano hii.


1982: Ghana walifanikiwa kuchukua kombe hili kwa mara ya nne dhidi ya Libya kwa mikwaju ya penalt 7-6 na kuweka historia kuwa fainali za kwanza  za kombe la Afrika kuamuliwa kwa mikwaju ya penalt. Katika fainali hizo ndipo jin ala Abedi Pele alietokea ‘benchi’ na kuonyesha kipaji cha hali ya juu mbali ya umri wake mdogo hivyo kuwa nyota wa soka barani Afrika na dunia kuanzia mwaka huo.

1984:  Kwa mara ya kwanza Cameroon walichukua kikombe hicho katika fainali iliyowakutanisha na Nigeria ambapo walishinda 3-1.

1986: Cameroon walifanikiwa kuingia fainali kwa mara ya pili lakini wakafungwa na Misri kwa mikwaju ya penalt mbele ya mashabiki 100,000 nchini Misri kwenye uwanja wa Cairo Stadium.

1988: Kwa mara ya tatu mfululizo Cameroon waliingia fainali lakini walionyeshwa upinzani mkubwa na Nigeria kabla ya mchezaji wa Cameroon Emmanuel Kunde kuifungia timu yake kwa penalt pekee hivyo Nigeria kulala 1-0 mjini Casablanca.

1990: Algeria iliifunga Nigeria 5-1 hivyo kutawazwa mabingwa wa soka barani Afrika kwa mwaka huo wa 1990.


1992: Kombe la Afrika liliongeza mwamko na kufikia timu 12, kichekesho kilikuwa siku ya fainali ambapo Ivory Coast iliilaza Ghana kwa penalt 11-10 baada ya muda wa kawaida na muda wa nyongeza kuisha kwa suluhu nchini Senegal.

1994: Zambia walifika fainali ingawa walipoteza karibu kikosi chote katika ajali ya ndege miezi kadhaa nyuma nchini Gabon, lakini Nigeria haikuwaonea huruma baada ya kuwatundika goli 2-1 katika fainali hiyo ambapo goli zote mbili za Nigeria ziliingizwa kimiani na Emmanuel Amunike aliekuwa akiwika sana kwa miaka hiyo.

1996: Kwa mara ya kwanza fainali za kombe la Afrika lilishirikisha timu 16 cha kutia matumaini nchi ya Afrika Kusini ilirudi katika michuano baada ya matatizo ya ubaguzi wa rangi nchini mwao kuwatoa katika fainali za kwanza kabisa mwaka 1957.

Mark William wa afrika Kusini aliwakatili Tunisia kwa kutumbukiza goli mbili peke yake hivyo Tunisia kulala 2-0 na afrika kusini kuchukua kikombe kwa mara ya kwanza.
1998: Kuonyesha wana kiu ya michuano hiyo Afrika Kusini waliingia fainali kwa mara ya pili mfululizo lakini Misri waliwatuliza na kuwachapa 2-0 mjini Ouagadougou.

2000: Nigeria kwa mara ya kwanza waliondoa kasumba ya wenyeji kufungwa katika fainali baada ya kuichapa Cameroon kwa mikwaju ya penalt 4-3 baada ya suluhu ya 2-2 katika dakika za kawaida na nyongeza.
 

2002: ilikuwa ni nchini Mali ambapo Cameroon walitawazwa mabingwa wa Afrika kwa mikwaju ya penalt dhidi ya Senegal iliyokuwa na vinara wa soka kama El-Hadji Diouf.

2004: Wenyeji Tunisia walibeba kikombe cha Afrika baada ya kuwachapa Morroco 2-1.

2006: Misri walitawazwa mabingwa kwa mara nyingine baada ya kuwachapa Ivory coast waliokuwa na kikosi imara kilichoongozwa na Didier Drogba.

2008: Misri waliendeleza ubabe na kunyakua ushindi wa Afrika tena baada ya mshambuliaji wao hatari Mohammed Aboutrika kuwainua mafarao hao dakika 13 kabla ya mchezo kuisha hivyo Ivory Coast kulala 4-1 dhidi ya Misri kwa mara ya pili mfululizo.

2010: Ilikuwa ni mwaka wa maajabu katika michuano hii baada ya
Misri kuwa taifa la kwanza kushinda kombe hilo kwa mara tatu  mfululizo ilikuwa ni mjini Luanda dhidi ya Ghana na kuifanya Misri mababa wa soka la Afrika kwa kuchukua kikombe hicho kwa mara ya saba.

2012: Zambia walinyakua kikombe hicho kwa mara ya kwanza baada ya tambiko lao mjini Gabon katika eneo walilopoteza wachezaji wako kwa ajali ya ndege. Mikwaju ya penalt 8-7 dhidi ya Ivory Coast iliamsha furaha ya wapenzi wa soka barani Afrika kwani watu wengi walikuwa wakiwaonea huruma Wazambia kutokana na dua walizokuwa wakiomba ili kuweka historia ya michuano hiyo.


Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania
29/01/2013

No comments:

Post a Comment