Wednesday, January 30, 2013

Mungu niepushie kuomba...


Kusema nisaidie, kwangu neno takilifu
Mola wangu nepushie, kulisema menikifu
Hekima nizidishie, moyo usiwe dhaifu
Kuomba kwaniumiza, madhali ninazo nguvu

Japo mimi masikini, nafsi yangu naisifu
Sitoranda mitaani, jina liwe maarufu
Nikaitwa maluuni, kwa kukodolea sefu
Za matajiri wachoyo, wanaosimanga watu

Mungu amenipa nguvu, na viungo kamilifu
Roho yangu si legevu, naushika msahafu
Naapa kwa wapumbavu, waliojipanga safu
Wakingoja nianguke, waruke wakinicheka

Kusimbuliwa sitaki, sipendi hiyo harufu
Bora kukosa riziki, kuliko kujikashifu
Mola ndie mstahiki, kwa yoyote mausufu
Hutenda cha madhukura, kisha akabaki kimya

Ni bora nikalimbika, kesho nipate sufufu
Watu watanikumbuka, si nyinyi wababaifu
Wanangu wakinizika, warithi mali nadhifu
Haitokuwa ya wizi, wala ya kudhulumiwa

Ninausulubu mwili, kwa kula mlo hafifu
Ili nitafute mali, kwa hasira kama pofu
Kuepuka udhalili, wa kuomba kiudufu
Mola aniepushie, kuwa mfano mbaya

Kaditama beti saba, tungo hii maarufu
Meandika kwa mahaba, si tambo na majisifu
Kuiandika katiba, hako wa kunikashifu
Iwe mbaya kwa kusoma, na maudhui sharifu

HAFIDH KIDO
Dar es Salaam, Tanzania
30/01/2013

No comments:

Post a Comment