Friday, January 11, 2013

Shaaban Robert, unamjua?

                         Shaaban Robert, picha yake hii inatumika sana katika majalada ya vitabu vyake.

                      Hili ndilo kaburi la shaaban Robert lililopo Vibambani Machui mjini Tanga.


Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 Januari, 1909 katika kijiji cha Vibambani kata ya Machui mjini Tanga. Jina lake linawakilisha taaluma ya fasihi na lugha ya Kiswahili katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

Asili ya jina Robert ni mwajiri wa babu yake ambae aliitwa 'Roberto' asili yake kutoka Italy. Bibi yake Shaaban alipokuwa na ujauzito alikuwa akianika uduvi katika ufukwe wa bahari ya hindi mjini Dar es Salaam, eneo la kurasini katika shamba la minazi. Wakati uchungu ulipomjia alijifungua hukohuko ufukweni kwa msaada wa wanakijiji.

kutokana na kuzaliwa ufukweni babu yake Shaaban alipewa jina la Ufukwe. Lakini babu yake Shaaban alipokwenda kazini na kumpa taarifa mwajiri wake mzungu juu ya kupata mtoto wa kiume, mzungu yule kwa furaha na namna alivyoshibana na babu yake Shaaban alitaka mtoto yule apewe jina lake yaani 'Roberto'.

Hivyo jina la ufukwe likafa akawa anaitwa Roberto, hata alipomzaa Shaaban alipohamia mjini Tanga katika shamba la Mikonge Amboni, mzee Roberto aliendelea kutumia jina hilo na mwanae Shaaban akawa akiitwa Shaaban Roberto, lakini alipoanza shule kwa kuwa alisoma shule za Kiingereza walimu wake wakawa hawawezi kutamka 'Roberto' wakawa wanamwita 'Robert' mwanzoni Shaaban alikuwa akiandika jina lake kama Shaaban Roberts, lakini alipokuwa mtu mzima akawa akijiita Shaaban Robert.

Alitumia maisha yake katika kuandika fasihi ya Kiswahili kuanzia mashairi, riwaya, tamthilia na kila fani iliyohusu fasihi andishi. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili wanasema tangu kufariki kwake tarehe 20 june, 1962  hakujatokea mtu yeyote aliekitendea haki Kiswahili kama alivyofanya Shaaban Robert katika uhai wake.

Baada ya kumaliza darasa la 11 Shaaban aliajiriwa na Serikali ya kikoloni wakati huo ikiitwa Tanganyika akiwa karani. Kuanzia mwaka 1926 mpaka 1944 alikuwa afisa forodha katika bandari mbalimbali nchini hasa Pangani na Bagamoyo, kuanzia mwaka 1944 mpaka 1946 alihamia mjini Morogoro katika ofisi ya mbuga za wanyama. Na kuanzia mwaka 1946 mpaka 1952 alihamia Tanga katika ofisi ya kupima ramani alipostaafu utumishi wa umma.

Kutokana na umahiri wake wa kuandika chama cha TANU kilimtumia katika shughuli zake akiwa mhamasishaji kwa kutumia kipaji cha ushairi. Mwalimu Nyerere alivutiwa sana na umahiri wa Shaaban Robert hata katika upande wa ushairi uliotukuka.

Katika tuzo alizopata kutokana na umahiri wake wa kuandika ni Margaret Wrong Memorial Prize for Writing, kadhalika utawala wa kiingereza ulimpa heshima ya uraia nchini Uingereza kwa tuzo ya Member of the British Empire (MBE).

Katika maandishi yake shaaban Robert alilenga sana utu, nafasi ya mwanamke katika jamii, ukombozi wa bara la Afrika, kukuza lugha ya Kiswahili, na maendeleo. Mwalimu Nyerere alimpa tuzo ya fasihi iliyotukuka kutokana na mchango wake katika jamii ya Tanganyika na Tanzania baadae, lakini tayari alikuwa ameshafariki.

Mpaka anafariki kwa maradhi ya moyo na upungufu wa damu, Shaaban Robert alifanikiwa kuandika vitabu 24 kwa lugha adhimu ya kiswahili, na mpaka sasa kazi zake zinazidi kukusanywa na  taasisi ya uchunguzi na kukuza Kiswahili (TUKI) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Kipo kitabu cha 25 ambacho kilitolewa miaka ya karibuni mabacho kina barua alizokuwa akiandikiana na jamaa zake.

Katika kitabu hicho kumeonekana uwezo mkubwa aliokuwa nao Shaaban Robert katika kuchagua maneno na ufasaha wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Kwani watu wengi walidhani Shaaban Robert hakuwa mjuzi wa lugha ya Kiingereza lakini katika barua zake zipo ambazo aliziandika kwa lugha hiyo ya kigeni kwa ufasaha wa hali ya juu.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
0713 593894/ 0752 593894
11/1/2013
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment